Bukobawadau

UONGOZI KCU(1990) Ltd UNAUKOMBA NA KUUZIKA USHIRIKA?

WAKULIMA  wanaounda ushirika wa KCU (1990) Ltd. mkoani Kagera wameamua kupiga kelele bila kuchoka, hata kama kelele hizo hazionekani kusikilizwa na yeyote kati ya wale waliolengwa kuzisikiliza. Wao, wanaushirika hao, wana imani kwamba kama Paulo na Sila, wanaoongelewa kwenye Biblia, walipiga kelele wakiwa kwenye kifungo cha kuonewa milango ya jela ikafunguka yenyewe na wao kuwa huru, basi nao itakuwa hivyo.
Wanaushirika hao wanasema kwamba kwa sasa ushirika wao hauna chochote cha kujivunia,  kitu kinachoufanya ushirika wao uonekane kama mkusanyiko au umoja wa mateso tu.
Eti zao ambalo ushirika huo uliundwa kulishughulikia, kahawa, halina manufaa tena kwao kwa vile ushirika wao ni kama umelitelekeza. Kahawa hainunuliwi tena KCU (1990) Ltd. kwa sasa kwa madai ya ushirika huo kutokuwa na pesa! Wakati ikisemekana kwamba hakuna pesa ya kununulia kahawa chama chao hicho kinayo madeni yasiyosemeka.
Pamoja na chama hicho kuwa na vitegauchumi lukuki lakini kinachozalishwa na vitegauchumi hivyo hakionekani. Ndiyo sababu vitegauchumi hivyo haviwezi kukinusuru chama hicho cha KCU (1990) Ltd. kwa kuyakwepa madeni yanayokikabili kwa sasa.
Inasemekana kwamba kinachoonekana katika ushirika huo ni “matanuzi” ya viongozi wasioelewa lolote kuhusu ukata unaoukabili ushirika wanaouongoza. Eti wakitazamwa viongozi hao haiwezi kuonekana kwamba ni watu wanaoendesha ushirika  unakaribia kukata roho! Kwamba viongozi wa KCU (1990) Ltd. ni watu wanaopendelea kujiweka ngazi moja na watu wanaoendesha taasisi zenye ukwasi wa hali ya juu sana.
Unatolewa mfano wa safari ya Burundi ya hivi karibuni. Eti safari hiyo ambayo imegharimu si chini ya shilingi milioni 23, tena zikiwa ni pesa za mkopo toka benki ya CRDB, haikuwa na umuhimu wowote kama viongozi hao wangekuwa wanaujali ushirika wanaouongoza kulingana na hali uliyomo kwa sasa.
Pia inasemekana kwamba, pamoja na safari hiyo kutokuwa na umuhimu wowote kwa viongozi wa ushirika, kwa vile tayari ushirika ulikuwa naye mwakilishi kule Burundi kwa ajili ya matakwa ya kitaalamu.
Hatahivyo inasemwa kwamba waliolipiwa kuingia kwenye mkutano wa Burundi, ingawa hawakuwa na umuhimu wowote kwenye mkutano huo, ni watu watatu tu, wajumbe wengine wa bodi walienda kutalii tu ikiwa ni sehemu mojawapo ya kuiongezea mzigo KCU (1990) Ltd. bila sababu yoyote ya maana.
Baada ya ujumbe huo wa KCU (1990) Ltd. kutoka kwenye safari hiyo ya kitalii nchini Burundi vikaanza kufanyika vikao vya siri kutaka kujua ni mtu gani anatoa nje siri za uongozi. Siri zenyewe ni kama hizo za uongozi kukihujumu chama hicho kikuu cha ushirika!
Ieleweke kwamba uongozi wowote unaofanya mambo yawe siri, hata kwa waliouweka madarakani uongozi husika, hiyo inakuwa ni siri isiyokuwa salama. Mara nyingi siri za aina hiyo zinakuwa ni siri za kifisadi.
Kinachoufanya uongozi ufanye mambo kwa usiri ni pamoja na mambo kama hayo ya safari ya Burundi iliyogharimu si chini ya shilingi milioni 23, pesa ya kuwapeleka wajumbe wa bodi kutalii wakati ushirika wanaopaswa kuuangalia mienendo yake ukiwa umekabwa koo na madeni.
Katika hali ya kawaida Bodi inakuwepo ili kuhakikisha madeni ya kizembe, kama hayo ya KCU (1990) Ltd. hayajitokezi, lakini jambo la kushangaza Bodi ya KCU (1990) Ltd. ndiyo inayoongoza kuzalisha madeni hayo ya kizembe!
Katika kutapatapa uongozi wa chama hicho cha ushirika ukitaka kujua ni nani anayetoa nje kitu unachodai ni siri, lakini bila kueleza siri hiyo inamnufaishaje mwanaushirika wa kawaida, uongozi huo unakisakama kitengo chake cha Moshi Export kuwa ndicho kinachotoa nje siri hizo!
Ikumbukwe kwamba kitengo hicho cha Moshi Export ambacho kimeamua kujiiendesha kwa uadilifu wa hali ya juu, ndicho pekee kwa sasa kilichobaki kuushikilia uhai wa ushirika huo, kikiteleza kidogo tu na kuanguka ushirika huo unazikwa kabisa.
Wanaushirika wa KCU (1990) Ltd. wanashangazwa na juhudi zinazofanywa na uongozi wa ushirika wao zenye makusudi ya kukiyumbisha kitengo hicho pasipo kujali kwamba juhudi hizo ni sawa na za mtu anayehangaika kukata tawi la mti alilolikalia!
Lakini hatahivyo uongozi huo haukijali kitu hicho, picha inayojitokeza ni ya kwamba uongozi huo hauwajali wanaushirika waliouweka madarakani. Sababu uongozi ulio makini ni lazima uwajali na kuwaheshimu walioupa madaraka.
Katika kufanya hivyo, kuwajali wadau, haiwezekani pakajitokeza kitu katika uongozi kinachoitwa siri katika utendaji wake, ambapo walioajiriwa au kuchaguliwa kuwatendea kazi wadau wanaficha matendo yao, kikazi, yasijulikane kwa wenye mali, waliowaajiri pamoja na kuwachagua.
Kutokana na hali hiyo tete katika chama kikuu cha ushirika cha KCU (1990) Ltd. baadhi ya vyama vya msingi vimeanza kufikiria kujiondoa kwenye ushirika huo. Hizo ni jitihada za kuwanusuru wanaushirika wake, hiyo ni baada ya kuuona uongozi wa KCU (1990) Ltd. uliopo madarakani kwa sasa unavyokusudia kuuzika kabisa ushirika huo mkuu hasa kwa kipindi hiki ambacho unaelekea kumaliza muda wake wa kinachoitwa uongozi.
Kwa kuanzia, chama cha msingi cha Magata, Muleba, Kagera, kimejiondoa rasmi kwenye ushirika huo. Chama hicho kimeishafanya utaratibu wa kujisajili kama chama kinachojitegemea. Kufanikiwa na kutofanikiwa
kwake kutakuwa kumetokana na uongozi mbovu wa KCU (1990) Ltd..
Wanaushirika wa Magata wanaeleza jinsi sekeseke lao ndani KCU (1990) Ltd. lilivyoanza. Eti meneja mkuu, kwa utashi wake, aliamua kukipandisha hadhi chama chao cha msingi na kukifanya kiwe cha kuuza kahawa inayotokana na kilimo cha asili, kwa maana ya kahawa inayolimwa bila ya mbolea ya viwandani ambayo kitaalamu inaitwa “organic”. Bei ya kahawa hiyo iko juu kuliko kahawa ya kawaida inayotokana na kilimo cha kisasa kinachotumia mbolea ya viwandani pamoja na madawa yenye kemikali.
Lakini hatahivyo karibu kahawa yote inayolimwa mkoa wa Kagera inatokana na kilimo cha asili, kwa maana ya karibu kahawa yote ya Kagera kuwa “organic”.
Wanaushirika wa Magata wanaeleza kuwa baada ya wao kudai mambo fulanifulani katika chama chao kikuu cha ushirika, mambo  ambayo ni sehemu ya haki zao za kiushirika, meneja mkuu, yuleyule aliyekipandisha hadhi chama chao cha msingi, akachukia na kuamua kukishusha hadhi chama hicho kwamba kahawa yao sio organic tena, kwamba itanunuliwa kwa bei ya kawaida!
Baada ya uamuzi huo wa meneja mkuu wanaushirika wa Magata wakajiuliza ni kigezo gani alichokitumia meneja huyo kuipandisha hadhi kahawa yao na ni kipi amekitumia kuishusha hadhi na kuiona ya kawaida wakati alishasema ni “organic”. Sababu wanasema, kiutaalamu,  haiwezekani malalamiko ya kitu kingine yakabadilisha aina ya kahawa.
Kufuatia uamuzi huo wa meneja mkuu, wanaushirika wa Magata wakagundua kuwa anachokifanya ni kutaka kuonyesha jeuri yake na mizengwe tu, wakaanzisha malalamiko. Malalamiko hayo yalipozidi kukua meneja huyo akatishia kukifuta uanachama chama chao cha msingi, ingawa kwa mujibu wa taratibu za ushirika, yeye kama mwajiriwa hiyo sio kazi yake.
Kwahiyo swali wanalojiuliza wanaushirika wa Magata, ni la kwamba inawezekanaje meneja mkuu, aliye mwajiriwa wao, awe na mamlaka ya kuwafuta uanachama wao wanaomwajiri! Baada ya kuona mizengwe hiyo ya ajabu ikiendelea kukua huku wakiwa wameshindwa kupata ushirikiano wa Mrajis Msaidizi wa mkoa, wakaamua kukitayarisha chama chao kianze kujitegemea.
Baadaye wakaenda kwa Mkurugenzi wa Bodi ya Kahawa na kupata kibali cha chama chao kujitegemea. Lakini baada ya kuona mambo yanawaendea vizuri wanaushirika hao kufikia kujiondoa kabisa katika ushirika wa KCU (1990) Ltd. ndipo Mrajis Msaidizi wa vyama vya ushiria mkoani Kagera akaanza kuingilia kati eti akitaka kuwasuluhisha na chama kikuu cha KCU (1990) Ltd..
Mrajis huyo Msaidizi wa mkoa haelezi ni kwa vipi meneja mkuu wa kuajiriwa, mtu asiyekuwa wa kuchaguliwa katika mfumo wa ushirika, awe na mamlaka ya kuwaamlia wanaushirika namna ya kujiendesha huku akiwafukuza baadhi ya wengine kutoka kwenye ushirika wa KCU (1990) Ltd. ambao kiuhakika ni mali yao. Wanasema “omushuma naita mukama w’engemu” kwa maana ya mwizi kumuua mwenye mali!
Nimalizie kwa kusema kwamba chama cha msingi cha Magata kimezigundua hujuma dhidi ya ushirika, kimetangulia kuonyesha mfano wa kukabiliana na hujuma hizo. Na pengine huo ndio mwanzo wa mwisho wa KCU (1990) Ltd.. Kilichochangia zaidi hali hiyo ni uongozi mbovu usioweka mbele maslahi ya wanaushirika isipokuwa kukomba kila kinachowezekana kukombwa na baadaye kukizika kabisa chama hicho kikuu cha ushirika KCU (1990) Ltd..
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau