Bukobawadau

MIZIKI YA INJILI NI BIASHARA NDANI YA HEKALU

Na Prudence Karugendo

MWANAMUZIKI  mmoja, au niseme mwimbaji, kwa vile muziki wa sasa,  hasa huu unaoitwa wa kizazi kipya au Bongo fleva, hauhitaji vyombo vya muziki zaidi ya waimbaji kupeleka mashairi yao studioni na kutafutiwa sauti za kwenye kompyuta, kasema anaachana na muziki huo wa kizazi kipya na kuugeukia muziki wa injili. Kwa uamuzi huo wapo walioona na wengine kudhani kuwa mwanamuziki huyo kaamua kumgeukia Mungu kwa maana ya kuokoka.

Niseme kwamba, kwa mtazamo wangu, sioni kama kuna kitu kuokoka hapo kutokana na muziki wa injili ulivyo,  ambao unatamba kwa sasa. Sababu muziki wa injili ulio sokoni kwa kipindi hiki umekaa kibishara zaidi kuliko kiimani. Kusema ukweli muziki wa injili wa sasa umekaa kibiashara kuliko hata muziki  wa Bongo fleva!

Kwa mujibu wa Injili, mwongozo wa imani ya Kikristo, kitu imani, maneno ya imani au ya kutia imani, havijawahi kuuzwa mahali popote. Hata Yesu Kristo, aliyekuja na injili na kuwa mwinjilishaji wa kwanza alikemea sana tendo la kutumia injili au maneno ya Mungu kwa ajili ya kutafuta riziki. Ni kwa sababu injili inapaswa kushibisha na kuneemesha roho, wala sio kushibisha na kuneemesha mifuko na miili.

Lakini kwa sasa injili inaonekana inavyotumiwa na baadhi ya watu kuzalisha kipato binafsi kilichojitenga kabisa na maneno ya injili yenyewe! Hata mwonekano wa wale wanaoitumia injili kujipatia kipato, kama walivyo wanamuziki wa injili, unajionyesha usivyofanana kabisa na mwonekano wa wainjilishaji wengine, kitu kinachoweka bayana kwamba wahusika hawajali wanachokinadi kinamwendea au kumuingia nani, bali wanakijali tu kile kinachotokana wanachokinadi, pesa, jambo linalotuleta kwenye majumuisho ya pamoja kwamba kinachofanyika ni biashara kamili.
 Katika injili tunaona kwamba kulitokea kitu kilichokuwa kama kongamano la injili, watu wakakusanyika toka mataifa mbalimbali, na Yesu Kristo akahubiri na kuponya. Kutokana na wingi wa watu hao na umbali wa walikotoka wakajitokeza watu wa kuwauzia huduma, lengo likiwa ni kufanya biashara kwa kujinufaisha na wingi wa watu hao. Jambo hilo halikumfurahisha Yesu Kristo hata kidogo.
Kristo aliona kwamba wauza huduma hao hawakuja kwa ajili ya neno la Mungu wala ukubwa wa neno hilo,  bali kulitumia neno hilo kwa ajili ya maslahi yao binafsi ya kimwili yasiyokuwa ya kiroho. “Yesu akaingia hekaluni, akawafukuza wote waliokuwa wakiuza na kununua hekaluni, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao waliokuwa wakiuza njiwa” Mathayo 21: 12.

Kilichomkasirisha Yesu ni watu kutumia jina la Mungu kufanya biashara zao. Sidhani kama hilo linaweza kugeuka anapowaona wanaoimba muziki wa injili kwa lengo la kujipatia pesa wakidai wanamtukuza Mungu. “Akawambia, imeandikwa, Nyumba yangu itaitwa nyumba ya sala; bali ninyi mmeifanya kuwa pango la wanyang’anyi” Mathayo 21 : 13.

Kama muziki wa injili unamtukuza Mungu inakuwaje unauzwa pamoja na kutozya viingilio unakochezwa? Ni lini tulimsikia au kumsoma Yesu Kristo akitozya viingilio kwa ajili ya kuwahubiria watu neno la Mungu?

Maana yote tuyafanyayo kuhusu injili mwongozo wake ni Kristo mwenyewe. Sasa unafanyaje yaliyo tofauti na matendo ya Kristo halafu unadai unaitangaza injili?

Mwimbaji mmoja wa muziki wa injili alialikwa kwenye usharika fulani, ambako kulikuwa kunafanyika harambee ya kutunisha mfuko wa ujenzi wa kanisa. Baada ya mwimbaji huyo kuimba wimbo mmoja alianza kudai alipwe pesa yake shilingi laki tatu! Eti naye huyo tuseme anamwimbia Bwana! Anamwimbia au anamwibia?

Muziki wa injili kwa sasa ni muziki kama ilivyo mingine yote, unachezwa kwenye maharusi, kwenye baa na sehemu zote za starehe. Kibaya zaidi ni pale muziki huo unapotumika kuchochea matendo aliyoyalaani Mungu badala ya kuyazuia huku ukiendelea kutumia jina la Mungu na maneno yake! Kuna ushuhuda unaoonyesha kuwa muziki huo unapigwa hata kwenye sehemu zote za kufanyia maovu!

Ajabu hatujasikia hata mara moja wanamuziki wa injili wakililalamikia hilo la muziki wao kupigwa kusikostahili. Wao wanachokijali ni mauzo ya muziki wao wakifurahia kipato kinachotokana na mauzo hayo.

Nitoe mfano wa Waislamu, imani ya Kiislamu inazingatia zaidi maadili yake. Haiwezekani Waislamu wakavumilia kuona au kusikia chochote kinachohusiana na imani yao kikitumika kusikohusika wakakubali kukaa kimya kwa kuutegemea ukimya huo uwapatie kipato cha aina yoyote. Ni lazima watakomesha tabia hiyo mara moja.

Lakini sasa muziki wa injili unaonekana unavyotumika kuhamasisha ngono, ufusika, ulevi na uchafu wa kila aina bila ya wahusika kuchukua hatua yoyote ya kukemea jambo hilo! Hiyo maana yake ni kwamba wanakubaliana na matendo hayo!

Nakubali kwamba muziki una gharama kuutengeneza, lakini hatahivyo kama maneno yaliyomo ni habari njema kwa wanadamu, Injili, basi ingetafutwa namna ya kukusanya pesa ya kuutengeneza, kwa njia iliyo safi, kusudi ikibidi muziki huo usambazwe na kugawiwa bure kwa watu ikiwa ni sehemu ya sadaka, kuliko kuonekana yanatumika maneno ya Mungu kibiashara, yaani biashara hekaluni. “Pozeni wagonjwa, fufueni wafu, takaseni wenye ukoma, toeni pepo; mmepata bure, toeni bure” Mathayo 10 : 8.

Siku za nyuma tulizoea kuiona na kuisikia miziki ya injili kwa maana halisi ya injili. Miziki hiyo ilikuwa ikipigwa katika maeneo ya kweli inakohubiriwa injili, yaani makanisani na kwenye mikutano ya injili bila waimbaji kulipisha viingilio wala kudai malipo ya ziada kwa ajili ya kazi hiyo ya kuimba nyimbo za kumtukuza Bwana.

Namkumbuka mzee mmoja aliyekuwa mahiri katika utunzi, uimbaji na uongozaji wa nyimbo za injili katika Jimbo Katoliki la Bukoba, Marehemu Bernard Buberwa, wa Parokia ya Mwemage, Ibwera Bukoba Vijijini. Mzee huyo alitunga nyimbo nyingi ambazo nyingine  bado zinaendelea kutumika makanisani katika Jimbo la Bukoba.

Lakini mzee huyo hakuwahi hata mara moja kutumia kipaji chake hicho kwa ajili ya biashara zaidi ya kukitumia kumuimbia Mungu na kutangaza neno lake kwa njia hiyo. Huyo ndiye hatuwezi kumweka fungu moja na wafanyabiashara hawa wa muziki wa injili wanaoligeuza hekalu la Mungu kuwa pango la wanyang’anyi, kama alivyosema Kristo.

Tunawaona waimbaji wazuri waliojaliwa bure vipaji vya sauti na uwezo wa kuimba, lakini kwa vile wanashindwa kutoa bure walivyopata bure ni mashaka makubwa kusema kwamba wanachokifanya ni kwa ajili ya Mungu.

Naamini kwamba ni dhambi kumhusisha Mungu na biashara. La sivyo wenye pesa peke yao, matajiri,  ndio pekee wangetarajiwa kuingia mbinguni kama Mungu angekuwa anatoza kiingilio.

Lakini kwa kuonyesha kwamba mali, pesa na utajiri ni vitu mbalimbali na utajiri wa mbinguni, Yesu alipomtembelea tajiri mkubwa, aliyeona kwamba pamoja na utajiri wake bado anataka awe na uhakika wa kuingia mbinguni, Yesu alimwambia agawe mali zake zote na kisha amfuate yeye. Kwa maana ya kwamba unapoutamani utajiri wa mbinguni hunabudi kuukana utajiri wa duniani. Soma Mathayo 19 : 16 – 26.

Ndiyo miziki ya injili tunaipenda tukifurahia midundo yake, ila hilo lisitufanye tuwaone wanaotoa midundo hiyo kuwa ni watu waliokolea kwa neno la Mungu wakiwa wamedhamiria kulifikisha kwa wengine. Hawa wanalitumia tu neno la Mungu kujipatia kipato binafsi, ni watu wanaofanya biashara kwenye hekalu na Mungu bila kujali kuwa wanamchikiza Yesu Kristo.

Kama kweli tunaizingatia injili hatunabudi kuwalaani

Next Post Previous Post
Bukobawadau