Bukobawadau

WANAOPINGA RASIMU YA KATIBA MPYA WANAMKANA JK

Na Prudence Karugendo
MWANZONI  kabisa alipoingia madarakani, Rais Jakaya Kikwete, alisema wazi kwamba jambo moja kubwa lililokuwa likisumbua kichwa chake ni kero zilizokuwa zikijitokeza kwenye Muungano wa Tanzania. Na kwa vile alikuwa amechaguliwa kuiongoza Tanzania ni wazi kwamba asingependa kuiongoza nchi yenye ugonjwa unaotishia uhai wake, uhai wa nchi aliyopewa kuiongoza.
Kwahiyo akaahidi kwamba kutokana na nafasi hiyo ya juu kabisa ya uongozi wa nchi aliyopewa na wananchi angejitahidi kadiri ya uwezo wake kuzitatua na kuzimaliza kero hizo zilizokuwa zikijitokeza kwenye Muungano. Hiyo ilikuwa ahadi ya kwanza na muhimu ya rais aliyekuwa ameingia madarakani.
Sasa rais anataka kukitimiza alichokiahidi chama chake kinamshika shati! Ni maajabu na kweli!
Kwa sasa kuna mchakato wa kuipata Katiba mpya ya nchi. Lakini ikumbukwe kuwa chama tawala, Chama Cha Mapinduzi, ambacho rais wetu ni mwenyekiti wake, hakikuwa kabisa na wazo la Katiba mpya. Hilo ni wazo la wapinzani ambao walipojaribu kulieleza Bungeni walichezewa mduara na wabunge wa CCM walio karibu robo tatu ya wabunge wote, ingawa wingi wao hauwiani kabisa na manufaa yao kwa wananchi.
Kuona hivyo wapinzani wakalichomoa wazo lao Bungeni na kulipeleka Ikulu kwa rais. Rais akaona mantiki yao, wazo la wapinzani likamkumbusha kero alizoahidi kuzishughulikia. Na kwa vile yeye ni rais wa watu wote, wakiwemo wapinzani, kinyume na mawazo ya wachache wanaomchukulia kama rais wa chama chake, akawaahidi wapinzani kuanzisha mchakato wa kuipata Katiba mpya.
Mpaka hapo tutaona kwamba rais alikuwa nalo wazo la Katiba mpya tofauti na fikira za wasaidizi wake na wapambe wa chama chake. Sababu bila hivyo ni vigumu mtu kukiridhia kitu ambacho haoni mantiki yake, na ikizingatiwa mtu mwenyewe ni rais aliye na mamlaka yasiyopimika wala kupingika katika jamii yake.
Kwahiyo JK akaunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba, akamteua Jaji Joseph Sinde Warioba pamoja na wajumbe wake, akawaapisha na kuwakabidhi kazi hiyo ya kuanzisha mchakato wa kuitafuta Katiba mpya.
Msisitizo ni kwamba kitendo cha rais kuwaapisha mwenyekiti na wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kinaleta maana ya kwamba watu hao wanaenda kufanya kazi kwa niaba yake. Yoyote yanayokuwemo kwenye kazi wanayoenda kuifanya, yawe mazuri au mabaya, wa kuwajibika ni rais mwenyewe.
Kazi hiyo ya Tume ya Warioba ikafanyika kiungwana, kiumakini na kitaalamu mpaka ikakamilika. Ikaletwa na kukabidhiwa kwa Rais Kikwete. Rais akaipitia na kuridhika nayo. Tarehe 22 / 1 / 2014, akaitia mkono, sahihi, ili iwe Rasimu, akaunda Bunge Maalumu la Katiba ili Rasimu hiyo ikawasilishwe kwenye Bunge hilo kusudi likaichambue na kutengeneza Katiba mpya kabla ya Katiba hiyo kuletwa kwa wananchi wakaipigie kura ya kuikataa au kuikubali.
Kwa ufupi ni kwamba JK asingekubali kuisaini Ripoti ya Warioba iwe Rasimu kama asingekubaliana nayo au kuyaona mapungufu makubwa ndani yake. Ni lazima angemueleza Warioba ayarekebishe mapungufu kwanza, au kwa mamlaka yake, kuivunja Tume hiyo na kuunda nyingine. Izingatiwe kwamba ile ni Tume yake Rais iliyokuwa ikifanya kazi kwa niaba yake.
Kwa maana hiyo siamini kabisa kwamba hotuba aliyoitoa JK Bungeni, iliyopaswa kuwa ya uzinduzi wa Bunge Maalumu la Katiba, lakini ikageuka kuwa ya kuichambua Rasimu, ilitokana na dhamira ya kweli ya rais. Dukuduku langu hilo linatokana na mlolongo mzima nilioueleza hapo juu kuhusiana na mchakato huu wa kuipata Katiba mpya.
Baada ya hapo wajumbe wa Bunge Maalumu wa upande wa CCM wakaanza kuonyesha wasiwasi wao kuhusu Rasimu hiyo kabla ya hata kuanza kuichambua! Ikaonekana Rasimu hiyo haionyeshi mustakabali mwema kwa chama chao!
Hivyo wakaanza kuandaa mikakati ya kuishughulikia Rasimu hiyo huku wakionekana kumshambulia waziwazi Jaji Warioba kwamba ni kama ameileta makusudi Rasimu hiyo kama mbinu ya kukiangamiza chama chao!
Wanaosema hivyo hawayatilii kabisa maanani mambo kama haya; kwamba baadhi yao hawaijui CCM wala kuipenda kufikia hata robo ya Jaji Warioba, kwamba alichokiwasilisha Warioba sio mawazo yake bali ya wananchi  kama alivyoelekezwa na rais, kwamba anachokitaka Warioba ni kuiona CCM iliyokomaa na kuacha kutegemea kubebwa na nguvu za dola na badala yake chama hicho kijitegemee chenyewe kama vinavyofanya vyama vingine.
Mwisho kabisa Warioba anaupenda Muungano, ni kwa vile anauelewa kuliko wajumbe wengi wa CCM wanaomshambulia kiushabiki wakiwa wameyaweka mbele maslahi yao binafsi ndani ya muungano huo wakikitegemea chama chao kuyapata wanayoyataka,  wakiwa wameyatelekeza maslahi ya nchi hasa ya Muungano.
Tatizo ambalo hata mimi naliona kwa hapa ni la baadhi ya wananchi kuupenda Muungano kwa vile unalinda maslahi yao binafsi bila ya kujali ni namna gani Muungano huo unalinda maslahi yake wenyewe.
Ikumbukwe Muungano ndio unaozaa jina la Tanzania, kwa maana hiyo ukishaondoa neno Zanzibar unachobaki nacho sio Tanzania Bara kama ilivyozoeleka kwa sasa, bali kinachobaki ni Tanganyika. Sababu neno TanZania ni muunganisho wa majina mawili ya Tanganyika na Zanzibar.
Haiwezekani ukaicha Zanzibar ikajitambua kwa rais wake,  Katiba yake, bendera yake, Wimbo wake wa Taifa, Bunge lake, Baraza lake la mawaziri nakadhalika, halafu Muungano wenyewe ukabaki imara, ni lazima utayumba na baadaye kutoweka.
Hicho ndicho alichokisisitiza Jaji Warioba, kwamba ili Muungano usiyumbe hapanabudi ukaitambua pia Tanganyika katika kujiwekea uwiano wake. Vinginevyo ukiendelea kuelemea upande mmoja matokeo yake utapinduka na kuzama kama MV Bukoba. Na katika kuzama hakuna heri yoyote.
Hizo ni kero zilizomo kwenye Muungano alizoziona Rais Kikwete na kusema jinsi zinavyomsumbua kichwa chake, hivyo akaahidi kuzishughulikia.
Kwahiyo wajumbe wanaodhani wanamshambulia Warioba waelewe wazi kuwa wanamshambulia na kumkana JK. Sababu kazi ya Warioba haikutokana na dhamira yake mwenyewe, hiyo ni kazi iliyokuwa kwenye dhamira ya Rais Kikwete, Warioba ni msaidizi tu.
Muungano wa Tanzania unapaswa usimame kwenye umakini huku zikijengwa hoja murua za kuulinda, hauwezi kulindwa na viroja.
Viroja ni kama hivi;  wapo wanaosema kwamba muungano wa miaka 50 utavunjikaje leo? Huku wengine wakisema kwamba asilimia kubwa ya Watanzania wa leo wamezaliwa baada ya Muungano kwahiyo eti hawaijui Tanganyika!
Kusema ukweli hapo sioni hoja yoyote ya kuulinda Muungano zaidi ya kuuchimbia kaburi.
Scotland na Uingereza ziliungana mwaka 1707, zaidi ya miaka 300 iliyopita, lakini leo hii nchi hizo zinaongelea kutengana kiustaarabu. Mbona umri wa muungano wa nchi hizo haujawa kikwazo kwa mazungumzo hayo ya kutengana? Ila umri wa muungano wetu, ambao ni zaidi ya mara 6 ya muungano wa Scotland na Uingereza, ndio uonekane mhimili wa kuulinda muungano wetu!
Kitu kingine ni kwamba Mwalimu Nyerere kazaliwa enzi za wakoloni, hakuwahi kusoma wala kufundishwa kokote juu ya nchi iliyoitwa Tanganyika huru na baadaye ikatawaliwa na wakoloni, lakini mbona hiyo haikumzuia kuongoza harakati za kuudai uhuru wa Tanganyika?
Sasa iweje wananchi wa Tanzania waliozaliwa baada ya Muungano wakasoma historia ya Muungano huo na Tanganyika iliyokuwa huru, wakose kuielewa Tanganyika? Na watashindwaje kuyahoji mambo ambayo wanaoona hayakwenda sawa wakati wa kuziunganisha hizi nchi mbili?
Mwisho ni kwamba kuna hadithi ya Waingereza inayosema juu ya mtu anayeliwa na dubu, eti mtu akiliwa na dubu na huyo mnyama akaendelea kuishi mzuka wa marehemu aliyeliwa utabaki ukiwasumbua jamaa zake mpaka dubu huyo atakapokufa.
Ndivyo ilivyo kwa mzuka wa Tanganyika. Mzuka huo unasababishwa na uwepo wa Zanzibar. Mzuka huo hauwezi kupotea hata baada ya miaka milioni moja kama Zanzibar inaendelea kujitambua.
Tukiangalia miaka ya 1960 mwishoni mpaka mwanzoni mwa miaka ya 1970, tutaona kwamba mzuka wa Tanganyika ulikuwa umetulia pamoja na kwamba ulikuwa muda mfupi tangu nchi hizi ziungane, sababu ni kwamba kilichokuwa kikitumika sana ni Tanzania Visiwani na Tanzania Bara. Neno Zanzibar lilibaki kutumika kama jina la mji tu basi.
Kwahiyo inapoandikwa Katiba mpya mambo hayo hayanabudi kuwekwa maanani, kama kweli wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wamekidhamiria wanachokifanya. Kumsuta Jaji Warioba hakufai, sababu wanaofanya hivyo watajikuta wanajisuta wenyewe au wakimsuta wanayedhani wanamfurahisha.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau