Bukobawadau

ZITTO KABWE;NABII ASIYEKUBALIKA NYUMBANI?

Ezekiel Kamwaga
JANA, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Kamati za Bunge za Hesabu Barani Afrika (AFROPAC) katika mkutano uliofanyika jijini Lusaka, Zambia.

Huu ni umoja mchanga kabisa ambao ndiyo uko katika mwaka wake wa kwanza. Kimsingi, uteuzi huu wa Zitto unamaanisha kwamba yeye ndiye atakuwa msimamizi mkuu wa shughuli za kila siku za umoja huu mpya.
Atakuwa kiongozi wa Sekretarieti ya AFROPAC na hivyo atakuwa anasimamia waajiriwa wote wa umoja huo kwa sasa. Hii maana yake ni kwamba Watanzania watapata nafasi zaidi za kuajiriwa.

Ndiyo maana, nafasi hii ilikuwa ikiwaniwa na wabunge wengi kutoka katika mabunge mengine barani Afrika. Kwenye umoja kama AFROPAC, nafasi ya Mkuu wa Sekretarieti huwa na faida kwa wananchi wa nchi anayotoka Katibu Mkuu.

Huu si uteuzi wa kwanza wa Zitto ambao unaonyesha heshima anayopewa nje ya nchi. Ni Zitto huyuhuyu ambaye miaka michache iliyopita aliteuliwa na aliyekuwa Rais wa Ujerumani, Horst Kohler, kuwa mmoja wa viongozi vijana wanaochipukia barani Afrika chini ya mpango uliofahamika kwa jina la Africa Initiative.
Katika bara zima la Afrika, serikali ya Ujerumani iliteua vijana takribani 40 tu ambao walionekana kuwa tumaini la bara hili katika miaka ijayo.

Katika kitabu cha Global Corruption, Mwanzilishi wa Taasisi ya Kimataifa ya Masuala ya Rushwa ya Transparency International (TI), Laurence Cockcroft, alimueleza Zitto kama kiongozi “makini, mwenye uelewa mpana na mpambanaji wa rushwa.”

Ni Zitto ambaye amechochea vijana wengi kujiunga na siasa katika miaka ya karibuni. Miaka kumi iliyopita, Bunge lilikuwa ni taasisi ya wastaafu na wateule wachache waliodumu kwa miaka mingi.

Ni Zitto ambaye uwepo wake na ujengaji wake wa hoja ulifichua nguvu na upya ambao taasisi hiyo ilikuwa inatakiwa kuwa nao. Kama utaongea na wabunge vijana walioingia bungeni katika Uchaguz uliopita, nusu watakwambia kwamba Mbunge huyu wa Kigoma Kaskazini ndiye aliyewashawishi kufuata njia hiyo ya uanasiasa.
Mwanasiasa huyu ni mtoto wa familia isiyo ya kitajiri wala yenye historia yoyote na Tanzania. Ni Zitto Kabwe ndiye aliyewaonyesha watu kwamba unaweza kuwa mtoto wa masikini na usiye na uhusiano wowote wa damu au uswahiba na familia tajiri na bado ukawa na fursa.

Na tangu ameingia bungeni, Mbunge huyu amekuwa nyuma ya karibu matukio yote makubwa ambayo yametokea bungeni katika miaka ya karibuni.

Yeye ndiye aliyeibua suala la Buzwagi ambalo leo limetupa Sheria Mpya ya Madini ambayo walau ina manufaa kwa wananchi kuliko sheria iliyokuwepo kabla hajaingia bungeni.

Zitto Kabwe ndiye aliyependekeza kwa serikali Waziri Sospeter Muhongo Mabadiliko ya Sheria katika Nishati ya Gesi ambayo leo yataiingizia serikali mabilioni ya fedha kila makampuni ya gesi yatakapokuwa yanauziana hisa yenyewe kwa yenyewe.

Kabla Zitto hajaingia bungeni, makampuni haya yalikuwa yakibadilisha majina au kuuziana hisa pasipo Tanzania kufaidika na lolote. Nchi hii imepoteza mabilioni ya shilingi kwa mtindo huu.

Leo hii, Mbunge huyu anafuatilia Ufisadi katika Ulipaji wa Kodi unaofanywa na Makampuni Makubwa si Tanzania pekee bali barani Afrika kwa ujumla.

Makampuni haya yanakwepa kulipa kodi au kulipa kodi kidogo kwa serikali kwa kutumia njia ambazo zilikuwa hazijabainika huko nyuma. Kama serikali itaanza kukusanya kodi yake stahili na kuzuia ukwepaji huo wa kodi, Zitto atakuwa amesaidia katika hilo.

Kodi hii ndiyo ambayo itasaidia kununua dawa katika hospitali zetu, madawati katika shule zetu, kuzuia vifo vya akinamama wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano na kujenga barabara na miundombinu mingine.

Mara zote, Zitto amefanya haya pasipo kutukana wala kugombana na watu. Siku zote amekuwa ni mtu wa kujenga hoja na amekuwa na marafiki karibu katika vyama vyote ambavyo viko hapa nchini.

Ni vigumu, vigumu sana kumlinganisha Zitto na Mbunge yeyote kijana katika Bunge la sasa… Binafsi, naamini kwamba huyu ndiye Mbunge wa muhimu zaidi kuliko wabunge wengine wote waliopo katika Bunge la Tanzania.

Na hii ni kwa sababu ya rekodi zake nilizotaja hapo juu. Badala ya kubishana kuhusu umuhimu wake, ni vema watu wakakumbushana na kueleza ni mbunge yupi amekuwa na mchango mkubwa bungeni kuliko huyu wa CHADEMA.

Kuna wabunge ambao wanazungumza mara kwa mara bungeni lakini baada ya siku tatu hakuna watu wanachokumbuka kuhusu hoja zao. Kuna wabunge ambao watakumbukwa zaidi kwa kupigwa na askari, kutoka nje ya Bunge, kutukana watu kwenye mitandao ya kijamii na kutoa maneno ya kashfa bungeni.

Kuna wabunge ambao watakumbukwa pia kwa kuwa mstari wa mbele kumkashifu na kumponda Zitto Kabwe. Tatizo ni kwamba, hakuna mwanasiasa atakayefanikiwa kwa siasa za namna hii ambazo hazisaidii Taifa.

MTU WA KITAIFA NA KIMATAIFA

Hakuna mwanasiasa wa upinzani hapa Tanzania ambaye ana uhusiano mzuri kimataifa na pia ana heshima miongoni mwa taasisi za dola pamoja na waasisi wa Taifa kuliko Zitto.

Kuna mwanasiasa gani hapa nchini ambaye ana uhusiano wa karibu na Waziri Mkuu wa zamani wa Malaysia, Dk. Mahathir Mohamed, kuliko Zitto?

Mahathir ni mwanasiasa muhimu kwa vile ndiye aliyeibadilisha nchi yake kutoka kuwa masikini na kuwa na uchumi wa kati. Zitto alimtafuta huyu kwa vile anatafuta namna ya kuikwamua Tanzania kutoka hapa ilipo sasa.

Zitto ni rafiki wa Raila Odinga. Zitto ni rafiki wa familia ya Mwanamapinduzi wa Msumbiji, Hayati Eduardo Chivambo Mondlane. Zitto ni mtu wa karibu na familia ya Mzee Keneth Kaunda kiasi kwamba majuzi alikwenda kumtembelea nyumbani kwake wakati Rais huyo wa zamani wa Zambia alipokuwa akiugua.

Inawezekanaje kwa mwanasiasa wa kawaida na mbinafsi (kama ambavyo Watanzania wanaaminishwa na baadhi ya wanasiasa), awe na ushawishi wa namna hii ambao hakuna mwingine wa umri wake anao?

Kama kijana, nafikiri ni muhimu kwa vijana wenzangu kuanza kumtazama Zitto kama mmoja wa wanasiasa muhimu katika kizazi chetu.

Ni rahisi sana kuingia katika mkumbo wa kusikiliza propaganda za watu ambao kwa sababu zao binafsi hawataki kukubaliana na ukweli huu au wameamua kupambana na ukweli huu kwa gharama yoyote.

Kama Afrika nzima inaona kwamba Zitto anafaa kuwa kiongozi mwandamizi wa taasisi inayoshikilia kupambana na ufisadi katika matumizi ya fedha za umma, iweje leo aonekane mbaya na mbovu kabisa hapa kwetu?

Anachohitaji Zitto Zuberi Kabwe (ZZK) ni kitu kimoja; Heshima.
Mimi nitakuwa mtu wa kwanza kukubali kwamba katika safari yake ya kisiasa, ZZK amefanya makosa mengi humo njiani.

Lakini, binadamu wanahitaji kuongozwa na mmoja wao. Anayekosea kama wao, anayeumia kama wao, anayecheka kama wao na anayejua mahitaji na matakwa yao.
Mimi ni Mkristo na katika kitabu cha Samweli nakumbuka Wana wa Israel walimwambia Mungu kwamba wamechoka kuongozwa na Mitume na wanataka kuongozwa na mmoja wao.

Hapo ndipo Mwenyezi Mungu alipomteua Sauli….na baadaye Daudi na kasha Suleiman. Na wote walifanya makosa yao katika uongozi wao.

Zitto Kabwe alikosea na atazidi kukosea katika miaka inayokuja. Si kwa sababu anataka lakini kwa sababu ni mwanadamu kama sisi na sote tu wakosaji.

Lakini, kwangu atazidi kuwa mwanasiasa wa kipekee katika kizazi chetu. Nitachukia kama mwisho wake utakuwa sawa na kisa cha Nabii asiyekubalika kwao.
Zitto Kabwe ni wetu. Tumsaidie kwa vile kwa kizazi chetu cha vijana wa sasa, yeye ni maalumu…. Wa kipekee, Zitto.

Zitto Kabwe. Zahoro Muhaji Vicent Kassala Joseph Peter Joseph Peter Kibatala Lutengano Mwalwiba Zitto Z Kabwe
Next Post Previous Post
Bukobawadau