Bukobawadau

TUSIACHE ULAZALENDO WA LEMBELI USAKAMWE NA WANAMAKUNDI

Na Prudence Karugendo
JAMES  Lembeli ni mbunge wa Kahama kupitia chama tawala, CCM. Lakini uanachama wake kwa chama hicho haumvui uzalendo wake kwa nchi yake wala mapenzi yake  kwa  wananchi wenzake.  Hataki kuutumia uanachama huo kuwaona wananchi wengine wasiokuwa wanachama wa chama chake kama maadui zake. Vilevile hataki kuutumia uanachama huo kuitelekeza nchi yake.
Lembeli kajiweka wazi kuwa anauvua umakundi wote, u CCM na utetezi wa kundi la wana Kahama, na badala yake kuuvaa uzalendo wa nchi  linapokuja suala la kuitetea na kuihami nchi yake. Huo ni uzalendo uliotukuka  kwa nchi.
Katika hilo Lembeli hana u CCM wala u Kahama, anabaki na kundi moja tu, nalo ni kundi la wananchi ambalo anataka liidai nchi yao ya Tanganyika.
Ikumbukwe kwamba uzalendo katika umakundi ni adui mkubwa wa uzalendo katika nchi. Wananchi hawawezi wakazama kwenye uzalendo wa kamundi yao wakaukumbuka tena uzalendo wa nchi yao. Mfano hai ndio huu ambapo baadhi ya wananchi wanakiona kikundi chao ndicho bora kuliko kila kitu. Kikundi chao kinaikana nchi yao, hakitaki hata kulisikia jina la nchi yao wao wanashangilia!
Wanausimamia msimamo wa kikundi chao mpaka kufikia kulionea kinyaa jina la nchi yao na kubaki wakilitukuza jina la kikundi chao, ambacho ni kikundi kidogo tu cha wananchi!
Fikiria nchi iliyo na idadi ya watu wanaokaribia milioni 50, watu wazima kwa watoto, vikongwe kwa walemavu nakadhalika, eti matakwa yao yatawaliwe na kikundi cha watu wasiofikia hata milioni 5 kikijiona ndicho pekee chenye  maamuzi juu ya mamilioni  ya watu hao wote!
Tukiangalia kwenye historia tutaona kwamba umakundi ulijionyesha tangu zamani kuwa ni adui wa uzalendo. Ndio maana wakoloni walibuni mbinu ya kuwagawanya wananchi katika makundi na kuyajengea uhasama kati ya kundi moja na lingine kusudi makundi hayo yasielewane na ikibidi yaishie kwenye ugomvi.
Mbinu hiyo ya wakoloni iliyopata umaarufu kama “divide and rule” gawanya utawale,  iliwasahaulisha wananchi uzalendo kwa nchi zao, na badala yake wananchi wakauhamishia uzalendo wao kwenye makundi ambayo lakini hayakuwasumbua wakoloni zaidi ya wananchi kupigana wenyewe kwa wenyewe huku wakoloni wakitawala bila misukosuko yoyote!
Kwa kulitambua hilo, Lembeli akatamka bila woga wala unafiki, kwamba yeye ni Tanganyika kwanza mengine baadaye. Uzalendo huo wa Lembeli ni tofauti na msimamo wa chama chake kilichozama kwenye umakundi zaidi kikiwa kimeusahau uzalendo pembeni.
Hapo ndipo Lembeli akatoka na kauli ya kwamba CCM siyo mama yake, kauli iliyowahi kutolewa na muasisi wa chama hicho, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.
Tafsiri ya neno hilo iko wazi. Ni kwamba CCM ni kikundi kilichoasisiwa na watu, kwahiyo kujiunga au kuachana nacho ni ihari ya mtu kwa kutegemea anavyouona mwenendo wa kikundi hicho.
Kikundi hicho hakijamuumba wala kumzaa mtu yeyote. Mtu anaweza akajiunga na kikundi hicho akiwa anaelewa kwamba wazazi wake, au mabibi na mababu zake hawakuwa kwenye kikundi hicho,  na pengine wengine hawakukijua kwa vile hakikuwepo enzi hizo.
Hiyo ni tofauti na nchi ambayo mtu kazaliwa na kukuta wazazi wake na mababu zake wana asili ya nchi ileile. Hivyo kuyaondoa mapenzi kwa kikundi na kuyaweka kwa nchi ni jambo linaloweza kuwashangaza tu  watu wenye matatizo ya kimtazamo.
Baada ya kauli ya Lembeli ya kwamba CCM siyo mama yake  wakazuka wapambe wa chama hicho, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, mjumbe wa NEC ya CCM, Boniface Butondo, Katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga, Adam Ngalawa na Katibu Mwenezi wa CCM mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Mlimandago, wakidai kwamba Lembeli kakidhalilisha chama chao!
Watu hao hawasemi Lembeli kakidhalilisha vipi chama chao. Kusema CCM siyo mama yake! Hivi kweli wapambe hao wanaweza wakatuhakikishia kuwa CCM ndiyo iliyobeba mimba ya Lembeli kwa miezi tisa? Kama hawawezi kufanya hivyo basi waelewe kuwa wao ndio wamemdhalilisha yeye na wawe tayari kumuomba radhi.
Katibu wa CCM mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Mlimandago, anadai kwamba Lembeli anajifananisha na Baba wa Taifa, sijui anajifananisha naye kwa lipi! Sababu hakuna mahali ambako Lembeli alitamka kwamba kwa sasa anaongea kama Nyerere.
Isipokuwa hizo ni hisia tu za Mlimandago za kumsikia Lembeli akitoa kauli ambayo CCM ilishindwa kuipiku tangu enzi za Nyerere. Leo hii ndipo anasema Lembeli kajifananisha na Nyerere!
Pengine ninachoweza kukiona ni kwamba Lembeli kaufuata uzalendo wa Nyerere, kwa hilo kuna kosa gani? Nyerere kama muasisi wa Tanganyika, sidhani kama kuna kosa iwapo wananchi wote wakiamua kufuata nyayo zake. Hapo Mlimandago kachemsha.
Na kwa taarifa yake, Mlimandago, ni kwamba kauli hiyo Nyerere aliitoa kwa waandishi wa habari,  kama alivyofanya Lembeli, tofauti na anavyofikiria yeye kwamba Nyerere aliitolea kwenye vikao vya CCM. Pengine ingebidi tumfahamishe ni wapi na wakati gani Nyerere alitamka kwamba CCM siyo mama yake.
Ila sitaki tumpe faida ya kutekeleza majukumu yake anayoonekana kuyatekeleza kwa kuyumbayumba.
Wapambe hao wa CCM wanasema kwamba Lembeli atambue kwamba umaarufu wake alionao umetokana na CCM! Kwamba kabla ya mwaka 2005 hapakuwepo Watanzania waliomjua na  waliomfahamu kama ilivyo sasa!
Hiyo ni kauli ya ajabu lakini iliyozoeleka katika chama hicho. Sababu haina maana kwamba Lembeli kazaliwa mwaka huo wanaoutaja. Lembeli alikuwepo na wenye kumjua tulimjua. Juhudi zake ndizo zilizowafanya CCM wamtamani na waone kuwa anawafaa kukinadi chama chao wilayani Kahama mpaka wananchi wakaamini kuwa anawafaa kuwa mbunge wao. Sidhani kama CCM imemuongezea lolote mpaka hapo.
Kama suala ni CCM kumpa umaarufu, wapo makada wangapi wa CCM tusiowajua mpaka sasa? Kwa nini hao CCM haiwafanyi wawe maarufu kama kweli chama hicho kinao utaalamu huo?
Hata huyo Mlimandago ndio kwanza nimemsikia pamoja na hao wenzake, ukimuondoa Mzee Mgeja, wakijaribu kuukwea umaarufu wa Lembeli ili nao wajitengenezee umaarufu wa kwao. Kama kweli chama chao kingekuwa na utaalamu wa kuwatengenezea umaarufu makada wake kwa nini wao wamtegemee Lembeli ili wajulikane?
Jambo hilo linadhihirisha pasipo na shaka kuwa Lembeli katumia jitihada na akili zake binafsi, vikichangiwa na uaminifu na uzalendo wake, kujulikana. Wala sio juhudi za kikundi chake, CCM.
Ni kama wao wanavyofanya juhudi zao binafsi kwa kumtumia yeye kupata umaarufu, kwani wanaweza kusema kuwa hizo ni juhudi za chama?
Lembeli kaweka mbele uzalendo kwa nchi yake tofauti na wanaotanguliza mapenzi kwa vikundi vyao wakiwa wameusahau uzalendo kwa nchi yao. Kama hatabadilika, huo ndio mfano wa kuigwa.
Faida ya kuujali uzalendo kwa nchi ni pamoja na kuijali nchi yako ukiwa unawachukulia wananchi wote kama ndugu zako. Kwa namna hiyo ni vigumu kuwabagua baadhi ya wananchi ukiwaona kama watu wasiokutakia mema kwa vile hawako kwenye kundi lako.
Utakuwa huwezi kuushawishi uhasama miongoni mwa wananchi kutokana na kuwachukulia wote kama kitu kimoja ambacho wewe mwenyewe ni sehemu yake.
Siri ya Tanzania, tangu ikiwa Tanganyika, kuwa na kinachoitwa amani na utulivu kwa muda mrefu, ndiyo hiyo. Wananchi kujiona ni kitu kimoja wakiwa wameyatanguliza mapenzi kwa nchi yao na wao kupendana bila kuathiriwa na umakundi.
Lakini linapokuja suala la umimi, huyu ni wa chama changu na huyo ni wa chama kingine, anaweza akasababisha chama changu kikaanguka na kunifanya nikikose nilichozoea kukifaidi, uzalendo kwa nchi kupatikana ni muhali.
Mawazo ya watu yanazama kwenye makundi na kuwashawishi walio kwenye makundi tofauti wabaki wanatazamana kama maadui. Kinachojitokeza katika hali ya aina hiyo ni kujengeka mbinu za kundi moja kutaka kulitokomeza kundi lingine.
Hayo tumeyashuhudia katika chaguzi zinazofanyika kwa sasa ambapo mapenzi katika makundi, vyama vya siasa, yanawafanya watu watekane nyara, wafanyiane matendo ya kiharamia na kigaidi na hata kufikia kuuana. Katika hali ya aina hiyo hakuna anayeweza kuonyesha mapenzi kwa nchi yake.
Ikumbukwe yanayoitwa mauaji ya kimbari nchini Rwanda yalitokana na mtindo huo wa maisha. Kujigawanya katika makundi na kuutukuza mgawanyiko huo, thamani ya utu ikapotea na kubaki inaonekana tu thamani ya mgawanyiko! Matokeo yake ni maangamizi!
Lembeli kaamua kuuvaa uzalendo pasipo kuyajali makundi. Tumuunge  mkono ili walio na virusi vya umakundi wasimlazimishe kumuambukiza ugonjwa huo hatari kwa mabavu. Tukimtelekeza na kumuacha aambukizwe kwa kulazimishwa tuelewe kwamba sote hatutakuwa salama.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau