Bukobawadau

KWA HILI KIKWETE AUNGWE MKONO

KATIKA hotuba yake ya kufunga mwaka 2013 juzi, Rais Jakaya Kikwete alisema Operesheni Tokomeza Ujangili iliyositishwa kwa muda kutokana na utekelezaji wake kukumbwa na kasoro itaendelea baada ya kukamilika kwa matayarisho ya awamu yake ya pili.

Rais Kikwete alisema kuwa wanakamilisha matayarisho ya kuanza awamu ya pili ya Operesheni Tokomeza Ujangili. Kwamba ni muhimu kuendelea nayo kwani wasipofanya hivyo majangili wataendelea na vitendo vyao viovu.

Alikumbusha kuwa wakati akilihutubia Bunge Novemba 7, mwaka jana, aliagiza ifanyike sensa katika Pori la Hifadhi la Selous. Na kuongeza kuwa sensa imekamilika lakini taarifa yake inatisha.

Kwa mujibu wa rais, kuna tembo 13,084 tu wakati mwaka 1976 walikuwa na tembo 109,419.

Kwa hili, tunamuunga mkono Rais Kikwete na kuitaka serikali iwe makini zaidi katika kutekeleza operesheni hiyo awamu ya pili ili kuepuka makosa ya awali ambayo sasa yanawapa mwanya majangili kutamba.

Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira ilieleza athari mbalimbali za operesheni hiyo, ikiwa ni pamoja na unyanyasaji, uharibifu wa mali na mauaji ya binadamu na mifugo.

Kasoro hizo ndizo zimesababisha rais kutengua uwaziri wa Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi), Dk. David Mathayo (Mifugo na Uvuvi) na Balozi Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii).

Ni ukweli usiopingika kuwa mawaziri hawa walizembea kwa namna moja au nyingine, lakini lazima tukubali kwamba uketelezaji wa operesheni hiyo uliingiliwa pia na majangili ili kudhoofisha dhamira nzima ya serikali.

Tunasema hivyo kutokana na ripoti hiyo kuwataja baadhi ya wabunge na madiwani kuhusika kukwamisha utekelezaji wa operesheni kutokana na wao ama jamaa zao kuhusika moja kwa moja na biashara hiyo.

Hata ndani ya Bunge wako baadhi ya wabunge ambao hoja yao haikujikita kupendekeza kusitisha na kuipanga upya operesheni hiyo baada ya kuonesha kasoro, bali wao walitaka isitishwe kabisa.

Tafsiri yake nini kama hawa si mawakala wa majangili wanaotumika kufanya udalali bungeni bila kujali kuwa wanyamapori wetu wanamalizwa?

Hoja yetu katika hili, tunamshauri rais aongeze umakini katika kuunda kikosi cha kutekeleza operesheni hiyo ili safari hii wakamatwe kweli watuhumiwa magwiji wanaojihusisha na biashara hiyo badala ya kuishia kutesa wanyonge.

Si kwamba tunakataa kuwa Operesheni Tokomeza Ujangili pamoja na matatizo yake haikuwagusa majangili, la hasha! Kazi kubwa imefanyika.

Mitandao hiyo inahusisha watu wa aina mbalimbali, wamo raia wa kawaida, watu maarufu, watumishi wa idara mbalimbali za serikali wakiwamo wa Idara za Wanyamapori na Misitu.

Rais alisema katika operesheni hiyo watu 1,030 walikamatwa pamoja na silaha za kijeshi 18, za kiraia 1,579 na shehena kubwa za meno ya tembo na nyara mbalimbali. Huu ni uthibitisho kwamba majangili wanatakiwa kusakwa kwa gharama yoyote.

Na Ansbert Ngurumo


Next Post Previous Post
Bukobawadau