Bukobawadau

URAIS 2015:MBONA HATUMUANGALII JAJI BOMANI?

Na Prudence Karugendo
Tumeingia 2014 wakati homa ya urais ndani ya vyama vya siasa, hususan CCM, ikiwa juu.
Nimeishaandika kwamba suala hili la wagombea kujulikana mapema, kwa uzoefu tulionao hapa nyumbani, hata katika nchi nyingi  za Kiafrika, suala hili muhimu hufanywa kwa kushtukiza, hivyo kuwanyima wananchi fursa ya kutosha kulijadili kwa kina.
 
Nadiriki kusema kwamba  imekuwa balaa tupu tangu uchaguzi wa kwanza uliorejesha mfumo wa vyama vingi hapa nchini, kutokana na watu kutojitokeza waziwazi kwa namna ambayo kweli ingemsaidia mwananchi wa kawaida kujua hatima yake.
 
Hii inadhihirisha namna ambavyo wagombea wengi watarajiwa hasa ndani ya CCM, chama ambacho kimejirithisa kwa mabavu utawala wa nchi yetu, wasivyokuwa na sifa zinazolingana na nafasi hiyo ya juu kabisa ya utumishi wa umma. Pia inatupa picha ya kwamba wagombea hao kupitia chama tawala   hawasukumwi na kero au shida  za wananchi, bali utashi wao katika kutimiza ndoto zao.
 
Angalia, imefikia mahali hata Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anazungumzia kuoteshwa ndoto, badala ya kutamka wazi namna anavyokerwa na hali ya baadhi ya mambo ilivyo hapa nchini. Au ni namna nyingine inayotaka kuzoeleka ya kufuata mkumbo tu, hasa ikizingatiwa kwamba Wizara hiyo imetoa Marais wawili sasa!
 
Ni wazi kwamba suala la maadili ya uongozi ni mgogoro kwa sasa.  Na inaelekea kuwa ni hatari ya kutisha haswa nikikumbuka mahojiano aliyowahi kufanyiwa  Marehemu Dr. Vedastus Kyaruzi, ambaye alikuwa ni miongoni mwa waanzilishi wa chama cha TAA na baadaye TANU. Baada ya uhuru alikuwa balozi wetu wa kwanza Umoja wa Mataifa,  na baadaye Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ulinzi, mpaka alipojiuzulu mwaka 1963 kwa kanuni za kimaadili na kuacha kabisa kufanya kazi serikalini. Hiyo ni tofauti na kujiuzulu kwa kuwajibika.
 
Hapa namnukuu Dr. Kyaruzi: “Nyerere atabaki with no match (bila wa kumlinganisha naye). Nyerere aliogopwa na kuheshimiwa na kila mtu. Marais waliomfuatia hawaogopwi wala kuheshimiwa. Viongozi wa sasa wanajilimbikizia mali kwa kutumia madaraka bila woga. “… halafu wanawakejeli wananchi, walipa kodi…(hivi ni vijisenti)! Hawana woga na sheria haiwagusi! Hapa ndipo tulipofikia baada ya miaka 50 ya Uhuru.” Anaendelea: “Mwl. Nyerere  aliweza kuwafanya watu waogope kufanya maovu, lakini si sasa. Tunaelekea gizani, tena giza totoro. Nadhani watu sasa wako tayari kulala na mabinti zao, hawana woga kabisa!”
 
“Katika hali hii ambayo viongozi wetu hawana woga tena, hawamwogopi tena Mungu, wana jeuri ya kuwaambia walipa kodi kuwa  (nimefuja mali sasa mnasemaje?), njia pekee iliyobaki ni mabadiliko, yatakayoongozwa na Mungu mwenyewe.”
 
Kama hali halisi inavyojionyesha basi ni wajibu wa kila mmoja wetu kufanya jitihada za makusudi ili kuzuia mapinduzi ya namna yoyote. Kwangu, tunavyoelekea uchaguzi mkuu, kipaumbele namba moja ni maadili, namba mbili ni maadili na namba tatu ni maadili. Hii ni tofauti na elimu kama kipaumbele cha kwanza, cha pili na cha tatu cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.
 
Nikirejea hoja ya Dr. Kyaruzi ya watu kuwa tayari kulala na mabinti zao, mfano hai ni kitendo cha aliyekuwa Waziri awamu ya Mkapa na Kikwete, Alhaji Prof. Juma Kapuya,  kutuhumiwa kubaka msichana ambaye pengine angeweza kuwa hata mjukuu wake!
 
Sina budi kusisitiza kuwa hili suala la maadili halina chama kwa namna lilivyo muhimu kulitekeleza.
 
Tunakumbuka waliowahi kugombea nafasi hiyo kupitia upinzani jinsi suala la maadili lilivyowasumbua na kuwapunguzia imani wananchi kwa kiasi fulani.
 
Baada ya kuonyesha jinsi gani maadili yalivyoporomoka nchini katika uongozi wa nchi, sasa niende moja kwa moja kumzungumzia mtu ambaye naamini anaweza kurejesha maadili ya uongozi na hivyo kulirejeshea taifa heshima yake ndani na nje ya mipaka yake. Huyu si mwingine bali ni Jaji Mark Bomani.
 
Hapa namwangalia mtu anayefaa kuwa rais wetu, kwahiyo msukumo nilio nao ni wa kiuzalendo zaidi,  usiofungamana na itikadi ya chama chochote cha siasa. Najua wapo wengine kama huyu, wasiokuwa na tamaa ya nafasi hiyo adhimu lakini wakiwa na uwezo nayo. Kuwataja na kuwajadili kwa manufaa ya nchi yetu naamini sio dhambi. Aliye na jina lingine, mbali na waliokwisha tajwa, na alilete tulijadili.
 
 
 
Leo nitajikita kumzungumzia Jaji. Kwa kweli hadithi ya Jaji Bomani ni ndefu, kitaifa na kimataifa,  na ni ya kutukuka. Ila havumi vizuri kwa mazingira yenye mizengwe ya CCM.
 
Hivi karibuni, kwenye mahojiano na gazeti moja la kila wiki kufuatia kifo cha Madiba, alionyesha kuyatambua kabisa matatizo yetu ya msingi kiasi cha kutia moyo.
 
Mwandishi alimuuliza; “Unadhani, inaweza kuichukua muda gani Afrika kupata viongozi wa aina ya Mwalimu na Madiba?”  Alijibu;  “Unajua, viongozi wa aina ya Mwalimu na Mandela hawategemei kizazi. Tunao hata leo, lakini hawapewi nafasi ya kuonekana na kutambuliwa na jamii, wanafanyiwa mizengwe. Wapo wanaojitokeza kwa kusaka sifa kwa madhumuni yao binafsi, na si kwa ajili ya kuwatumikia watu wao. Lakini wapo wachache wanajitokeza kwa sababu ya kuona uchungu wa maisha ya watu wao. Tunao lakini hawapati nafasi!”
 
Nadiriki kutamka kuwa Jaji Bomani anajizungumzia na yeye pia, maana aliwahi kugombea Urais 1995. Ni bahati mbaya kwamba Mwl. Nyerere alimwamini Mkapa  kuwa angeweza kusimamia maadili kikamilifu kuliko wagombea wengine wote.
 
Ukiacha suala hilo la Urais, Mwl. Nyerere alimwamini Jaji Bomani kiasi cha kumuomba awe msaidizi mkuu wa usuluhishi wa mgogoro wa Burundi, na kufuatia kifo cha Mwalimu, Mandela, aliyechukua nafasi ya Mwalimu kwenye suala hilo,  alimuomba kuendelea na nafasi hiyo mpaka mwisho. Si jambo la kubahatisha kufanya kazi na  mashujaa hao  wawili wa Afrika.  Alilinda heshima ya taifa letu kikamilifu.
 
Tukirejea ndani ya nchi, niliwahi kuandika mwaka jana kuwa ni jambo la kushangaza kidogo kwamba kwenye eneo alilobobea, haswa la sheria na mambo ya katiba, ingetarajiwa kuwa angetumika katika Tume ya Katiba. Katika kuonyesha sababu, hivi karibuni alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari pale Maelezo, bila woga aliwaonya CCM kutoingilia maamuzi ya wananchi juu ya Muungano wanaopendelea na vile vile kwamba yuko tayari ‘kufafanua mawazo yake mbele  ya chombo chochote, kiwe kikao cha CCM au kamati yoyote ya Bunge la Katiba’. Huyu ni mtu anayeheshimu kanuni ya demokrasia na anaonyesha njia sahihi ya kusonga mbele.
Na haishangazi kwamba kufuatia mkutano wake huo, mwandishi Aidan Mhando, alitamka: "mimi nimeguswa na maneno ya Jaji Bomani ambaye naweza kusema ni kiongozi shupavu aliyeamua na kuthubutu kutoa ya moyoni kwa masilahi ya taifa."
Tunapoelekea kupata Katiba Mpya, ni vyema pia kunukuu maneno ya msomi mahiri  wa siasa kutoka Afrika ya Kusini, Tom Lodge, anaposema: “ In new democracies the quality of political leadership matters more than in established political systems, however carefully scripted the constitutional safeguards may be against the abuse of power. Institutions are still fluid and susceptible to being shaped by dominant personalities.”
Tafsiri isiyo rasmi: “ Katika demokrasia changa ubora wa uongozi wa kisiasa una uzito mkubwa kuliko ndani ya  mifumo iliyojengeka kisiasa, pamoja na uangalifu wa hali ya juu wa Kikatiba kudhibiti matumizi mabaya ya madaraka. Taasisi nyingi bado hazijakomaa na hivyo kukabiliwa na uwezekano wa kufuata matakwa ya watu fulani.”
 
Hii inazidi kuniongezea sababu za kuamini nchi  inamhitaji mtu wa aina ya Jaji Bomani. Vilevile naamini atakuwa tayari kuondoa usiri wa mali za viongozi, tatizo ambalo ni kilio cha muda mrefu kwa kuonyesha kwa vitendo, maana hata ndani rasimu ya Katiba Mpya, ni suala lililopewa uzito unaostahili. 
Pengine kwa haraka niongeze kuwa viongozi wetu wengi hawana maisha yanayoeleweka nje ya siasa. Hii inawapa wananchi wakati mgumu kuhusiana na namna wanavyopata mali zao. Na matokeo yake ni nani wa kumfunga paka kengele.
 
Watanzania tunafahamu namna viongozi wetu wanavyojihusisha na njia zisizofaa katika kuchuma mali. Mfano ni suala la biashara ya madawa ya kulevya ndani ya Bunge letu tukufu. Sifa ya wazi kumhusu Jaji Bomani ni kwamba chanzo cha mapato yake kinaeleweka, maana ni wakili wa kujitegemea, pamoja na mambo mengine anayoyafanya kimataifa.
Kuhitimisha kwa uchache tu kuhusu Jaji Bomani, ni vyema kurejea tena mahojiano yake na gazeti moja la kila wiki. Swali zuri sana aliloulizwa mwishoni mwa mahojiano hayo ni: “Mandela ameondoka, Mwalimu Nyerere ameshatutoka. Una lipi la kuwaambia Watanzania kuhusu Mandela na kuhusu sisi Watanzania kama taifa?”
 
Alijibu, pamoja na mambo mengine kuhusu Tanzania;  “Kwa Tanzania na sisi Watanzania kama taifa, ni kwamba Tanzania lilikuwa ni taifa linaloheshimika duniani kwa namna tulivyojitolea na kuwa kimbilio la wanyonge na watu waliokumbwa na madhila katika nchi zao.”
 
“Heshima ile hatunayo tena. Leo tunaadhimisha miaka 52 ya Uhuru wa nchi hii, lakini bado tunao baadhi ya wananchi wetu  ambao Uhuru huu uliwakuta wakiwa ndani ya nyumba za nyasi na udongo, leo baada ya miaka 52 wanaishi kwenye nyumba za aina ileile! Nini maana ya Uhuru kwa wananchi hawa?”
 
Anaendelea kusema; “Mimi nilidhani uhuru huu ungetuletea mabadiliko ya kimaendeleo katika maisha ya wananchi wetu…”
 
Kauli zake zinaweka wazi msimamo wake juu ya usimamizi na matumizi sahihi ya rasilimali za nchi kwa maendeleo na ustawi wa watu wake na hususan  vita dhidi ya rushwa na matumizi mabaya ya madaraka.
 
Nihitimishe kwa kusema, Tanzania mpya bila kiongozi atakayesimamia maadili kikamilifu ni sawa na safari ndefu iliyojaa kila aina ya bugudha. Jaji Bomani unaijua njia ya safari yetu barabara, jaribu kutuepusha na hatari ya Mapinduzi!
 0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau