Bukobawadau

CHIZA DHIHIRISHA WEWE SIO MZIGO

Na Prudence Karugendo
WAKATI Rais Kikwete akielekea kumaliza muda wake wa uongozi wananchi wamechachamaa kutokana na mambo kudorora katika serikali yake. Ikabidi chama tawala, CCM, kiingilie kati na kufanya uchunguzi kuhusu hali hiyo, kikagundua kuwa baadhi ya wasaidizi wa rais, mawaziri, ndio wanaochangia kwa kiasi kikubwa kuufanya uongozi wa nchi kwa sasa uonekane unazorota.
Chama tawala kikawataja majina mawaziri hao, kisha kikawapachika majina mapya ya kiutendaji, mawaziri mizigo, na kumshauri rais aibwage chini mizigo hiyo. Katika mawaziri hao mizigo mmojawapo akawa ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Mhandisi Christopher Chiza, na aliyekuwa naibu wake, Adam Malima.
Lakini kwa mshangao wa kila mwananchi Rais Kikwete akaonyesha kuwa bado anayo imani na mawaziri wake hao walioitwa mizigo, akawarudisha wote kwenye baraza lake la mawaziri pale alipolifanyia marekebisho!
Sasa kwa vile rais kajitenga na wananchi walio wengi, kimsimamo, ingebidi mawaziri hao walioitwa mizigo, lakini rais akaendelea kuonyesha imani kwao, nao walipe fadhila kwa kumsaidia bosi wao wakionyesha imani kwake vilevile. Wabadilike na kutenda mambo yanayokubalika kwa wananchi wakikumbuka kuwa rais aliapa kuwatumikia wananchi kwa uwezo wake wote na kuhakikisha anawaridhisha pasipo na shaka. Hiyo ingesaidia Rais Kikwete na kumfanya amalizie kwa amani muda wake wa uongozi uliobaki.
Katika makala hii nataka nimuangalie Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza.
Pamona na malalamiko mengi yaliyoelekezwa kwake na wakulima, kuna moja kuu ambalo hata mimi nimeliandika mara nyingi bila kuchoka, nalo ni la vyama vya ushirika.
Ieleweke kuwa vyama vya ushirika ndiyo nguzo kuu ya wakulima. Vyama hivyo ndivyo vinavyokiangalia kile anachokizalisha mkulima na kukifanya kimneemeshe kiuchumi. Maana mkulima hawezi kukithamini kilimo kama shughuli hiyo ni ya kumfanya abaki fukara akilima bila kuona manufaa yoyote, hasa pale kilimo chenyewe kinapokuwa si cha chakula.
Ila kwa sasa ushirika unakufa. Na kinachouua ushirika ni uongozi mbovu katika ushirika huo. Ni Pale wanaoaminiwa na wanaushirika na kupewa dhamana ya kuuongoza ushirika wanapowageuka wanaushirika wenzao na kuwa watu wa kuyajali tu matumbo yao na kukiacha kile walichotumwa kukisimamia na kukiimarisha.
Kwa upande huo nataka niutumie kama mfano ushirika ninaoufahamu vizuri wa KCU(`990) Ltd.. Huo ni ushirika ulionilea, ukanisomesha mpaka nikaweza kupata akili za kutambua nini maana ya ushirika. Ingawa ushirika huo kwa sasa hauna fahamu, hauwezi kulea tena wala kumsomesha yeyote!
KCU(1990) Ltd. ni chama kinachokufa katika mazingira ya ajabu! Chama kinachokufa kwa umasikini wakati kinazo mali lukuki na utajiri mwingine wa ajabu!
Pamoja na ukweli kwamba zao kuu (kahawa) linalosimamiwa na chama hicho bado linazalishwa kwa wingi katika maeneo yote yanayounda ushirika huo, bado chama hicho kinavyo vitegauchumi vingi ambavyo vingetosha kukiendesha kwa uimara hata kama zao hilo lisingekuwepo kwa sasa.
Tatizo kubwa lililopo ni kwamba viongozi na watendaji wa chama hicho wamekigeuza pango ambamo viumbe wanaweza wakajineemesha kwa kuishi bila kulifanyia pango hilo ukarabati wa aina yoyote wakiwa wamesahau kuwa pango hilo lina wenyewe!
Matokeo yake vitegauchumi vyote vya chama hicho vinakufa kutokana na kuzalisha kisichoonekana. Wanaonufaika na kidogo kinachopatikana ni viongozi na watendaji wa ushirika huo peke yao, lakini wanaushirika, wenye mali, wanaishia kupata maneno tu ya kwamba chama hakina kitu!
Mfano chama hicho kinamiliki hoteli ya kitalii ijulikanayo kama Lake Hotel, lakini cha ajabu imetelekezwa kufikia kuzalisha shilingi milioni 1 kwa mwaka huku ikiwa imetumia shilingi milioni 150! Hiyo ni kwa mujibu wa moja ya mahesabu ya mwaka yaliyokaguliwa ya chama hicho.
Lakini hatahivyo, pamoja na uongozi wa KCU (1990) Ltd. kuona hali iliyonayo hoteli hiyo ya Lake bado ukashawishika kununua hoteli nyingine iliyojulikana kama Yasillah kwa kiasi kisichopungua shilingi milioni 500! Uongozi haukujiuliza ni kitu gani kiliisibu hoteli kongwe ya Lake na utawezaje kukiepuka kisiisibu na kuifilisi vilevile hoteli hiyo mpya.
Hivyo vyote ni mbali na mali nyingine za chama hicho kama karakhana, majengo, magari, viwanja na mashamba katika sehemu mbalimbali za mkoa wa Kagera, vilivyogeuzwa vichwa vya wendawazimu ambavyo kila mlevi anajifunzia kunyoa!
Kinachoonekana kutiliwa maanani na KCU (1990) Ltd. ni namna uongozi wake unavyoweza kufanya hadaa ili uongozi wa nchi ngazi ya taifa huuchukulie ushirika huo kuwa bado una nguvu na unaweza kujiendesha.
Hivi karibuni uongozi wa chama hicho uliandaa jengo linalodaiwa ni la kitegauchumi cha ushirika huo na kulitayarisha likazinduliwe na rais. Na rais, kwa kutojua kinachoendelea, akalizindua.
Jambo la kushangaza ni kwamba kwa sasa wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wanalalamika kwamba jengo lililozinduliwa kwa mbwembwe nyingi huku rais akiumwagia sifa uongozi wa KCU (1990) Ltd. kwamba walau unacho cha kuonyesha, mpaka sasa bado lipo kama pambo tu bila kuonyesha chochote linalokichuma. Swali wanalojiuliza wanaushirika hao ni kwamba jengo hilo ni kitegauchumi kweli au ilikuwa ni njia ya kumhadaa rais ili aseme Kagera bado kuna ushirika ambao unafanya kazi? Wanauliza kwa nini jengo hilo liwe kitega hewa badala ya kuwa kitegauchumi?
Chama hicho kikuu cha ushirika kinacho kitegauchumi kingine cha Moshi Export. Hicho ni kitengo kinachojitegemea ambacho kazi yake ni kuinunua kahawa ya KCU (1990) Ltd. au kwingineko inakopatikana kahawa na kuitafutia soko nje ya nchi au kokote kuliko na soko zuri. Faida inayopatikana, baada ya kitengo hicho kutoa pesa ya kujiendesha, ndiyo inakuwa mali ya ushirika.
Lakini baada ya KCU (1990) Ltd. kuanza kufilisika uongozi wake umefikiria kukifilisi pia kitengo chake hicho cha Moshi Export! Ikumbukwe kitengo hicho kinajitegemea, na kilianzishwa kwa juhudi za wapenda ushirika bila kutumia hata senti moja kutoka katika chama hicho kikuu cha ushirika.
Jambo lingine linalodhihirisha kuwa uongozi ndio unaoufilisi ushirika huo ni kwamba wakati huu, wanaojiita wajumbe wa bodi ya chama hicho kikuu cha ushirika wanashinikiza waende nchini Burundi eti kwa ajili ya maonyesho yanayofanyika nchini humo!
Pesa inayotakiwa kwa ajili ya safari hiyo haipungui shilingi milioni 23! Wajumbe hao hawakumbuki madeni yanayokikabili chama chao!
Ikizingatiwa kuwa wajumbe hao sio watendaji, na ushirika tayari unaye mtu anayeuwakilisha katika maonyesho hayo ya Burundi, moja kwa moja safari hiyo wanayoilazimisha wajumbe hao inajionyesha kuwa ni ya kwenda kutalii tu bila kujali kuwa anayeumizwa na uamuzi huo wa wajumbe wa bodi ni mkulima, mwanaushirika.
Wakati hayo yakitendeka, tena kwa kufanywa na watu walioaminiwa na wanaushirika na kukabidhiwa majukumu ya kuuongoza, kahawa inawaozea wakulima majumbani kwao kiasi kwamba wengine hawaoni tena faida ya kuivuna, wanaicha iozee mashambani! Chama kikuu kinadai hakina pesa ya kuinunulia!
Hayo yote yanatokea wakati Mrajis Msaidizi wa Ushirika wa mkoa, Rwekiko Nestory Shoros, ambaye bahati mbya au nzuri, ni mweneyeji wa Kagera anayeelewa maana ya kahawa kwa wenyeji wa sehemu hiyo, akiwa anaangalia tu bila kutia neno lolote la kuunusuru ushirika huo.
Na badala yake, wanaushirika wanasema kwamba Mrajis Msaidizi huyo kaishajifanya sehemu ya uongozi wa ushirika huo! Eti yeye anachokijua ni kushiriki vikao vyote vya ushirika, hata viwe vinavyowahusu tu wahudumu ndani ya ushirika huo!
Nilipompigia simu huyo Mrajis Msaidizi ili kuhakikisha jambo hilo kwa kutumia namba ambayo mara zote naitumia kuwasiliana naye, mwanzoni hakupokea, nikamtumia ujumbe wa maandishi hakujibu. Baadaye nikampigia tena akapokea na kusema siyo yeye!
Kwahiyo pamoja na yote hayo, jambo kuu ambalo angelifanya Waziri wa Ushirika, Chiza, na kuwarudishia imani wananchi, ambao wengi wao ni wakulima walio katika ushirika, kuwa yeye sasa amejiondoa kwenye mizigo ni kuhakikisha anauamsha ushirika kutoka kwenye nusu kaputi uliyomo kwa sasa.
La kwanza na muhimu kuliko yote ambalo Chiza angeanza nalo katika jitihada za kuufufua ushirika ni kuhakikisha anamshirikisha Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG), kuvikagua vyama vya ushirika badala ya kuwatumia wale waliozoeleka kuvikagua. Tena hatua hiyo ingeanzia kwa vyama vikuu vya ushirika vilivyojitengenezea majina makubwa miaka ya nyuma ikiwemo KCU (1990) Ltd.
Watakaobainika kuuhujumu ushirika wachukuliwe hatua za kisheria ikiwemo kufilisiwa mali zao zote bila huruma yoyote. Hilo linawezekana, sababu kama wao walio wachache, wanawafilisi bila huruma wanaushirika walio wengi, iweje huruma ijitokeze kwa wao wachache?
Kazi kwako Waziri Chiza, kujiondoa kwenye mizigo au kuendelea kuuzidisha uzito kichwani kwa bosi wako.
Prudencekarugendo@yahoo.com
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau