Bukobawadau

WALIOWAJIBISHWA MAGATA- MULEBA WAANZA KUVURUGA SHUGHULI ZA KCU (1990)LTD



Na Deogratias Kishombo
SASA ni dhahiri kwamba baadhi ya kikundi kidogo cha waliokuwa viongozi wa chama cha msingi cha Magata katika Wilaya ya Muleba ambao wamewajibishwa na bodi ya Chama kikuuu cha Ushirika mkoani Kagera (KCU 1990 ltd) kutokana na utovu wa nidhamu kwa kukiuka masharti ya msingi ya kilimo hai (organic) kwa kununua na kuingiza kahawa ya kawaida (conventional coffee) wameanza kuvuruga wanachama na ushirika wa mkoa.
Wameanza kuvuruga ushirika kwa kutumia baadhi ya vyombo vya habari wakitaka kuwashawishi wakulima kujitoa katika chama kikuuu cha msingi mkoani hapa cha KCU (1990) Ltd kitendo ambacho kimeanza kuwaacha wanachama wa Magata njiapanda. Wanachama wanasema hawataki kuburuzwa.
Wakati serikali ya Wilaya ya Muleba chini ya Afisa Ushirika wa wilaya hiyo Bwana Malelo Magoma ikisema hakuna taarifa rasmi ya kujitenga kwa chama hicho, kiongozi wa kikundi hicho cha wanaotaka kujitenga Bwana Yusufu  Kakwata  huku akijua kwamba anakiuka baadhi ya vifungu vya sheria ya ushirika anasema lazima wajitenge.
Baadhi ya wanachama na viongozi waliohojiwa na mwandishi wa makala hii wanasema hao wanaotaka kujitenga hawana nia njema na ushirika wa Kagera wakisema kwamba ushirika wa Kagera umefanya mambo mengi na umeleta manufaa kwa wanachama na umekuza uchumi wa mkoa na nchi kwa ujumla.
Wanaenda mbali kwa kusema kwamba hicho kikundi cha akina Kakwata kitaua ushirika na hakitaweza kuwasaidia wananchi walio wengi ambao bado wana imani na KCU (1990) Ltd.
“Hatuna imani na hatuwezi kuwa salama kama Magata itajitenga. Walio wengi tutapata shida tu hasa sisi wakulima wa kawaida ambao tumekuwa kwa muda mrefu tukitegemea KCU (1990) Ltd”  anasema Amrati Siraji, Mwenyekiti wa zamani wa chama cha msingi cha Magata.
Anaongeza kwamba wakati akiwa Mwenyekitu wa chama hicho amefanya mambo mengi kwa wanachama wake na wanachama wengi walikuwa na imani naye lakini baadae alikuja kushangaa kuondolewa kwa mizengwe na kundi linalotaka kujitenga.
“Sasa hivi wakulima tuliowengi nafikiri tuwe makini na watu hawa wanaotaka tujitenge. Nafikiri wao waondoke watuachie Magata yetu” alisema.
Naye Mbunge wa Muleba Kusini Profesa Anna Tibaijuka akiongea na mwandishi wa habari hizi akiwa Dodoma alisema kwamba hayo maneno ameyasikia lakini hayaungi mkono.
“Kuna kamati ya chama cha msingi ilinifuata ikitaka kupata maoni yangu nilichowaambia kujitenga hakukubaliki. Kwanini kujitenga? Alihoji.
Profesa Tibaijuka anaongeza kwamba jambo la maana siyo kujitenga ila muhimu ni kuangalia ni namna gani   chama kikuu cha ushirika (KCU 1990 LTD) kinaweza kusaidiwa  ili kifanye kazi zake kwa ufanisi ili kifikie malengo yake.
”Mimi naamini katika kuboresha na kusaidia ni namna gani KCU inaweza kuwa efficient kuliko kujitenga” anasema.
Naye Veterani wa Ushirika na ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha msingi cha Kamachumu Mzee Karugaba Mayanja anasema hayo maneno ya kujitenga aliyasikia kwa baadhi ya watu lakini anasema hayo mambo ya kujitenga hayana maana.
Akiongea kwa umakini mkubwa anasema amekuwa mwenyekiti wa chama cha msingi cha Kamachumu tangu mwaka 1988 hivyo anafahamu mambo mengi ya ushirika hivyo hoja zinazoibuliwa hivi sasa ni kuvuruga Ushirika wa Kagera ambao umejizoelea sifa nyingi ndani na nje nchi.
“Kwani sisi Muleba tujitenge tuna nini?. Miundo mbinu yote ya ushirika haipo hapa. Na ushirika hauko rahisi kama watu wanavyofikiri unahitaji mambo mengi ya msingi ambayo hapa siyaoni” alisema Mzee Karugaba.
Hivi karibuni baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vililipoti kwamba chama cha msingi cham Magata wanataka kujitenga huku vikisema kwamba tayari maombi ya kujitenga yameishapelekwa serikali.
Kiongozi wa kikundi kinachotaka kujitenga Bwana Yusuf Kakwata ambaye anatajwa na wanachama kwamba yeye ndiye kinara wa kutaka kujitenga kwa Magata anasema kwamba nia yake ya kuwashawishi wana Magata inaendelea.
“Tunaendelea na mchakato wa kujitenga” alisema.
Alipobanwa zaidi  na maswali ya waandishi wa habari waliofika nyumbani kwake alisema: “Kwanza mlipoanza safari kuja kwangu nilijua kwamba mnakuja hivyo najua mnachokitafuta” alisema.
Alisema kwamba sababu ya kufukuzwa kwake kutoka kwenye ujumbe wa bodi ya KCU (1990) Ltd ni kutokana na wivu dhidi yake kwa sababu anazalisha kahawa nyingi na kufukuzwa kwake kwenye shughuli nyingine za KCU (1990)Ltd ni chuki binafsi.
“Mimi ni mkulima wa kahawa namba mbili kitaifa hivyo yote yanayotokea hapa ni chuki na wivu tu wa kahawa” alisema.
Kwa mujibu wa taarifa iliyosainiwa na ya Mkaguzi mkuu wa Chama Kikuu cha Ushirika Bwana Stanislaus Mutahyabarwa inaonesha kwamba orodha ya kikundi cha wanaotaka kujitenga cha Magata ni wale wote ambao bodi ya KCU (1990) LTD imewawajibisha kutokana na makosa mbalimbali ikiwemo udanganyifu uliofanyika Magata PCS LTD tangu mwaka 2010 hadi 2012 ambao walio wengi walikuwa viongozi chamani.
Pamoja na makosa mengine  viongozi hao wa zamani wanatuhumiwa kuuzia chama kwa bei ya kahawa hai wakati siyo hai na kwa njia hiyo kukiibia chama jumla ya  mamilioni ya shilingi na kuleta usumbufu katika soko  la biashara ya kahawa hai (organic coffee).
Mwisho
Mwandishi wa makala haya ni mshauri wa habari wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani Kagera. Anapatikana 0688 065574. E-mail: pmediaconsultancy@gmail.com
Next Post Previous Post
Bukobawadau