Bukobawadau

MKOA WA KAGERA WAKAMILISHA MAANDALIZI YA UZINDUZI WA MBIO ZA MWENGE KITAIFA MWAKA 2014

Mkoa wa Kagera unaendelea kukamilisha maandalizi ya Uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa utakaofanyika Mei 2, 2014 katika Uwanja wa Kaitaba Manispaa ya Bukoba kuanzia saa 1: 00 asubuhi na kuendelea.
Katika kuhakikisha kila shughuli iliyopangwa siku ya uzinduzi inafanyika kama ambavyo imepangwa Katibu Tawala Mkoa wa Kagera Bw. Nassor Mnambila ametembelea uwanja wa Kaitaba uliofanyiwa marekebisho makubwa na kujionea Halaiki ya watoto iinavyoendelea na mazoezi yake.
Katika kutembelea uwanja  huo Bw. Mnambila, zilifanyika shughuli zote zitakazofanyika siku hiyo ya uzinduzi hasa watoto wa halaiki kuimba na kuonyesha vitendo kwa kuumba maneno mbalimbali na mfano wa Mwenge wa Uhuru ili kuhakikisha muda unazingatiwa siku ya uzinduzi.
Aidha  Bw. Mnambila alitoa taarifa fupi kwa waandishi wa habari  kuhusu maandalizi yalipofikia hivi sasa kwa kusema kuwa maandalizi hayo mpaka yanaendelea vizuri na yamegawanyika katika sehemu kuu nne ambazo ni Kama ifuatavyo.
Kwanza ni Marekebisho ya Uwanja wa Kaitaba ambao umefanyiwa marekebisho makubwa ya  ujenzi wa vyoo vipya viwili, kurudisha mfumo wa maji, kuezeka majukwaa ya pembeni matatu na  kurekebisha viti vyake, Kupakaa rangi na kuzungushia uzio mpya wa ndani, kazi ambazo zipo katika hatua za mwisho kabisa.
Pili, Halaiki ya watoto, Bw. Mnambila aliwajulisha  Waandishi wa Habari kuwa watoto wa Halaiki kwa hivi sasa wameishaiva kupitia walimu wao na kinachosubiriwa ni siku yenyewe  ya uzinduzi aidha bado wanaendelea kufanya mazoezi ili kujiimarisha vizuri zaidi.
Tatu ni Wageni waalikwa  ambapo alisema kuwa wageni wa Kimataifa, Kitaifa na Mkoa tayari wamepelekewa mialiko ya  kushiriki uzinduzi huo ili wahudhurie na kushiriki na wananchi wa Mkoa wa Kagera siku ya tarehe 2/05/2014

Nne Bw. Mnambila aliwashukuru Wadau, Watu binafsi, Taasisi mbalimbali, Wabunge  na wananchi wote ambao waliombwa na kutoamichango yao  kuchangia uzinduzi huo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2014.

Mwisho kabisa Katibu Tawala wa Mkoa wa KageraBw. Mnambira aliwaomba wananchi wa mkoa wa Kagera kuhudhuria kwa wingi siku ya Uzinduzi ili kushiriki pamoja katika tukio la kihistoria kwa Mkoa wa wetu  Kuzindua Mbioa za Mwenge wa Uhuru Kitaifa

Imeandaliwa na:Sylvester Raphael
AFISA HABARI
RS-KAGERA@2014
Next Post Previous Post
Bukobawadau