Bukobawadau

FEDHA ZA IPTL KAA LA MOTO

Dodoma. Tuhuma za ufisadi wa zaidi ya Sh200 bilioni katika akaunti ya Escrow ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zinaonekana kuwa kaa la moto na jana zilitikisa Bunge na kuibua mvutano mkali.
Hata hivyo, suala hilo sasa limekabidhiwa kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) ili kubaini ukweli wake.
Tuhuma hizo ziliibuliwa juzi na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ambaye alisema kashfa hiyo ni zaidi ya ile ya Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) ya BoT iliyotokea mwaka 2005.
Kafulila alisema ufisadi huo unamhusisha Waziri wa Nishati na Madini, Waziri wa Fedha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gavana wa BoT na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme (Tanesco).
Ingawa Kafulila hakutaja kwa majina, Waziri wa Nishati ni Profesa Sospeter Muhongo, wa Fedha ni Saada Mkuya, Katibu Mkuu wa wizara hiyo (Nishati) ni Eliakim Maswi na AG ni Frederick Werema.
Hata hivyo, akihitimisha hotuba ya bajeti yake na kujibu hoja mbalimbali za wabunge, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alimwagiza CAG na Takukuru kuchunguza tuhuma hizo ili kubaini ukweli.
“Hoja iliyopo na inayoleta ubishani ni kuondoa pesa kutoka akaunti ya Escrow na kuzipeleka IPTL. Tunajiuliza kama ni ufisadi, ni ufisadi wa nini wakati fedha zile ni za IPTL?” alihoji Pinda.
Pinda alifafanua suala hilo lilipoandikwa kwa kirefu na gazeti dada la Mwananchi (The Citizen), CAG aliwasiliana na Katibu Mkuu wa Nishati, Gavana wa BoT na Mkurugenzi wa Tanesco ili kupata picha ya mchakato mzima.
“Wakati akiendelea hivyo, CAG akapata barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa Nishati akimwomba afanye uchunguzi wa kina na wakati huo huo kamati ya PAC nayo ikamwelekeza kuchunguza jambo hilo.”
Waziri Mkuu aliongeza kusema: “Kwa tuhuma zenyewe zilivyo, itabidi tuwahusishe Takukuru nao wafanye kazi kwa upande wao ili kupata ukweli.
“Kwa maelezo na mtiririko ulivyo, kinachobaki ni tuhuma zinazojitokeza ambazo upo uwezo mkubwa wa vyombo hivi kuweza kuzibaini. Naliomba Bunge lako likubali CAG akubali kukamilisha kazi hiyo.”
Waziri Mkuu alisema wako viongozi wa Serikali ambao wametuhumiwa katika suala hilo hivyo ni vyema likachunguzwa kwa uzito wake ili wale watakaobainika wamekula rushwa washtakiwe.
Katika ufafanuzi wake huo, Pinda alisema katika mabishano hayo yako maswali ambayo anafikiri ni ya msingi kuhojiwa ikiwamo kama IPTL ililipa kodi stahili zinazohusiana na pesa hizo.
Pinda alisema kisheria, fedha zile zilipokuwa zinakwenda Escrow, akaunti zilipaswa kukatwa  kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), na wabunge wanaweza kuhoji kuanzia hapo.
Hali kadhalika, Waziri mkuu alisema wabunge wanaweza pia kuhoji kama wakati IPTL inauzwa kwa mwekezaji mpya kampuni ya PAP kama ililipa kodi kama sheria za nchi zinavyotaka.
Waziri mkuu alisema hata uamuzi wa mahakama ya kimataifa ya usuluhishi, ilielekeza fedha hizo zipelekwe IPTL kwa vile ni zao na zilitunzwa tu katika akaunti hiyo katika kipindi cha mgogoro.
Spika wa Bunge, Anne Makinda alitangaza kuwa PAC imekwishamwandikia barua ikimtaka akubali CAG achunguze suala hilo na yeye amekubali, na taarifa yake itapelekwa bungeni kupitia PAC.
Hata hivyo, kulitokea mzozo kati ya Spika na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika baada ya Mnyika kumtuhumu Spika kuwa anafanya kazi ya Serikali badala ya kumwacha Waziri mkuu atoe majibu.
Mnyika alikuwa akishikilia msimamo wa kuundwa kwa kamati teule akisema uko uzoefu wa miaka ya nyuma ambapo CAG alitumika kuisafisha kampuni ya Richmond katika kashfa ya kufua umeme.
Mbunge huyo alisema suala la kuamua kama iundwe kamati teule ya Bunge ama la inatakiwa kufanywa na Bunge na siyo Spika hivyo kwa mtazamo huo, Spika anafanya kazi ya Serikali.
Hata hivyo, Spika alimtaka  Mnyika akae chini kwa sababu tayari suala hilo litashughulikiwa na CAG na haiwezekani mambo mawili kwenda kwa wakati mmoja kwani huko ni kupoteza muda.
Mnyika alijaribu bila mafanikio kumweleza Spika kuwa anataka kuondoa shilingi kwenye Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu inayofikia Sh5 trilioni kwa mwaka 2014/2015 lakini aligonga mwamba.
Kwa upande wake, Werema alisema suala la akaunti ya Escrow, Watanzania wanayo haki ya kujua kama kodi mbalimbali zilizotakiwa kulipwa kisheria, kama zililipwa na IPTL na washirika wake.
“Ni vizuri tuelewe, unapomtaka Waziri mkuu auende kamati teule hiyo siyo kazi yake…, kama kuna ufisadi lazima ujulikane lakini vitu vyote viko wazi,” alisisitiza Werema.
Kabla ya Waziri mkuu kutoa ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Uchumi, Viwanda na Biashara, Luhaga Mpina aliomba mwongozo wa Spika akisisitiza Kafulila alisema uongo.
Mpina alisema maelezo ya Kafulila kuwa Gavana wa BoT alipobanwa na kamati yake alikiri kutoa fedha hizo kwa shinikizo, yalikuwa siyo ya kweli na wala hayakutamkwa na Gavana mbele ya kamati.
“Maelezo ya Gavana wa BoT ninayo, haiwezekani watendaji wa Serikali wanafika mbele ya kamati halafu wanakuja kuzushiwa maneno ambayo hawakuyasema.
“Mimi jana baada ya tukio hili kutokea, niliwaita wajumbe wangu kwa sababu suala hili liliwasilishwa kwa mfumo wa semina, hatukuwa na hansard,  tuliwauliza wote wakasema halikusemwa.
Hata hivyo, alisema kwa vile suala hilo lina harufu ya rushwa ni vyema CAG akashirikiana na Takukuru kuchunguza kwa vile taasisi hiyo inayo mamlaka kisheria kuzifikia kampuni binafsi.
Baada ya maelezo hayo, Kafulila alisimama na kuomba mwongozo wa Spika akisema jambo hilo ni kubwa na  limekuwapo tangu mwaka 2005 mpaka leo na kutaka apewe nafasi ya kuthibitisha.
“Kwa sababu ya unyeti wa jambo lenyewe kuwagusa vigogo ambao ushahidi wa kila mmoja alivyohusika ninao, niruhusiwe ili nithibitishe kila mmoja alivyohusika kwenye ufisadi huu,” alisema.

“Mheshimiwa Spika, tuache mizunguko na porojo nyingine, twende kwenye uhalisia. Kuna kodi zimekwepwa, kuna ufisadi umefanyika, wananchi wanataka kujua ukweli wa jambo hili,” alisema.

CHANZO: MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau