Bukobawadau

“EKA MBE” KANALI FABIAN MASSAWE

Na Prudence Karugendo
NIANZE  makala hii kwa usemi wa lugha maarufu mkoani Kagera,   Kihaya, usemao kwamba “ebitagira mahyo tibyera”. Usemi huo hauna tafsiri ya moja kwa moja katika Kiswahili isipokuwa kwa maelezo yaliyozunguka ili kupata maana yake. Ni kwamba Wahaya wanaamini kwamba mtu akiwa analima shambani asipopata mtu wa kumpa pole ya kazi mazao anayoyalima hayawezi kusitawi vizuri. Lakini hatahivyo mantiki ya usemi huo ni kwamba juhudi zozote zisizothaminiwa inakuwa ni kazi bure. “Ebitagira mahyo tibyera”.
Nimeanza na maelezo hayo kusudi nipate kueleweka katika kusudio langu la makala hii ya kumpongeza mkuu wa mkoa wa Kagera, Kanali Fabian Massawe, kwa juhudi zake anazozionyesha za kuuinua tena mkoa  huo ambao kwa miaka ya karibuni uliporomoka sana kimaendeleo.
Itakumbukwa kwamba tangu enzi za wakoloni kulikuwepo na jamii za makabila mawili katika iliyokuwa Tanganyika zilizokuwa juu kimaendeleo; jamii za Wahaya na Wachagga. Kuwepo  juu kimaendeleo kwa jamii hizo mbili kulileta aina ya  ushindani kati ya Wachagga na Wahaya, ushindani wa kimaendeleo wa kutaka kuonyesha nani zaidi kati yao.
Ni katika hali hiyo kulipojitokeza imani kwamba Mhaya asingeweza kuongea Kichagga wala Mchagga kuongea Kihaya. Lakini kwa sasa hayo yamekwisha na kubaki kwenye historia. Hiyo inatokana na ukweli kwamba hakuna tena ushindani wa kimaendeleo kati ya Wachagga na Wahaya ambapo hali halisi kwa sasa inaonyesha kwamba Wachagga wamewaacha mbali Wahaya kimaendeleo. Huo ni ukweli usio na ubishi.
Hilo linajidhihirisha kwa njia mbalimbali. Nakumbuka siku moja nilimshukuru kiutani rafiki yangu Mchagga kwa lugha yake kwa kumwambia “aika mbe” jamaa mmoja aliyekuwa karibu akabaki mdomo wazi akisema kwamba kweli dunia sasa imebadilika! Akaongeza kuwa zamani Mhaya kuongea Kichagga au Mchagga kuongea Kihaya ilikuwa sawa na Mwislamu kula nyama ya nguruwe! Lakini kwa sasa Wachagga wanaongea Kihaya na Wahaya wanaongea Kichagga. Hiyo ni kwa sababu upinzani uliokuwepo wa kimaendeleo kati yao haupo tena. Tumekubali yaishe.
Lakini hatahivyo nimegundua kwamba ukosefu wa ushindani wa kimaendeleo si jambo jema. Unadumaza maendeleo kwa ujumla. Kunapokuwa hakuna changamoto kutoka upande wowote ni vigumu jamii kupaona mahali ilipozembea ili ipafanyie kazi. Kwa maana hiyo kutoweka kwa ushindani wa kimaendeleo uliokuwepo kati ya jamii ya Wachagga na jamii ya Wahaya ni jambo ambalo haliwafurahishi Wachagga, pamoja na kuonekana kwa sasa wako mbele ya Wahaya kimaendeleo. Kumbe Wachagga wangependa ule ushindani wa karibu kati yao na Wahaya uendelee ili uzidi kuchochea kasi ya maendeleo.
Ukweli wa jambo hilo umedhihirishwa na uteuzi wa Kanali Fabian Massawe, Mchagga, kuwa mkuu wa mkoa wa Kagera. Katika maneno yake, Kanali Massawe, anaonyesha kutoka rohoni mwake jinsi anavyosononeshwa kuuona mkoa ambao ulikuwa ukitamba kwa maendeleo ukiwa ni mfano kwa ajili ya mikoa mingine kuiga, ulivyorudi nyuma kwa kasi ya kutisha. Ni kwa sababu hiyo Kanali Massawe ameamua kuupeleka mchakamchaka mkoa huo ili kujaribu kuurudisha katika kiwango ulichokuwa nacho huko nyuma.
Moyo huo alio nao Massawe wa kuuinua mkoa wa Kagera siwezi kusema kwamba unatokana na bidii tu ya uchapa kazi, ni lazima kuna kitu cha ziada, kuna msukumo wa ziada. Na msukumo huo ni historia niliyoiongelea kidogo hapo juu.
Sio kwamba mkoa huo mpaka unadorora kiasi hicho haukuwa nao wakuu wa mkoa, maana kwa kipindi cha karibu miaka 30 na zaidi mkoa huo umekuwa nao wakuu wa mkoa kadhaa wakichapa kazi ila kwa namna tofauti na namna anavyofanya Massawe kwa wakati huu. Waliomtangulia walichapa kazi lakini hatahivyo mkoa ukawa unarudi nyuma badala ya kusonga mbele.
Pia wapo waliokuwa wakienda Bukoba kwa vitisho wakisema kwamba mkoa huo muda wote umekuwa juu kimaendeleo kwahiyo ingebidi ufunge breki na kuisubiri mikoa mingine. Vilevile yupo aliyewahi kutamka kwamba mie nimekuja kiboko yenu mtanitambua! Katika hali kama hiyo ni kitu gani kingeuzuia mkoa huo usidorore?
Kwa kuyakumbuka hayo ndiyo maana nasema utendaji wa Massawe una kitu cha ziada zaidi ya uchapa kazi. Massawe ni lazima anasukumwa na historia ya jamii ya mkoa wake na ile ya jamii ya mkoa anaoutumikia kwa sasa. Bilashaka anashangazwa na kusikitishwa na tofauti inayojionyesha kwa sasa kati ya jamii hizo mbili, jamii zilizokuwa zimekabana kimaendeleo miaka ya nyuma.
Kwa kuzitumia sifa alizo nazo Massawe ameanza kuonyesha matumaini ya kuuinua mkoa wa Kagera na kutaka kuurudisha tena kwenye chati. Na kwa vile anaonyesha dhamira inayotoka rohoni mwake, dhamira yenye msukumo wa kihistoria, sina shaka atafanikiwa kutimiza lengo. Lengo la kuuona mkoa wa Kagera ukirudi katika ushindani wa kutambiana kimaendeleo na mkoa wa Kilimanjaro pamoja na mikoa mingine ambayo nayo kwa sasa imechomoza kimaendeleo.
Kama ninavyoonyesha,  Massawe ni kamanda msitaafu wa jeshi. Hiyo ni sifa ya kwanza inayoonyesha kuwa mkuu huyo wa mkoa yuko tayari kuongoza katika hali yoyote ngumu. Sababu kama alikuwa tayari kuongoza katika hali ya vita, au katika vita, sioni ni ugumu gani utakaomfanya ajione mnyonge katika hali ya amani na kushindwa kuwaongoza raia dhidi ya ufukara usio na silaha wakati alizoea kuwaongoza wanajeshi katika mapambano ya silaha.
Sifa nyingine ni kwamba yeye ni mwalimu kitaaluma. Mwalimu anazo mbinu na maarifa ya kumwezesha mtu kukielewa kilichokusudiwa. Kwa sifa hiyo Massawe anayo nafasi ya kuwafanya wana Kagera wauone ukweli wa kwamba wamerudi nyuma sana kutoka pale walipokuwa miaka ya nyuma, na si kuuona ukweli huo tu bali kuuchukia na hivyo kutamani kurudi kwenye nafasi yao waliyokuwepo na hata zaidi.
Fikiria Wahaya, kabila moja  maarufu mkoani Kagera, lililokuwa linajivunia elimu kiasi cha kujulikana kiutani nchi nzima kama “nshomile” kwa maana ya nimeelimika, sasa hivi shule zilizo katika maeneo yao ndizo zinazofanya vibaya zaidi katika mitihani ya taifa! Neno “nshomile” limebaki kutumika  tu katika utani uliojaa kebehi. Haiwezekani watu wa jamii hiyo wafanye madudu kielimu halafu neno  hilo liendelee kuwa na maana.
Lakini kulingana na mikakati aliyonayo Kanali Massawe kwa upande wa elimu, na ikizingatiwa kuwa yeye ni mwalimu kitaaluma, nina imani kwamba atawarudisha akina “nshomile” kwenye majivuno yao hayo yakiwa ya kweli na siyo majivuno ya kubaki wameegemea kwenye historia ya kwamba iliwahi kutokea eneo lao likatoa wasomi. Yeye anataka Bukoba na Kagera kwa ujumla paendelee kutoa wasomi wa kweli kweli kama ilivyo mkoani Kilimanjaro, kusudi wengine watakapokuwa wanasema wale ni akina “nshomile” wawe ni nshomile kweli na siyo kebehi.
Kudorora kwa mkoa wa Kagera kulikuwa kumeingilia tabia mpaka tamaduni za watu wa mkoa huo! Mfano kabila la Wahaya ni moja ya makabila yenye utamaduni wa usafi hapa nchini. Ni utamaduni huo uliowaepusha na milipuko ya ugonjwa wa kipindupindu ambayo imeyasakama makabila karibu yote nchini isipokuwa Wahaya tu. Lakini kwa miaka ya karibuni utamaduni huo ulianza kuingiliwa na kuonekana kama unabadilika. Hali halisi ya mabadiliko hayo ilikuwa inajionyesha mara tu mtu alipokuwa anaingia katika mji wa Bukoba, mji ambao umo katika eneo la Buhaya. Uchafu ndio uliokuwa ukitangulia kumkaribisha mgeni aliyekuwa akiingia kwenye mji huo na kuyaonyesha mabadiliko yaliyokuwa yanaukabili utamaduni wa Wahaya.
Kwa sasa jambo hilo nalo linaonekana kushughulikiwa kiukamilifu na Kamanda Massawe. Kwa mujibu wa mwandishi Joyce Lobozi aliyeongea na mkuu huyo wa mkoa hivi karibuni, Kanali Massawe anasema mwitikio wa wananchi katika kuyaweka mazingira kwenye hali ya usafi ni mzuri. Na yeye amejipangia kila siku ya Alhamisi kuwa siku ya kukagua usafi katika maeneo mbalimbali mkoani humo. Kwa maana hiyo Bukoba bila uchafu inawezekana, kama ilivyowezekana huko nyuma.
Pamoja na hayo yote ningependa nimkumbushe Kamanda Massawe  kitu kimoja . Ni kwamba mganga yeyote hawezi kuutibu ugonjwa asiouelewa. Mtu anayeumwa tumbo lakini akienda kwa mganga anadai anaumwa kichwa ni vigumu kupata msaada wa mganga.
Ni kwamba tofauti na ilivyozoeleka kwamba Wahaya ni watu wanaojipendelea, ukweli ni kwamba Wahaya ni watu wa ajabu sana. Tunaweza kujiuliza, iweje watu wanaojipendelea maendeleo yao yarudi nyuma kwa kasi ya kutisha kiasi hiki? Hilo ni tatizo la kuumwa tumbo lakini kwa mganga ukadai unaumwa kichwa, mganga atatibu kichwa huku tumbo likiendelea kukusumbua.
Tatizo la kweli linaloisumbua jamii ya Wahaya, jamii kubwa kuliko zote mkoani Kagera, liko hivi. Wahaya hawana umoja wala mshikamano. Anapotokea mmoja akapatwa na tatizo inakuwa shangwe kwa wengine, wataanza kusema, muache aipate…..kakoma kuringa…..kaisha yule nakadhalika. Likimpata mwingine naye itakuwa hivyohivyo. Hawana wazo la kuunganisha nguvu ili kulikabili tatizo linaloanzia kwa mmoja kusudi lisisambae kwa wengine. Matokeo yake ndiyo haya, mkoa uliokuwa kinara sasa unaburuza mkia!
Akitokea mtu kwenye jamii ya Wahaya akatoa wazo lenye manufaa kwa jamii nzima ni nadra sana wazo hilo kuungwa mkono wala  kukubalika. Imani iliyozoeleka ni ya kwamba mtoa wazo ataringa iwapo wazo lake litaleta mafanikio. Kwahiyo ili kumkomoa, bila kuelewa kuwa wanajikomoa wenyewe, watalipinga wazo hilo kwa nguvu zao zote. Mambo yatalala doro, watabaki kwenye shida ileile ilmradi wasionekane wamemnufaisha aliyetoa wazo la kuimaliza shida inayoleta usumbufu.
Jambo lililotokea kuwa maarufu sana kwa akina “nshomile” ni kwamba pakitokea mtu akapata nafasi ya juu atahakikisha chini yake anapajaza na watu wa jamii yake, lengo si kuwainua, atahakikisha wanabaki hapo muda wote wa uhai wake, ili aweze kuwapata watu wa kumsujudia kwa gharama raihisi. Wasiolielewa tatizo hilo wanawachukulia watu hao kuwa wanajipendelea na wana ukabila!
Kwa ufupi ni kwamba kwa kiasi kikubwa maendeleo ya mkoa wa Kagera yamerudishwa nyuma na hulka hizo za ajabu za wakazi wa mkoa huo. Kwahiyo mtu wa kuusaidia mkoa huo ni lazima kwanza atafute namna ya kuwashawishi wakazi wa mkoa huo wajaribu kubadili tabia na mitazamo yao, hasa tabia ya “kantamuhira” neno lenye maana ya sitaki niungue kwa ajili yake,  neno linaloleta maana ya kuwa na roho ya korosho.
Nimeyasema haya kwa nia njema kabisa ili Kamanda Massawe aweze kulijua tatizo lililojificha na kutafuta namna ya kulipatia tiba, kama kweli amedhamiria kuuona mkoa wa Kagera unainuka tena na kurudi kwenye ushindani wa kimaendeleo na mkoa wa Kilimanjaro kama ilivyokuwa tangu zamani. Maana Waswahili walisema kwamba mficha maradhi…..msomaji utamalizia mwenyewe.
Tahadhari yangu kwa Kamanda Massawe ni kwamba katika uchapaji kazi wake aiache demokrasia ichukue mkondo wake. Historia inatuonyesha kwamba wote waliojaribu kutumia uchapaji kazi wao kama kishawishi cha kuichokonoa demokrasia waliishia kuangamia bila kupewa shukurani yoyote kwa mambo mazuri waliyokuwa wameyatenda.
Nimalizie kwa kueleza kiini cha matumaini niliyonayo  kwa Kamanda Massawe. Nimemfahamu Kanali Fabian Massawe tangu akiwa Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee iliyo chini ya Jeshi la Kujenga Taifa, Mgulani, Jijini Dar es salaam. Mafanikio aliyoyaonesha katika shule hiyo, kutoka shule changa  hadi kufikia kuwa shule ya kuchuan na   shule  kongwe za Jijini Dar es salaam na katika taifa kwa ujumla, ni mafanikio yasiyo ya kubeza. Ni mafanikio hayo yanayonipa imani kuwa hata kule Kagera ataweza.
Wahaya wanasema “ebitagira mahyo tibyera”, ndiyo maana hata mimi nataka nimshukuru Kamanda Massawe kwa lugha yake, “Eka Massawe saa”. Najua kule Bukoba watakuwa wanamuita Mangi kama tulivyozoea kuwaita wanaume wa Kichagga kote tunapowaona.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau