Bukobawadau

UMAMUMA KATIKA UONGOZI WA NCHI NI CHANZO CHA UHARIBIFU WA MAZINGIRA

Na Prudence Karugendo
 
MAZINGIRA ni uhai: Neno hilo tulifundishwa shuleni tangu madarasa ya awali. Tulikuwa tunafundishwa kwamba mimea ndiyo hutoa hewa ya Oksijen tunayoivuta pamoja na kuchangia upatikanaji wa mvua. Vilevile tulikuwa tukifundishwa kuwa mimea inalinda nchi isigeuke kuwa jangwa sambamba na kutokea upepo mkali (vimbunga) katika maeneo yasiyo na miti. Mambo hayo yote tulikuwa tukifundishwa tangu awali ili tukue tukielewa umuhimu wa kutunza mazingira.
 
Inastaajabisha kuona watoto wadogo wanafundishwa na kuelewa  umuhimu wa kulinda mazingira wakati watu wazima hawauoni umuhimu huo! Lakini sidhani kama hawa watu wazima ni kweli hawayahitaji mazingira, kama hawahitaji hewa ya oksijeni, hawahitaji mvua, kwamba wao wanatamani jangwa na vimbunga! Ukweli ni kwamba tofauti ya uelewa wa umuhimu wa kuyahifadhi mazingira kati ya watu wazima na watoto inasababishwa na majukumu yanayojitokeza katika mfumo wa maisha ya mwanadamu.
 
Wakati mtoto anategemea kila kitu kitoke kwa mzazi wake, chakula, mavazi, malazi, elimu nakadhalika, mzazi inambidi achangamshe akili kuweza kukabiliana na jukumu hilo. Na ndipo mzazi anapotumia kila kilicho kwenye upeo wake kama nyenzo ya kukabiliana na jukumu hilo, jukumu la malezi. Ni kwa kufanya hivyo binadamu anashtukia yumo kwenye uharibifu wa mazingira.
 
Mathalani, mzazi hawezi kuwaacha watoto wakakosa kupikiwa chakula eti kwa kuchelea kukata miti kwa ajili ya kuni, kutokana na kukosa nishati mbadala, wakati ukataji wa miti ni sehemu ya uharibifu wa mazingira.
 
Mtu mzima anachangia uharibifu wa mazingira pengine si kwa kutotambua au kutothamini umuhimu wake, bali anasukumwa na hali iliyomzunguka na kujikuta ameangukia katika uharibifu huo pale anapokuwa anapanga mikakati ya kukabiliana na hali hiyo kwa kutoa vipaumbele, kipi kianze na kipi kifuatie.
 
Katika hali ya  umasikini, kama hii ya kwetu Tanzania, ambayo asilimia kubwa ya wananchi wanaishi katika nyumba za miti na udongo, nani atakuelewa ukimwambia asikate miti ya kujengea kibanda chake cha kujihifadhi na familia yake eti kwa lengo la kutunza mazingira? Kati ya ustawi wa mazingira na uhai wa familia yake kipi kinaonekana kuwa na umuhimu zaidi ya kingine? Katika akili ya kawaida mtu anajali familia yake kwanza, mambo ya mazingira ni sawa na habari yoyote ya mitaani.
 
Baada kuonyesha, japo kwa ufupi, jinsi umasikini niliokuwa nautaja kama (hali), unavyotulazimisha kuharibu mazingira yetu, nataka nionyeshe pia jinsi maamuzi mabovu ya Serikali, ambayo kwa vyovyote vile yanapitishwa na uongozi mbovu, yanavyousaidia umasikini kulikuza tatizo hilo.
 
Neno uongozi, kwa maana nyingine, ni uelekezaji. Hii inaleta maana ya kwamba uongozi bora ni ule ulio na taswira ya jambo unaloongoza kulielekeza. Vinginevyo utakuwa ni uongozi kipofu ambao haufai kabisa sababu utakuwa unawaburuza wanaoongozwa kwenda kusikojulikana, kwa vile uongozi hauoni, matokeo yake yanaweza yakawa ni kuishia kwenye maangamizi!
 
Kwahiyo katika suala hili, uongozi wa nchi ilibidi uwe unayaona madhara ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na wananchi, si kwa mapenzi yao, bali katika jitihada za kukabiliana na hali ya umasikini uliowazunguka na kutishia uhai wao, na hivyo uongozi kuonyesha njia mbadala ambayo wananchi wangeitumia na kuyaacha mazingira yasitawi kwa manufaa yao.
 
Badala yake uongozi ndio unaokuwa wa kwanza kuzitia kufuli njia zote ambazo zingetumika ili kulinda mazingira na kuwalazimisha wananchi wazidi kujikita katika njia za asili. Njia mojawapo kuu ya uharibifu wa mazingira ni ya nishati.
 
Tangu mwanadamu agundue moto aliachana kabisa na matumizi ya vyakula vya porini vilivyokuwa vinaliwa bila kupikwa. Kwahiyo alianza kutumia kuni na baadaye mkaa kama njia kuu za kuendeshea nishati yake hiyo aliyoigundua. Na baadaye, kadiri akili zake zilivyozidi kukua, ndipo mwanadamu akagundua njia nyigine za kuzalisha na kutunza nishati hiyo kwa njia ya umeme. Sayansi ya umeme iligunduliwa ili iwe nyepesi na rahisi kuimudu na kuitumia badala ya ile iliyokuwa inapatikana kwa kupekecha vitu kama vijiti na kugonganisha mawe na hatimaye kutumia  kuni au mkaa ili iweze kufanya kazi.
 
Nishati ya umeme ni kati ya mambo yaliyopatikana kutokana na uvumbuzi wa teknolojia inayoendelea kuboreshwa kila kukicha. Teknolojia ipo kumrahisishia binadamu shughuli zake. Kwa maana hiyo nishati ya umeme nayo ipo kumrahisishia binadamu shughuli zake, siyo katika upatikanaji wake tu,  ambao ni tofauti na ule wa kupekecha miti na mawe ili moto upatikane, bali pia kumudu gharama zake. Ndiyo maana nishati ya umeme inapaswa kuwa rahisi kuliko karibu aina zote za nishati.
 
Nchi nyingi duniani umeme ni kitu cha lazima. Tena hii haitokani na hatua ya maendeleo ambayo pengine imefikiwa na nchi hizo inayoweza kulifanya jambo hilo lionekane kama mbwembwe zitokanazo na  jeuri ya maendeleo. Ukweli ni kwamba kinachotiliwa maanani ni tafsiri ya teknolojia katika kurahisisha maisha na shughuli za mwanadamu sambamba na kuhifadhi mazingira yanayomzunguka. Teknolojia ya umeme inavifanya vitu kama ukataji wa miti kwa madhumuni ya kuni na kuchoma mkaa vibaki kwenye historia tu.
 
Lakini jambo la kusikitisha ni kwamba hapa nchini kwetu  hali ni tofauti. Nishati ya umeme ni kitu ambacho kimefanywa kionekane ni cha anasa tu na hivyo kuishia kuwanufaisha wateule wachache! Sidhani kama nishati hii inafikia kiwango cha kukidhi japo robo ya umuhimu wake hapa nchini mwetu.
 
Tatizo linalotukabili ni la uongozi wetu  kuangalia pafupi. Ingekuwa uongozi wetu unaangalia mbele zaidi, sasa hivi si ajabu kila Mtanzania angekuwa anatumia umeme na hili tatizo la ukataji wa miti kwa ajili ya kuni na mkaa pengine lingeishatoweka.
 
Inaeleweka kwamba gharama za umeme na usambazaji wake inabidi zifidiwe. Sasa uongozi ungekuwa unaangalia mbele zaidi na kuliona janga lililo mbele yetu ambalo tunajaribu kuliepuka, janga ambalo linatishia zaidi vizazi vijavyo, tusingeng’ang’ania gharama za umeme zifidiwe na kizazi cha sasa tu kwa kupandisha viwango vya gharama za umeme kiasi cha kuwafanya wananchi waepukane nao na hivyo kubakia kwenye njia yao ya asili ya kupata nishati ambayo ni ya  mkaa na kuni.
 
Ikizingatiwa kuwa kinachofanyika leo si kwa ajili ya wanaoishi leo peke yao, suala hili la mazingira ingebidi litizamwe kwa upeo mrefu, bila ubinafsi wa kujijali sisi tunaoishi kwa sasa peke yetu.  Ieleweke kwamba uzembe wowote, katika suala hili la mazingira, utakuwa ni mzigo mkubwa kwa vizazi vijavyo. Kwa maana hiyo, hata gharama za umeme zingerefushwa mpaka kwa vizazi vijavyo,  kwa maana ya watumia umeme kuchangia kidogokidogo mradi waweze kumudu  gharama za matumizi yake. Bora vizazi vijavyo vikakuta deni la umeme hata kama ni la miaka mia mbili itakayokuwa imepita kuliko kukuta nchi ikiwa  jangwa.
 
Malengo ya muda mfupi yanayowekwa na uongozi husika ndiyo yanayo tuelekeza katika maangamizi. Haya ni malengo ambayo uongozi, kwa kusukumwa na tamaa ya kujinufaisha haraka haraka, hayazingatii kabisa masuala muhimu kama hilo la utunzaji wa mazingira.
 
Mfano, kinajengwa kiwanda cha saruji. Mtu atadhani lengo ni kuwawezesha wananchi kuwa na makazi bora sambamba na kulinda mazingira kwa kuwafanya wananchi waache kukata miti kwa ajili ya kujengea na badala yake watumie saruji. Ukweli unabainika pale kiwanda kinapoanza uzalishaji. Bei ya saruji inayopangwa bila kuzingatia kipato cha mwananchi ndiyo inayodhihirisha kuwa lengo la wenye kiwanda cha saruji ni kurudisha mtaji wao haraka iwezekanavyo na kutengeneza faida, na wala ujenzi wa kiwanda hicho cha saruji hauna uhusiano na utunzaji wa mazingira!
 
Ingekuwa Serikali (uongozi) inao mkakati wa kutunza na kuyalinda mazingira isingeshindwa kushauriana na hawa inaowaita wawekezaji, ili kuwapunguzia kodi au Serikali yenyewe kutoa ruzuku, kusudi saruji iuzwe katika kiwango ambacho mwananchi wa kawaida  anaweza kukimudu.
 
Kinyume chake Serikali ndiyo ya kwanza kuwakoromea wenye viwanda kwa vitisho vya kodi ambayo moja kwa moja inaingizwa kwenye bidhaa inayozalishwa na kuwafanya wananchi wazione bidhaa hizo kuwa siyo stahiki yao! Ung’ang’anizi huo wa kodi umo katika malengo ya muda mfupi ya uongozi wetu niliyoyataja hapo juu. Malengo ambayo yanalenga zaidi kujinufaisha bila kujali hatima ya nchi.
 
Sasa hivi tumo katika msukosuko wa ukame. Mito, mabwawa na hata maziwa vinatishia kukauka. Hii imechangiwa zaidi na utowekaji wa misitu kitu ambacho ni kama sumu kwa vyanzo vya maji. Mabwawa ya kuzalisha umeme nayo yamekauka, wenye kutumia umeme tunawaona wanavyohaha. Lote hilo ni tatizo la uongozi kukosa dira. Kama Serikali ingekuwa na malengo ya muda mrefu, ikawawezesha wananchi kutumia umeme, bila tamaa  ya kutaka kupata vipato vikubwa kwa muda mfupi, sasa hivi tusingekuwa tunaongelea tatizo hili la umeme.
 
Tatizo hili limekuja sababu watumiaji wa umeme ni wachache wakati wazalishaji wa umeme wanataka vipato vikubwa na kwa haraka, maana yake ni kupandisha zaidi viwango vya gharama ya umeme. Wananchi wa kawaida wakabaki kwenye nishati yao ya asili, kuni na mkaa. Matokeo yake ni misitu kutoweka, vyanzo vya maji kukauka na ukame kutamalaki.
 
Tamaa ya kujinufaisha kwa muda mfupi inayoonyeshwa na uongozi wa nchi bila kujali majaaliwa ya nchi yatakuwaje ni tatizo kubwa linalozikandamiza nchi za dunia ya tatu kwa kuyafanya matatizo yanayozikabili yazidi kurundikana badala ya kupungua kila kunapojitokeza kinachodaiwa kuwa ni jitihada za kupambana na matatizo hayo. Hiyo ni kwa sababu tamaa hii imetokea kuwa kivutio kikubwa  kwa manyang’au popote yalipo duniani, kuacha sehemu nyingine na kuamua kukimbilia kwetu.
 
Mifano hai ni miradi ya IPTL, Richmond, Dowans, Symbion na mingine ya aina hiyo. Miradi hiyo ilisukumwa zaidi na tamaa ya kujinufaisha haraka kuliko umuhimu wa miradi husika uliotokana na tatizo lililokuwa linatukabili kwa wakati ule. Wajanja walipiga mahesabu ikaonekana kwamba megawati  za umeme ambazo zingezalishwa zigelazimishwa zote kuuzwa TANESCO kwa kipindi fulani bila kujali kama zilikuwa zinahitajika na kutumika zote ama vinginevyo.
 
Matokeo yake ni TANESCO kulipa  mabilioni ya shilingi kila mwezi hata katika kipindi ambacho TANESCO ilikuwa haitumii hata uniti moja ya umeme wa makampuni hayo mumiani! Hiyo maana yake ni kwamba TANESCO nayo, ili kujinusuru, inabidi iwakamue wateja wake, wananchi, angalau ijaribu kufidia gharama za bure zinazopokwa na hao manyang’au.
 
Isingekuwa tamaa  ya kujinufaisha haraka kwa wachache, miradi ya makampuni hayo ikalenga kuwanufaisha wananchi wa Tanzania katika ujumla wao, kwanza pasingekuwepo na ulazima wa makampuni hayo kuiuzia TANESCO hata kile isichokihitaji,  TANESCO nayo isingelazimika kupandisha viwango vya uuzaji wa umeme wake  kitu ambacho kingekuwa kishawishi kwa wananchi kutumia umeme na kuhifadhi mazingira. Kinyume chake, makampuni hayo mumiani yanazalisha umeme yanaiuzia TANESCO, wananchi wanashindwa kuutumia umeme huo kutokana na gharama zake kuwa nje ya uwezo wao, wanabaki kutumia mkaa na kuni, misitu inaisha, maji yanakauka, umeme unaozalishwa na maji ambao ndiyo tegemeo la gridi ya Taifa karibu unazimika, ule wa wawekezaji hautoshi, basi kivumbi, tamaa  imezaa balaa!
 
Mfano mwingine wa wachache kuwa na tamaa ya kujinufaisha ndani ya matatizo yanayotukabili ni ule mradi wa gesi ya Songosongo. Niliwahi kuambiwa na mtaalamu mmoja aliyeshiriki katika utafiti wa gesi hiyo ya Songosongo kwamba gesi hiyo ikishapatikana ndiyo ungekuwa mwisho wa matatizo. Imani yake, mtaalamu yule,  ilikuwa kwamba kwa vile gesi ilikuwa inapatikana nchini mwetu tulikuwa na haki ya kuitumia jinsi ambavyo tungetaka tofauti na bidhaa nyingine za mafuta tunazoagiza kutoka nje. Kinyume cha matumaini yetu, naona sasa kuna kampuni inayojiita SONGAS inayojifanya kumiliki gesi hiyo na kutuuzia sawa na bidhaa nyingie za mafuta tunazoagiza kutoka Mashariki ya Kati!
 
Jambo lililonistua ni kwamba kuna mpango wa kuzuia uchomaji mkaa! Mbona mpango huu umekuja wakati usio wake? Kuna njia gani mbadala ambayo itatumiwa na wananchi karibia asilimia 98 ya Watanzania ambao uhai wao unategemea nishati ya mkaa? Na itakuwaje kwa zile asilimia mbili zilizokuwa zinategemea umeme na ghafla zikaugeukia mkaa baada ya umeme kutokuwa wa uhakika?
 
Kwa vile mambo yote yanafanywa kwa mtindo wa zima moto wakati yamesababishwa na uzembe wetu, inabidi tuchague moja kati ya mawili, ama tukubali kufa ili kulinda mazingira yetu, au tuyaache mazingira yaalibike kulinda uhai wetu.
 
 
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau