Bukobawadau

MAKUBWA KUTOKA KWA WANANCHI WA MTWARA

 Muoonekano wa Jengo la Mahakama ya mwanzo iliyochomwa moto usiku wa kuamkia leo
Nyumba ya  Mwenyekiti wa CCM Mtwara, ndugu Sinani ikiwa imevunjwa tu vioo.
Hii ndo Nyumba ya Mbunge Hawa Gasia iliyovunjwa vioo na kuchomwa moto
Kwa kile kinachoaminika kuwa ni kukua kwa mgogoro wa Gesi Mkoani Mtwara na Kusini kwa ujumla, usiku wa kuamkia leo Mahakama ya Mwanzo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani imeteketezwa kwa moto.
Pikipiki 17, magari 8 na nyumba kadhaa zapigwa moto wilayani Masasi 
Mbunge wa Masasi (CCM), Mariam Kasembe
Hali ya kuzidi kupotea kwa utulivu ambao Tanzania imekuwa ikijivunia kwa miaka mingi, imeendelea kujidhihirisha leo baada ya vurugu kubwa kuzuka mjini wilayani Masasi, mkoani Mtwara, baada ya baadhi ya wananchi kufanya maandamano makubwa pamoja na kuchoma moto baadhi ya mali za viongozi, chama na serikali kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kuchoshwa na vitendo vya uonevu dhidi yao.
Miongoni mwa mali zilizochomwa moto katika tukio hili, ni pamoja na nyumba mbili za mbunge na waziri wa zamani bi. Anna Abdallah moja iliyo katika eneo la Mtambi na nyingine katika eneo la Jeddah, pamoja na nyumba ya mbunge wa sasa wa jimbo la Masasi, Mariam Kasembe.
Kwa mujibu wa shuhuda wetu katika vurugu hizo, chanzo cha fujo hizo kinaelezwa kuwa ni mzozo baina ya Askari Polisi na madereva wa pikipiki za kubebea abiria maarufu kama Bodabora, mzozo ambao ulianzia eneo la stendi ya mabasi mjini hapo.
“Kulikuwa na mzozo baina ya askari na waendesha bodaboda, na ilikuwa katika eneo la stendi ya mabasi hapa Masasi, sasa baada ya mzozo huo ndio vijana wakaanza kujikusanya na kuanza maandamano hayo ambapo moja kwa moja walienda kuanza kufanya uharibifu huo” ameeleza shuhuda wetu.
Maandamano hayo ambayo yalishindwa kudhibitiwa na vyombo vya usalama mapema kabla hayajapamba moto, yalielekea nyumbani kwa mama Anna Abdallah, ambapo walichoma nyumba zake hizo mbili, pamoja na kupora mali kadhaa zilizokuwa kwenye nyumba hizo, kisha wakaelekea kwenye nyumba ya mbunge wa sasa wa jimbo hilo ambaye inadaiwa kuwa vijana hao wamesema amekuwa hawasikilizi wala kuonyesha kushughulikia matatizo yao.
“Hawakuandamana kwenda kwa mbunge kwa lengo la kwenda kupeleka malalamiko yao ili ayafanyie kazi, bali kwenda kufanya hicho walichokifanya kwani wamekuwa wakidai kuwa mbunge wao ni muuza sura tu asiye na msaada wowote kwao wala jimboni kwao kwa ujumla” ameendelea kueleza shuhuda wetu.
Mbali ya hayo, wananchi hao pia wamechoma moto ofisi ya Maliasili ya Wilaya ya Masasi, jengo moja katika ofisi za halmashauri ya wilaya hiyo, ofisi za chama tawala nchini, zilizoko wilayani huko. Aidha, shuhuda huyo ameendelea kusema kuwa, takriban pikipiki 17 na magari 8 vyote vikiwa mali ya serikali na watu binafsi, vimeteketea kwa moto.
Shuhuda huyo ameeleza pia kuwa, wananchi hao walivamia gereza lililoko mjini hapo na kufungulia wafungwa waliokuwemo ndani ambao inadaiwa baadhi yao pia walijiunga na waandamanaji hao katika kuzidi kusababisha uharibifu.
Kana kwamba vijana hao walikuwa wakijua wanachokifanya, imeelezwa kuwa, walifanya pia mpango wa kuharibu daraja linalounganisha wilaya yao na ile ya Newala, kwa lengo la kuweka kizuizi kwa askari waliokuwa wakitokea huko kuja kuongeza nguvu kukabiliana nao.
Jitihada zaidi za kuwasiliana na mamlaka za kiusalama wilayani humo zinaendelea kufanywa na kikosi cha Jukwaa Huru na tutawajulisha wasomaji wetu wapendwa pindi mawasiliano yakikamilika

SOURCE JUKWAA HURU.
Next Post Previous Post
Bukobawadau