Bukobawadau

SHIRIKA LA NELICO NA MABARAZA YA WATOTO WILAYA YA GEITA WAFANYA ZIARA YA KIMAFUNZO KATIKA SHIRIKA LA KIVULINI

Mkurugenzi wa Shirika la Kutetea Haki za Wanawake na Wasichana la KIVULINI akitoa historia ya shirika la KIVULINI kwa wawakilishi wa mabaraza ya watoto mara baada ya kutembelea ofisi za shirika hilo hapo jana. KIVULINI ni shirika lisolo la kiserikali linalofanya shughuli za kupinga na kutetea Haki za Wanawake na Wasichana katika mikoa yote ya kanda ya ziwa pamoja na mkoa wa Singida tangu mwaka 1999.
Afisa Utetezi na Mitandao ya Kijamii toka Shirika la KIVULINI Bi. Khadija Liganga akifafanua jinsi KIVULINI ilivyoweza kuliinua Shirika la Mtandao la Watoto la Jijini Mwanza (Mwanza Youth and Chidren Network) na kuweza kusimamia na kutetea Haki za Watoto katika jiji la Mwanza. 
Picha ya Pamoja ya Maafisa wa Shirika la KIVULINI, Mkurugenzi na Afisa Mradi wa NELICO, Afisa Maendeleo jamii wa wilaya ya Geita, Muwakilishi wa Plan International pamoja na Wawakilishi wa Mabaraza ya watoto wilayani Geita mara baada ya kumaliza ziara ya Kimafunzo katika ofisi za shirika la KIVULINI.

Shirika la watoto la New Light Children Center Organization (NELICO) la mkoani Geita kwa kushirikiana na Idara ya Maendeleo ya jamii Geita, limeambatana na wawakilishi 20 toka Mabaraza ya watoto ya kata kumi na moja (11) za wilaya ya Geita kwa ziara ya kimafunzo katika shirika la kutetea Haki za Wanawake na wasichana, KIVULINI la mkoani Mwanza.

Ziara hiyo ya kimafunzo katika shirika la KIVULINI imefanyika hapo jana ikiwa na lengo la kujifunza namna KIVULINI ilivyosaidia Baraza la watoto Mwanza kuweza kuratibu na kutekeleza shughuli zake kikamilifu na kuwa imara zaidi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Mkurugenzi wa NELICO Bi. Paulina Alex alisema kwamba ziara hiyo imelenga kutoa mafunzo kwa mabaraza ya watoto wilayani Geita juu ya mbinu za kuratibu na kutekeleza miradi mbalimbali lakini pia kujua mafanikio na changamoto za shirika la KIVULINI katika kupiga vita ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika mikoa ya kanda ya ziwa.

“Mabaraza ya watoto ya  Geita bado ni machanga sana na hivyo kufanya safari hii ya mafunzo kuwa ya muhimu sana. Katika safari hii wawakilishi wa mabaraza ya watoto wameweza kupata elimu kubwa kutoka KIVULINI na Baraza la watoto la Mwanza (Mwanza Youth and Children Network) ambalo ni zao la KIVULINI” alisema Bi. Paulina.

Ziara hiyo pia ilikuwa na Bw. Maximillian Kitigwa amabe ni mwakilishi toka shirika la Plan International ambao ni wadau wakubwa wa watoto kwa mkoa wa Geita pamoja na Afisa Maendeleo ya jamii wa wilaya ya Geita Bi. Emma Busanji. Watoto hao pia watafanya ziara katika Mkoa wa Arusha kujionea juhudi za  wadau wa maendeleo katika mkoa huo katika kuwaokoa watoto dhidi ya kufanyishwa kazi hatarishi hasa katika sekta ya madini.

Kivulini ni shirika lisilo la kiserikali la kutetea na kulinda Haki za Wanawake na Wasichana. Shirika la Kivulini linahamasisha jamii (Wanawake, Wanaume na Vijana) kulinda, kutetea Haki za Wanawake na Wasichana kwa kupinga vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia. Makao makuu ya shirika yapo jijini Mwanza, Wilaya ya Ilemela, Tanzania.


Next Post Previous Post
Bukobawadau