Bukobawadau

HII TUMEIPENDA KUTOKA KWA MJENGWA:KWENYE NCHI YA KUSADIKIKA KUNA MAFRURIKO YA HABARI!

Watoto wakisoma Magazeti
Ndugu zangu,
Kwenye nchi ya Wasadikika kuna mambo mengi ya ajabu. Wasadikika kwa sasa wako kwenye 'hatari kubwa' ya kuzama kwenye mafuriko ya habari.

Haijapata kutokea kwenye Nchi ya Wasadikika kuuanza mwaka na mafuriko ya habari. Kwa sasa Nchi ya Kusadikika ina habari nyingi kiasi cha wahariri kwenye vyumba vya habari kufikiria kuongeza kurasa za magazeti. Na kwenye redio kuongeza dakika za matangazo.
Na kawaida ya mafuriko huja na mazagazaga. Ndio, kwenye mafuriko haya ya habari kuna ' mazagazaga' ya habari pia.
Na Wasadikika wanapenda sana ' mazagazaga'. Ni zile habari zenye kuzagaa mitaani na mara nyingi huwa hazina vichwa wala miguu. Na nyingine haziandikwi kabisa magazetini wala kutangazwa redioni- Ni mazagazaga tu yenye kuzaa habari pia.
Ndio, mazagazaga ni habari zisizoumiza sana vichwa, maana huna haja ya kifikiri sana na unaweza kuzianzia katikati na hata mwisho wa habari na ukawa na cha kuzungumza. Naam, Wasadikika wanapenda sana mambo ya kuambiwa na yanayotokana na walichosema akina Sadiki.
Hata hivyo, kwenye nchi ya Wasadikika, ukiachana na ' mazagazaga' yanayoelea na ukajitahidi kuzama sana kwenye mafuriko ya habari, basi, unaweza kukutana na habari nzito na za kichambuzi haswa. Habari zitakazokufanya uelewe yale ambayo hukuyaelewa kabla...
Yote hayo kwenye Nchi ya Wasadikika. Nchi yenye mambo ya ajabu.
Maggid Mjengwa,
Dar es Salaam- Jiji kwenye Nchi ya Wasadikika
0754 678 252
Next Post Previous Post
Bukobawadau