Bukobawadau

WAHAYA NA ZAHAMA KWA KINAMAMA

Na  Prudence Karugendo
WAHAYA  ni kabila maarufu linalopatikana kwenye eneo la Bukoba katika mkoa wa Kagera, Kaskazini Magharibi mwa Tanzania.
Kabila hilo ni moja ya makabila yaliyowahi kustaarabika na kuendelea, kielimu na kiuchumi, tangu enzi za wakoloni wakati nchi hiyo ikijulikana kama Tanganyika,  kabla ya kuungana na Zanzibar na kuwa Tanzania.
Kutokana na kabila hilo kuwa miongoni mwa makabila yaliyotangulia kupata elimu nchini Tanganyika, Wahaya wakaanzisha usemi wa kiutani, kwa lugha yao ya Kihaya, wakisema “inye nshomile” wenye maana ya kwamba “mimi nimesoma” yaani nimeenda shule na ninaelewa mambo mengi. Na huo ndio ukawa mwanzo wa makabila mengine ya Tanzania kuanza kuwatania Wahaya kwa kuwaita kina NSHOMILE.
Lakini pamoja na kabila hilo la Kihaya kuonekana limeelimika ukweli ni kwamba bado limeukumbatia ukandamizaji wa kijinsia wa tangu enzi na enzi, kina mama wakiwa ndio walengwa wakuu wa ukandamizaji huo. Ingawa tunaweza kusema kwamba kwa sasa ukandamizaji huo umepungua kwa kiasi fulani, lakini bado unaendelea katika baadhi ya maeneo, hasa sehemu za vijijini, kutokana na kujifunga zaidi katika utamaduni wa kabila hilo.
Mpaka sasa katika mila za Kihaya ni vigumu kuwalinganisha mwanamume na mwanamke kama binadamu walio sawa. Na inapotokea mwanamume wa Kihaya akataka kujiweka sawa na mkewe kunajitokeza mambo mawili. Jamii nzima ya Kihaya itamshangaa mwanamume huyo,  tena ikimlaumu kwa desturi hiyo,  inayoonekana kuupotosha utamaduni wake, au la pili itamuona mke wa mwanamume huyo kama mchawi aliyemroga mume wake mpaka akajisahau na kuanza kufanya mambo kinyume na utamaduni wake  bila yeye kujielewa.
Kama ilivyo ada kwa kila kabila hapa duniani, kuoana, mwanamume na mwanamke kuchukuana kwenda kuishi pamoja na kuanzisha familia yao, ni jambo la kawaida na lisiloepukika. Lakini jambo hilo inafaa litokane na makubaliano ya pande zote mbili.
Lakini katika mila za Kihaya sio lazima makubaliano hayo yawepo. Kipo kitu kinaitwa “okuleya” ambapo kijana au mwanaume anaweza akamuona msichana akamtamani, bila msichana kumfahamu kijana au mwanaume husika, mwanaume au kijana akaanza kufanya mipango ya kumteka nyara msichana husika ili akamchukue kuwa mke wake! Jambo hilo halina maelewano wala makubaliano, ila limehalalishwa kiutamaduni!
Wataandaliwa vijana wenye mabavu na kumvizia popote msichana mlengwa na kumkwapua kwa nguvu, huku wakimpa vipigo kama analeta ukaidi, kisha wanampeleka kwa yule anayetaka kumuoa. Kesho yake asubuhi na mapema anatumwa mtu, mtu mzima, nyumbani kwao na msichana aliyechukuliwa,  kwenda kutoa habari kwamba mtoto wao wasimtafute kwingine, yuko salama kaolewa na mtu fulani.
Badala ya wazazi wa msichana kuja juu watanywea, ikiwa ni alama ya kuhalalisha kitendo hicho cha kibabe na chenye kukiuka haki, ila watataka kiasi fulani cha pesa kitolewe kama faini ya kufanya kitendo hicho. Na kwa upande wa mwanaume, watenda kosa, faini hiyo inakuwa imeishaandaliwa tayari.
Katika makala hii nitatoa mifano miwili ya unyama wa aina hiyo nilioushuhudia mwenyewe.
Mfano wa kwanza unamhusu dada yangu mwenyewe. Ilikuwa sikukuu ya Pasaka, jioni baada ya kutoka matembezini dada akabadilisha nguo na kuingia jikoni kuanza maandalizi ya chakula cha usiku. Mara wakaja Vijana wanne wanajifanya kuulizia kitu fulani. Dada alipotoka nje ili awasikilize vizuri wakamdaka na kumfunika na makhanga na kumbeba juujuu. Mdogo wangu wa kiume alipojaribu kumsaidia dada yake akapigwa vibaya mno!
Kama kawaida kesho yake asubuhi akatumwa mtu kuja kutoa taarifa nyumbani kwetu akiwa ametayarisha faini tayari, na faini ikakubaliwa kama ishara ya kuhalalisha kitendo hicho haramu! Dada yangu akawa ameolewa kwa mtindo huo.
Ushuhuda mwingine ni wa binti ambaye hakuwa kwenye mpango wa kutekwa nyara ila alijikuta anaagukia huko katika kutaka kumnusuru dada yake!
Dada yake alikuwa na kijana ambaye alikuwa rafiki yake. Kijana akataka kutumia njia ya mkato kuoa badala ya kusubiri taratibu za kuchumbia, ndipo kijana akatangaza kijijini kwetu kwamba siku fulani anamleta mke. Kumbe habari hizo zikamfikia hata yule binti aliyekuwa rafiki yake.
Siku ya siku kijana akaenda, alipofika sehemu waliyozoea kukutana na rafiki yake huyo wa kike, kijana akiwa ameambatana na vijana marafiki zake kwa ajili ya shughuli ya kumbeba msichana, yule msichana mlengwa hakuonekana. Badala yake akaja mdogo wake kuwaeleza wale vija, kama kuwakoga, kuwa dada yake hayupo katumwa sehemu ya mbali kidogo. Alipowakaribia,  bila yeye kuwa wasiwasi wowote, wakambeba yeye na kumuingiza kwenye gari na kuondoka naye!
Kwahiyo ikabidi aolewe mdogo mtu, ambaye hakuwa kwenye mpango na wala hakuwa na urafiki wowote na yule kijana zaidi ya kuonekana kama shemeji, aliyekuwa abebwe akanusurika na mpaka sasa ndiye shemeji!
Tukiacha ukandamizaji huo ambapo wanawake wanaonekana kuporwa haki zao za kujifanyia maamuzi katika mahusiano, yapo mambo mengine ya muhimu na ya lazima kuyatekeleza kwa mwanamke wa Kihaya aliyeolewa, ingawa mambo yenyewe yanaweza yakafanywa na jinsia zote mbili, yaani mwanamke na mwanamume.
Mambo hayo ni pamoja na kilimo cha musimu. Mwanamke analazimika kupanda maharage na mahindi punje mojamoja, tena kwa mkono, kwenye shamba ambalo wakati mwingine linaweza kuwa na ukubwa wa ekari kumi na zaidi.  Wanalazimika kupanda kwa mkono kutokana na mashamba yenyewe yalivyo. Ni mashamba ya kilimo mseto “mixed farming” ambako haiwezekani kutumika kifaa kingine chochote kurahisisha upandaji huo.
Hiyo ni kazi ya mwanamke peke yake ambapo tamaduni za Kihaya zinamzuia mwanamume kujihusisha na kazi hiyo hata kama ana hamu ya kumsaidia mkewe.
Mbali na hiyo mwanamke wa Kihaya anapaswa kuwa na mashamba ya kilimo kingine cha musimu, mashamba ya njugumawe na karanga, mazao ambayo kawaida hulimwa mbugani au maporini, nje kabisa ya makazi ya watu. Inaweza ikawa hata umbari wa kilometa 10 na zaidi ambako mwanamke inambidi aende kila siku, kwa mguu, kwa karibu mwezi mzina na zaidi kuyahudumia mazao hayo.
Mwanamke asipolima mazao hao inaweza ikawa ishara ya kuharibu na kuvunja ndoa yake, sababu itaonekana hamjali mume wake kwa kutomlimia mazao hayo ya musimu. Na kwa tamaduni za Kihaya uko ni kukiuka majukumu ya mwanamke aliye kwenye ndoa. Ikumbukwe kwamba mnufaika mkubwa wa mazao hayo ni mwanamume, ingawa karibu mara zote hajihusishi na kilimo cha mazao hayo.
Mazao hayo yanapokomaa, yakavunwa na kutayarishwa kupikwa kwa mara ya kwanza ni lazima yapikwe rasmi kwa ajili ya mwanamume ikiwa ni sehemu ya kumuonjesha jasho la mke wake. Vinginevyo itakuwa ni vurumai tupu ndani ya nyumba.
Pamoja na ukweli kwamba anayehudumia mazao hayo mwazo hadi mwisho ni mwanamke kiasi cha mazao hayo kuonekana ni mali yake, umiliki wake huo unaishia shambani tu. Mazao yakishavunwa na kuletwa ndani umiliki unageuka, yanakuwa ni mali ya mwanamume!
Kitu kingine kinacholeta sekeseke kwa wanawake wa Kihaya walio kwenye ndoa ni musimu wa senene. Senene ni wadudu jamii ya panzi wanaotokea mara mbili kwa mwaka, mwezi wa nne, Aprili, na mwishoni mwa mwaka. Wadudu hao waligeuzwa kuwa chakula cha heshima cha Wahaya tangu zamani.
Katika miaka ya nyuma ilikuwa ni mwiko kabisa wadudu hao kuliwa na wanawake, kama ilivyokuwa kwa karibu vitu vyote vitamu ambavyo vilikuwa halali kwa wanaume tu. Isipokuwa kazi ya wanawake ilikuwa ni kuwatafuta wadudu hao kwa ajili ya waume zao tu, kuanzia usiku wa manane kila musimu wake ukifika.
Inagawa kwa sasa baadhi ya wanawake wa Kihaya wanawala senene, lakini ulazima wa kuwatafuta na kuwakamata umebaki ni kwa ajili ya wanaume tu. Na kwa mwanamke asiyefanya hivyo aelewe anahatarisha ndoa yake.
Hayo na mengine ambayo sikuyataja yanajionyesha kabisa jinsi yalivyowaweka wanawake wa Kihaya majaribuni kwa kuwapokonya haki zao za kiubinadamu.
Hivyo pamoja na Wahaya kujiita NSHOMILE hicho bado ni kitu kinachowapita pembeni pasipo kuuangalia ukubwa wa madhara yake  yanayoweza kujitokeza iwapo hawakuufanyia marekebisho utamaduni wao.
Sababu mpaka sasa bado ni jambo la kawaida kuwasikia wazazi wa Kihaya wakimhimiza kijana wao  ili aoe apate mtu wa kumsaidia kazi, hasa za kulima mashamba, kana kwamba kuoa ni sawa na kununua trekta!
Nimalizie kwa kusema kwamba mtazamo huo batili katika utamaduni wa Kihaya usipofanyiwa marekebisho, kuendelea kujiona au kujiita NSHOMILE kutakuwa ni batili pia.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau