Bukobawadau

JK anakubali kuiacha Tanzania kwenye maangamizi!

Na Prudence Karugendo
MHESHIMIWA  Jakaya Mrisho Kikwete ni mtu mwema sana. Ndiyo maana alipotangazwa kuwa rais wa nchi yetu kwa mara ya kwanza wananchi karibu wote walishangilia, wa chama chake, CCM, na wa vyama vingine vya upinzani.
Ila sina uhakika kama wote walioshangilia ushindi wake walimwelewa kiundani, inawezekana wengine walisukumwa na muonekano wake kuushangilia ushindi huo wakiamini kwamba wamepata rais bora. Tuliobahatika kumwelewa kwa karibu ndio tulioshangilia tukikielewa tunachokishangilia. Nitajaribu kueleza.
Tangu kabla ya JK kuwa rais alionyesha utu na wema ambao ni nadra sana kuonyeshwa na kila mtu. Mfano, alionyesha kuwajali wafanyakazi wenzake waliokuwa chini yake, pale alipokuwa waziri, akiwahangaikia kuliko hata ndugu zao wa damu pale walipokuwa wanapatwa na matatizo yaliyo kwenye uwezo wake wa kuyatatua. Jambo hilo lilikuwa halifanywi na kila mtu wa hadhi yake.
Hata baada ya kuwa rais tunaona Kikwete aliyoendelea kuyafanya katika kuonyesha ukaribu wake kwa jamii anayoingoza. Kuwajulia hali walio kwenye matatizo, wanaoumwa, kuwahani waliofiwa na hata mwenyewe kushiriki mazishi, wakati mwingine, katika sehemu mbalimbali, akiwa rais wa nchi, bila kujali umaarufu wa aliyekufa ukoje katika jamii. Pia katika furaha, anajichanganya na wanajamii kufurahi nao pasipo kujali uwiano wao katika jamii.
Kwakweli hilo ni jambo la kushangaza na kujivunia,  kuwa na rais wa aina hiyo. Rais asiyeinyanyapaa jamii anayoiongoza, rais wa watu anayejihisi ni mmoja wa watu hao. Kwakweli hicho ni kipaji chake ambacho hatunabudi kumsifia nacho. Sio marais wote wenye kipaji cha aina hiyo.
Nikishamwangalia hivyo rais wetu, yapo mengine yanayotatanisha sana, ambayo ndiyo yamenisukuma kuandika makala hii. Mambo yanayoonyesha kana kwamba KJ anao mpango wa kuiacha nchi hii katika maangamizi pale atakapoondoka madarakani katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu kijacho.
Ikumbukwe kwamba Tanzania ni nchi iliyokuwa imezoea amani na utulivu, kiasi cha kuichukulia hali hiyo kama mali yake ya urithi. Nchi ambayo wananchi walizoea kuhitilafiana bila kukosana, kugombea bila kugombana, kuchukizana bila kuchukiana, kupoteza bila kupoteana nakadhalika nakadhalika.
Mlezi wa kwanza wa hali hiyo, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, katika kuikomaza hali hiyo ya amani na utulivu, akaamua kuachia madaraka kwa hiari yake, bila kubanwa na Katiba ya nchi wala kitu kingine chochote, huku wananchi wakiwa bado wanampenda sana na yeye akiwa bado anazo nguvu zake kamili, akisema kwamba naye anataka amuone kiongozi wake.
Nyerere alikuwa haijui hali hiyo ya kuongozwa sababu tangu tunapata uhuru yeye alikuwa kiongozi.
Pamoja na mambo mengine aliyowahi kuyasema Mwalimu, kama yale ya cheo ni dhamana, pia alitaka kuonyesha kwamba uongozi unaweza ukabadilishwa toka kwa mmoja kwenda kwa mwingine bila chuki wala fujo.
Wakati Mwalimu anaachia madaraka alikuwa na umri wa miaka 63 tu. Lakini katika nchi nyingine wapo vikongwe wa miaka 90  na bado wanatamani kuendelea kugombea wakijiona bado wana nguvu sana!
Nyerere aliiacha nchi katika amani na utulivu. Watu walikuwa wanagombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa kushindanisha hoja. Hapakuwepo vitisho wala vishawishi vingine tunavyoweza kuviita rushwa.
Sasahivi hali hiyo imetoweka. Ushindani wa kisiasa umekuwa kama vita, au niseme ni vita kamili. Sababu vita ni mapambano yanayosababisha vifo. Mara nyingi tunaona jinsi chaguzi za wakati huu zinavyoambatana na vifo, kutekana, kujeruhiana na mambo yote machafu yanayoashiria kuwa nchi yetu inaingia kwenye maangamizi.
Kwa leo nataka niutumie uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga, Iringa,  kuonyesha ninachokisema hapa.
Yaliyojitokeza Kalenga ni mambo machafu ya kutisha, ya kusikitisha, ya hatari na ya kukatisha tamaa, yakionyesha ni jinsi gani nchi yetu inavyochungulia kuzimu!
Jambo la kusikitisha na linaloshangaza kupita kiasi ni la kuwaona wanasiasa wakishangilia na kufurahia kinachoitwa ushindi, kamwe watu hao hawaonekani kutilia maanani ni mazingira gani yametumika kukipata hicho wanachokishangilia. Hakuna anayejali kuwa kulikuwepo kutekana nyara, kuchomana visu, kutishiwa kuuawa, kubakwa pamoja na kudhalilishana kulikovuka mipaka. Hayo yote tunayasikia kwenye nchi zenye machafuko.
Wanasiasa wanashangilia tu kinachodaiwa ni ushindi bila kujali kuwa kimepatikana katika mazingira haramu. Kwa nini nasema hivyo? Hebu tuangalie.
Wananchi waliojiandikisha kupiga kura Kalenga ni watu elfu 70. Waliopiga kura ni watu elfu 28 tu, hata nusu haifiki! Kwa maana hiyo watu elfu 42 hawakupata haki yao ya kupiga kura, na ndio walio wengi.
Mengi yanasemwa, shahada za kupigia kura zilikuwa zinanunuliwa kama njugu, ushahidi ni wa mtu aliyekamatwa na shahada za kupigia kura za watu mbalimbali zaidi ya 100. Kuna watu ambao majina yao hayakuonekana kwenye orodha ya wapiga kura pamoja na kuwa na shahada zao halali walizopewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Hao ni mbali na idadi kubwa ya wananchi ambao Tume ya Taifa ya Uchaguzi imegoma kuwasajili kama wapiga kura kwa kukataa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.
Katika hali kama hiyo, ambapo Tume ya Taifa ya Uchaguzi haitaki kuupima ukweli halisi wa matakwa ya wananchi, unaweza ukapata wapi ujasiri wa kusema kwamba mgombea fulani kashinda uchaguzi ilhali karibu robo tatu ya waliopaswa kumchagua au kumkataa wamekoseshwa kwa makusudi haki yao ya kuonyesha wanachokitaka?
Tukiliacha hilo, tutaona kwamba kila chama cha siasa nchini kina utaratibu wake wa kulinda maslahi yake. Kutokana na Jeshi la Polisi nchini kuwa na majukumu mengi ya kuulinda usalama wa raia na mali zao pamoja na mambo mengine ya ziada, uwezekano wa jeshi hilo kuyalinda maslahi ya kila chama cha siasa kiukamilifu unapungua.
Kwa kulizingatia hilo, ndipo kila chama cha siasa kikabuni utaratibu wa kujilindia maslahi yake. Huo ndio mwanzo wa vikundi vya Green Guard, Blue Guard, Red Brigade nakadhalika. Vikundi vyote hivyo vinapaswa kuwa sehemu ya ulinzi shirikishi kwa kusadiana na Jeshi la Polisi, kwa namna ya sera za jeshi hilo zilivyo kwa sasa.
Lakini jambo la kushangaza na kutia uchungu ni la kwamba Jeshi la Polisi linakitambua, kukiheshimu na kukiogopa kikundi kimoja tu cha ulinzi wa vyama vya siasa, nacho ni Green Guard cha CCM! Vikundi vingine vyote vinaonekana ni vya kihuni na ni maadui!
Kivipi? Siku moja kabla ya uchaguzi mdogo wa Kalenga, Kamanda wa Polisi mkoani Iringa, Ramadhani Mungi, alitangaza kwamba jeshi lake limejiimarisha kulinda usalama katika eneo lote la Kalenga wakati wa uchaguzi huo mdogo. Kwahiyo akasema kwamba hatapenda kuvisikia vikundi vya Green Guard wala Red Brigade katika kipindi hicho.
Kumbe tangazo hilo lilikuwa kama la kutaka kuwaondoa Red Brigade kusudi Green Guard wafanye uhalifu wao kiurahisi!
Sababu baadaye tulisikia mbunge wa Chadema, viti maalumu, Rose Kamili, katekwa na kufanyiwa kila vitendo vya kinyama, kihuni na kishenzi na kikundi cha Green Guard. Lakini badala ya Kamanda Mungi kutueleza namna alivyowashughulikia wahuni hao, akaonekana anakibariki kitendo walichokifanya kwa kusema kwamba walimkamata mbunge huyo akitoa rushwa! Kauli yake ya kwamba hataki kusikia Green Guard wala Red Brigade akawa ameisahau!
Sote tunaelewa kwamba kazi ya kuwashughulikia watoa na wapokea rushwa ni ya watu wa Takukuru, ni lini Mungi ameigeuza kazi hiyo na kuifanya iwe ya vijana wa Green Guard?
Hata hivyo hakuna sheria inayosema kwamba anayekamatwa akitoa au kupokea rushwa apelekwe kwenye ofisi za CCM na kusulubiwa, kama alivyofanyiwa Rose Kamili. Sheria hiyo ni ya Mungi na vijana wake wa Green Guards!
Shabiki mmoja wa CCM anasema kwamba kitendo cha Green Guards kumteka mbunge kinalipiza kisasi kitendo cha Red Brigade kumteka mkuu wa wilaya katika uchaguzi mdogo wa Igunga.
Lakini ikumbukwe hekaheka na hinyahinya zilizojitokeza kufuatia kitendo hicho cha Igunga. Mbona hatukuona kitu kama hicho kule Iringa? Au tuseme polisi wanalinda usalama wa wananchi wakiangalia itikadi zao ziko upande gani?
Je, ingetokea yule mama wa Igunga akaingizwa kwenye ofisi ya Chadema na kufanyiwa unyama kama aliofanyiwa Rose Kamili ndani ya ofisi ya CCM hali ingekuwaje? Ofisi hiyo ya Chadema isingekuwa gofu sasa hivi?
Baada ya tukio la kutekwa mbunge Rose kamili yakafuatia matukio mbalimbali ya kutekwa vijana kadhaa wa Chadema kuhusiana na uchaguzi huo wa Kalenga. Vijana hao wamefanyiwa unyama wa kila aina kama baadhi yao walivyotoa ushuhuda baada ya kunusurika vifo.
Wakati mwingine Kamanda Mungi alidai kuwa polisi inawashikilia vijana wawili kutoka Arusha, kwamba walienda Iringa kwa ajili ya kufanya vurugu kwenye uchaguzi wa Kalenga. Taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Slaa, zinasema kwamba vijana hao ndipo wamepatikana baada ya kupotezwa kwa siku karibu nne!
Lakini Mungi hasemi lolote kuhusu vijana wa CCM waliosombwa  kutoka kila kona ya Tanzania na kujazwa Iringa, pamoja na vitendo vyao kueleza kila kitu kutokana na unyama walioufanya kule.
Wapo wanaosema kwamba yaliyotokea Kalenga yanatokana na amri ya mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, ya kwamba CCM wanapaswa wajilinde wenyewe na kujibu mapigo! Lakini badala ya kujibu mapigo mbona wanashambulia?
Ni wazi kwamba mambo hayo, yaliyo na baraka za mwenyekiti wa chama tawala na Amiri Jeshi Mkuu, yanaifanya nchi yetu ichungulie kuzimu. Sababu sioni yataiepushaje nchi isikumbwe na zaama kama zile za Anti-Balaka na Seleka kule Afrika ya Kati.
Je, hicho ndicho anachopanga kutuachia Kikwete, tuliyemuona ni kiongozi bora,  kama zawadi ya kumaliza muda wake madarakani?
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau