Bukobawadau

NASAHA ZA NYERERE UGHAIBUNI

Katiba mpya, Nyerere anapotumika kuwakwamua majirani  wakati sisi tumekwama!
 
Na Prudence Karugendo
 
NAPENDA misemo ya wahenga kwa vile mara zote huonekana  imelenga mbali. Wahenga wa Kihaya walisema kwamba “ente ya ahai telya bunyasi bwaho”. Maana ya usemi huo ni kwamba ng’ombe hali nyasi zilizo karibu na anakoishi. Kawaida ng’ombe huwa anapelekwa mbali kwa ajili ya malisho akiziacha nyasi zilizo karibu  na anakoishi zije kuliwa na ng’ombe wengine kutoka mbali na hapo.
 
Hebu tuuangalie mfano wa usemi huo wa wahenga wa Kihaya ndani ya jamii yetu. Watanzania tumekuwa tukijivunia jina la Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, hili ni jina la mtu ambaye kwa mapenzi yetu kwake na mapenzi ambayo yeye mwenyewe alikuwa nayo kwa nchi yake na watu wake, tumeamua kumtunukia  hadhi ya Baba wa Taifa.
 
Busara na hekima za Nyerere katika kutetea usawa na usahihi wa kila jambo ziliwafanya watu wa mataifa ya mbali kutamani kwamba bora mtu huyo angekuwa anatoka katika mataifa yao. Mfano, Rais Joachim Chisano wa Msumbiji, wakati wa kuuaga mwili wa Mwalimu pale Uwanja wa Taifa, kwa majonzi makubwa alitamka kwamba “Watanzania na wananchi wa Msumbiji sote tunalia kwa sababu Baba wa Taifa wa Tanzania ni Baba wa Taifa wa Msumbiji”.
 
Kauli hiyo ya Chisano ilikuwa na maana ndefu zaidi ya ilivyofikiriwa kuwa pengine ililenga katika urafiki na udugu kati ya Tanzania na Msumbiji. Hiyo ni kutokana na kwamba Chisano alitamka na tukamsikia tukiwa tumemuelewa katika mazoea ya urafiki na udugu wa nchi hizi mbili. Lakini kuna watu ambao hawakuwahi kulitamka hilo pamoja na kwamba walilitamani sana, au wengine walitamka na hatukulisikia kutokana na kutokuwa nao karibu.
 
Katika gazeti moja la nchini Marekani iliwahi kuandikwa tahariri kwamba Nyerere alipaswa kuzaliwa katika nchi kama Marekani lakini bahati mbaya akazaliwa Tanzania! Hiyo yote ni katika kuonyesha thamani aliyokuwa nayo kiongozi huyo muasisi wa taifa letu, thamani ambayo sisi Watanzania naona tunashindwa kuifanyia kazi zaidi ya kubaki tunaimba tu “Baba wa Taifa Baba wa Taifa” huku tukifanya mambo yasiyo na uwiano hata kidogo na thamani ya jina la mtu huyo tunayemtumia kuringa kuwa ni Baba wa Taifa bila jitihada zozote za kuhakikisha tunanufaika na uadhimu wake.
 
Wahaya wanasema “ente ya ahai telya bunyasi bwaho”. Wakati Watanzania tunashindwa kulitumia jina la muasisi huyo wa taifa letu kujikwamua katika mambo mbalimbali walau hata kujaribu kuzitumia nasaha zake kutatua baadhi ya mambo yanayotuelemea, wenzetu wa nje wanazitumia sanaha zake kupata ufumbuzi wa matatizo yao.
 
Kwa sasa nchini mwetu kuna mahitaji ya Katiba mpya. Haya ni mahitaji yanayoonekana hata kwa kipofu. Mambo yetu yanaenda ndivyo sivyo huku baadhi ya watu, hususan waliomo katika  mfumo wetu wa utawala, wakijinufaisha na katiba iliyopitwa na wakati. Katiba iliyoandikwa wakati wa udikteta wa chama kimoja cha siasa,  lakini inaendelea kufanya kazi hata  wakati ambapo tunajidai tumo kwenye demokrasia ya mfumo wa vyama vingi vya siasa!
 
Nchi nyingi katika bara letu, hususan katika ukanda wetu huu wa Afrika Mashariki, zimepitia katika udikteta wa chama kimoja cha siasa ingawa karibu zote kwa sasa zimo katika kinachoitwa mfumo wa kidemokrasia ya vyama vingi vya siasa. Nasema hivyo kutokana na mfumo huo kutopewa nafasi ya kufanya kazi ipasavyo.  Kama tunavyoelewa mfumo huu umekuja kwa shinikizo wakati watawala wengi walikuwa bado hawajajiweka sawa kuupokea. Zipo sababu zilizokuwa zinawafanya watawala  wasiufurahie mfumo huo wa kidemokrasia na hivyo kulazimika  kuupokea shingo upande, mfumo ukarasmishwa kimaneno huku katiba za nchi zikiendelea kubaki zilezile zinazotambua udikteta wa chama kimoja cha siasa. Kimaneno Katiba inasema vyama vingi vya siasa lakini kimatendo ni kama Katiba inavilaani vyama hivyo na kubaki inakitambua chama kimoja pekee kilichohusika kuiandika.
 
Nchi nyingi zimepigana kufa na kupona kuhakikisha katiba za nchi hizo zinabadilika kulingana na  matakwa ya wakati. Moja ya nchi ambazo zimefanikiwa kuandika katiba mpya, siyo kubadili kwa kuchomeka viraka kama ilivyo hapa kwetu, ni Kenya. Zilifanyika kampeni za kuwaelimisha wananchi wa Kenya  juu ya mahitaji ya kuandika katiba mpya nchini mwao. Wapo waliokuwa wanaona katiba yao ya zamani  inafaa kwa wakati huu na hivyo kutoona umuhimu wa kuandika katiba nyingine. Kwa maana hiyo ikabidi ifanyike kura ya maoni kuona ni upande upi unakuwa na nguvu kati ya ule unaoona umuhimu wa kuandika katiba mpya na ule unaosema iendelee ileile ya zamani.
 
Ni katika kampeni hizo za kuwashawishi wananchi kukubali kuandikwa kwa katiba mpya ambapo kulijitokeza kitu ambacho ndilo lengo langu la makala hii. Katika sehemu maarufu kwa mikusanyiko ya hadhara,  Uhuru Park,  Jijini Nairobi, Makamu wa Rais wa sasa, Kalonzo Musyoka, katika jitihada zake za kuinadi katiba mpya alitumia nasaha za Baba wa Taifa la Tanzania, Mwalimu Julius K. Nyerere, kuwashawishi Wakenya kukubali kuandikwa kwa katiba mpya ya nchi yao na Wakenya wakamuelewa bila tatizo lolote.
 
Kalonzo Musyoka aliwauliza wananchi waliokuwa wanasikiliza kampeni hizo, kama walikuwa wanamkumbuka Mwalimu Julius Nyerere,  wote wakasema wanamkumbuka, akawauliza tena ni nani? Kwa pamoja wananchi wakasema Baba wa Taifa wa Tanzania. Akasema sawa, yule alikuwa ni mwalimu, akasema Mwalimu Nyerere aliwahi kufundisha juu ya katiba ya nchi, maana yake na umuhimu wake kulingana na wakati inapohitajika.
 
Kusema ukweli, nikiri kwamba somo alilokuwa analiongelea Kalonzo Musyoka kutoka kwa Nyerere nilikuwa sijawahi kulisikia. Musyoka akawaeleza wananchi kuwa Mwalimu Nyerere aliwahi kusema kwamba katiba ya nchi ni kama mtoto. Mtoto anapozaliwa anafurahiwa na wazazi wake, wanamnunulia nguo za utotoni. Lakini kadri mtoto anavyokua ni lazima wazazi waendelee kumnunulia mtoto nguo nyingine kwa vile zile za awali atakuwa tayari kaishazizidi. Kwahiyo eti wazazi wanaompenda mtoto wao hawawezi kuzing’ang’ania zile nguo za uchanga za mtoto wao kuwa ndizo zinazomfaa bila kununua nyingine. Kwahiyo kwa nasaha hizo za Mwalimu Kalonzo Musyoka akawa amewashawishi Wakenya kuunga mkono kuandikwa kwa katiba mpya. Wakenya wakawa wamenufaika na nasaha za Baba wa Taifa wa Tanzania.
 
Wakati Kenya wanafurahia Katiba mpya ya nchi yao waliyoizindua kwa mbwembwe kana kwamba ndipo wanapata uhuru wao, sisi Tanzania bado tunaendelea kuing’ang’ania katiba iliyochakaa ikiwa imepachikwa viraka kila sehemu. Tunapaswa tujiulize, Watanzania tuna tatizo gani? Ina maana Kenya wanatuzidi akili kwa kiasi  hicho cha kutamani kitu kipya wakati sisi tunaona kilichochakaa ndicho kinachotufaa?
 
Inawezekana Kenya nako walikuwepo ving’ang’anizi ambao walikuwa hawapendi mabadiliko ya katiba yao, lakini wakaja kulainishwa na nasaha za Baba wa taifa wa Tanzania, sasa inakuwaje ving’ang’anizi wa Tanzania washindwe kulainishwa na nasaha za Baba wa Taifa lao ambazo alikuwa anazitoa kila kukicha mpaka mwisho wa uhai wake? Hapa ndipo ninapokubaliana na wahenga wa Kihaya kuwa “ente ya ahai telya bunyasi bwaho”,  ng’ombe hali nyasi za karibu na anakoishi.
 
Yapo mambo mengi ambayo Mwalimu alikuwa anatuhasa kutoyafuata ili kulinda maadili yetu na heshima yetu. Lakini mambo hayo kwa sasa ama yanafuatwa au kukiukwa kulingana na mahitaji ya kila kundi katika jamii yetu. Cha ajabu hata yaliyo machafu yanaweza yakafanyika kwa madai ya kwamba wakati uliopo unakinzana na wakati ule ambao baadhi ya mambo yaliharamishwa. Lakini linapokuja suala la katiba ya nchi wakati ule wa zamani ilipoandikwa katiba tuliyo nayo unakuwa sawasawa kabisa na wakati tulionao kwa sasa! Ndipo yanapojitokeza madai ya kwamba kwani katiba tuliyo nayo ina matatizo gani?
 
Tuliona jinsi Azimio la Arusha, kwa mfano, azimio ambalo Mwalimu amekufa nalo mfukoni mwake akiamini kwamba ni azimio la utu, lilivyozikwa kirahisi kule Zanzibar. Hapakuwepo na kura ya maoni au kuwashawishi wananchi kwa namna yoyote kulikataa azimio hilo kwanza  ndipo yafanyike mabadiliko. Viongozi peke yao walikaa Zanzibar na  kuamua kulifuta kinyemela baada ya kuona linakinzana na maslahi yao.
 
Kwahiyo kitu ambacho kinakinzana na maslahi ya viongozi, hata kama kwa wananchi ni muhimu na kizuri kiasi gani, ni rahisi kubadilishwa. Lakini kitu ambacho ni muhimu kwa wananchi na kwa mustakabali wa nchi, kama kinaonekana hakitaleta manufaa kwa watawala kinakuwa kigumu kubadilika. Kitaendelea kuchomekwa viraka kulingana na matakwa ya watawala mpaka wakati usioeleweka.
 
Lengo langu katika makala hii ni kuonyesha jinsi Watanzania tunavyoshindwa kujinufaisha na mambo tuliyojaaliwa kuwa nayo zikiwemo nasaha za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere. Kama ilivyo kwa raslimali zote tulizo nazo ambazo zinawanufaisha watu wa nje, hata nasaha za Mwalimu zinaonekana kuwanufaisha wageni sisi tukibaki tumetumbua macho kama viziwi. Haya,  Kenya wameandika katiba mpya wakizitumia nasaha za Mwalimu kama mwongozo wa kufikia mafanikio hayo, sisi tunalia na katiba iliyojaa viraka. Tunashindwa kuzitumia nasaha za Mwalimu kupata katiba mpya wakati Mwalimu alikuwa ni wetu na Baba wa Taifa!
 
Hata kama nchi yetu si ya kishirikina lakini kwa hili ni lazima tumtafute mchawi, maana hii si bure. Wenzetu kunufaika kwa kitu ambacho sisi tumekikalia huku pengine tukihitaji msaada kwao utakaotoka na kitu kilekile tulichokikalia si jambo la kawaida. Kama ni usingizi basi huu umepita kiasi, tusipojihimu si ajabu tukapitiliza na huo kuwa mwisho wetu.
 
 
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau