Bukobawadau

NEMBO YA WATANZANIA MASHUHURI

Mchora Vibonzo Mashuhuri Nchini Ndugu Chris Katembo ametengeneza Nembo Maalum na ya Kipekee ya Watanzania Mashuhuri.
Ukurasa wa Watanzania Mashuhuri unatoa Shukran za dhati kwake kwa Nembo hii ambayo ikikamilika ndiyo itakuwa Nembo Rasmi ya Ukurasa.
Kauli Mbiu yetu ni "Watanzania Mashuhuri: Historia katika kuhuisha Uzalendo wa Kitanzania".
Ahsante sana Chris Katembo.

 OMARI MAHADHI MWINYIMTWANA 'BIN JABIR', MLINDA MLANGO FAHARI YA TANZANIA
 Pichani ni Mlinda Mlango wa zamani wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Ndugu Omari Mahadhi Mwinyimtwana 'Bin Jabir', Mmoja wa wachezaji mahiri wa Soka ambao Nchi hii imewahi kupata.

Omari Mahadhi alikuwa ni Mlinda Mlango mahiri na wakutumainiwa wa timu ya Taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' katika miaka ya 1970 katikati mpaka miaka ya 1980 mwanzoni. Licha ya kuwa na umbo la kawaida, lakini alikuwa hodari mno awapo golini na kutokana na umahiri aliokuwanao ilikuwa sio rahisi kufungwa bao kirahisi.

Mahadhi alichaguliwa kuchezea Taifa Stars akitokea klabu ya African Sports 'Wanakimanumanu' ya Jijini Tanga. Pamoja na kuichezea klabu ya African Sports, pia ameichezea kwa mafanikio makubwa klabu ya Simba SC aliyojiunga nayo mwaka 1975.

Kwa muda wote ambao aliichezea Simba aliweka rekodi ya kukaa golini katika mechi nyingi ambazo walishinda dhidi ya Wapinzani wao Klabu ya Dar Young Africans 'Yanga' na alikuwa langoni katika kikosi cha Simba cha mwaka 1977 kilichoifunga Yanga mabao 6-0.

Baada ya kustaafu kucheza soka la ushindani miaka ya themanini mwanzoni, Mahadhi alijishughulisha na kazi ya Ukufunzi wa Soka akifundisha baadhi ya timu zikiwemo 'Simba SC' ya Dar es salaam na 'Waziri Mkuu FC' ya Dodoma.

Mahadhi ameacha heshima na hazina kubwa ya vipaji, wanawe kadhaa wakifuata nyayo zake kwa kuchezea Klabu ya Coastal Union ya Tanga na kisha Klabu za Azam Fc, Simba SC na Yanga za Dar es salaam.

Kwa hivi sasa hatunaye tena Nguli Omari Mahadhi 'Bin Jabir', kwani amefariki dunia katika miaka ya 1980 mwishoni, Lakini bado nyoyoni mwetu atabaki kuwa Fahari yetu na Kiigizo chema cha Kizazi cha Soka cha Tanzania. Mola amlaze pema Ndugu Omari Mahadhi Mwinyimtwana 'Bin Jabir'.

Next Post Previous Post
Bukobawadau