Bukobawadau

CCM NA KERO ZA WANANCHI

Miaka 60 CCM ndipo inakumbuka kero za wananchi!
Na Prudence Karugendo
MTU  mmoja nisiyeelewa yuko upande gani kiitikadi, kama anafuata itikadi za upinzani au za chama tawala, kanipa wazo la kufikirisha kama mojawapo ya changamoto za kisiasa.
Kanitumia ujumbe mfupi wa maandishi kwenye simu yangu akisema hivi, “Kinana wa CCM anazunguka nchi nzima akisikiliza kero za wananchi, Slaa wa Chadema anazunguka nchi nzima anahubiri serikali tatu. Je, ni yupi tumuombee dua ya mafanikio?”
Katika kutafakari kwangu nagundua jambo la kushangaza. Kinachonishangaza ni namna baadhi ya watu wanavyovilinganisha hivi vyama viwili, CCM na Chadema. Maana kuvilinganisha hivi vyama ni sawa ni na kulinganisha mzee wa miaka 80 na kijana wa miaka 20.
Ni lazima kutakuwepo na tofauti kubwa inayoletwa na kupishana sana kwa umri wa watu hao wawili, mzee na kijana. Mzee ni lazima atakuwa ameyaona mengi, amefanya mengi au kushindwa mengi kuliko kijana anayelinganishwa naye.
Kwahiyo mzee kukubali kulinganishwa na kijana, hata kama hakutamka, ni lazima atakuwa amekubali kushindwa.
Tukiviangalia vyama vya CCM na Chadema tutaziona tofauti za wazi zinazotokana na kupishana sana kwa umri wa vyama hivyo. Ni sawa na tofauti zilizokuwepo kati ya chama cha TANU, kilichokuwa kinapigania uhuru na wakoloni waliokuwa wanatutawala.
Wakati TANU ikionyesha athari za kutawaliwa wakoloni walikuwa wakidai kwamba chama hicho hakijawafanyia lolote wananchi!
Sasa wakati CCM inachezea kwenye umri wa miaka 60 Chadema ndio kwanza inachezea kwenye umri wa miaka 20. Ni tofauti kubwa sana ambayo kwa mtu mwenye aibu ni vigumu kutamani kulinganishwa na mtu aliyemzidi kwa kiwango hicho.
Kwa mantiki hiyo, anayekubali kulinganishwa na mtu aliyemtangulia umri kwa kiasi kikubwa namna hiyo atakuwa anakiri kushindwa kuitumia vizuri tofauti hiyo ya umri kukifanya kile alichopaswa kuwa amekifanya.
Sababu mbali na uzoefu unaotokana na umri mkubwa ilio nao CCM, chama hicho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne, lakini Chadema ndio kwanza inataka ipewe ridhaa ya kuonyesha namna ya kuongoza.
Mbali na CCM kuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne, chama hicho kimeendesha udikteta wa kutawala kimabavu, bila kutaka kuuona upinzani wowote kwa zaidi ya robo karne!
Lakini kwa wakati huu chama hicho tawala kinajinadi kwa wananchi kikitaka kilinganishwe na Chadema huku kikihoji Chadema imewafanyia nini wananchi kana kwamba kuna wakati kiliwahi kuona Chadema inatawala kama chenyewe kilivo!
CCM kinajinadi kama chama kipya huku wakati mwingine kikilia na kupiga mayowe kuwa kinaonewa na Chadema,  kikitaka kupata huruma ya wananchi kama vile chenyewe na Chadema viko sawa kiumri na kiuwezo!
Chama tawala kinasahau kuwa uzembe wake ndio umevizaa vyama vya upinzani kikiwemo Chadema. Maana bila uzembe huo sidhani kama kungekuwepo na mwananchi yeyote ambaye angekuwa anaufikiria upinzani kwa vile kila jambo lingekuwa katika mstari wake.
Wakati huu ambapo chama kichanga,  Chadema, kinajaribu kufanya kazi ya kuwafumbua wananchi macho ili wauone, wauelewe, wautambue na kuuthamini muundo wa taifa lao, kazi kama iliyofanywa na TANU enzi za wakoloni, CCM eti ndio kwanza inajaribu kusikiliza na kuzielewa kero za wananchi! Tuseme muda wote huo wa zaidi ya nusu karne haikujuwa kama wananchi walikuwa na kero! Hicho ndicho chama tawala!
Ni yaleyale yaliyokuwa yakifanywa na wakoloni katika kuzikata makali harakati za TANU za kuwafumbua macho wananchi ili waione, kuitambua na pia kuidai nchi yao toka kwenye makucha ya wakoloni.
Hivi kama kweli CCM ingekuwa nao uwezo wa kuzisikiliza kero za wananchi ingekuwa inazitafuta hivi sasa baada ya miaka 60 ya uwepo wake? Kipindi hicho kisingetosha kuifanya ikawa inazielewa kero za wananchi kama mtu anavyolielewa jina lake? Kinana angelazimika kuzunguka nchi nzima akifanya kazi hii anayoifanya kwa sasa?
Tunachoweza kusema ni kwamba CCM haikutaka kutatua kero hizo na sasa imejikuta imekwama, haiwezi tena kuzitatua kero hizo. Kwahiyo inachokifanya ni kujaribu kukwamisha juhudi za Chadema na vyama vingine vya upinzani za kuwafumbua wananchi macho.
Inachokifanya Chadema kwa kushirikiana na vyama vingine vya upinzani kwa sasa ni kuwafanya wananchi wautambue kwanza muundo wa taifa lao, hiyo ndiyo kero namba moja.
Bila kuitambua kero hiyo,  tiba ya kero zilizobaki haiwezi kupatikana kamwe. Itapatikana tu dawa ya kutuliza maumivu ya kero wakati kero zenyewe zikibaki palepale kama CCM ilivyodumu nazo kwa miaka 60.
Sababu hiyo ni kero iliyodumu kwa zaidi ya miaka 50 sasa pamoja na kwamba kila kitu ambacho kingewafanya wananchi wayafurahie maisha yao ndani ya uhuru wao kimekuwepo muda wote kikiwa kimejaa tele.
Kwa ufupi ni kwamba kero zote zinazotajwa na wananchi zimetokana na kero hiyo kuu iliyosababishwa na CCM na kuendelea kulindwa na chama hicho kwa muda wote huu.
Nimejaribu kufuatilia kampeni za pande hizi mbili, CCM na upinzani, dhidi ya masaibu yanayowapata Watanzania kwa sasa na kugundua kitu fulani. Sijasikia hata mara moja wapinzani wakiacha hoja na kushambulia nafsi za watu kwa njia ya kuparamia kama wanavyofanya CCM.
Mfano,  maneno kama jitu, zee, nene, refu, fupi nakadhalika, ni maneno yanayotolewa pale mtu anapokuwa ameishiwa hoja. Sababu unene wa mtu, urefu au ufupi wake havina uhusiano wowote na matatizo yanayowapata wananchi.
Lakini mara zote ninazomsikiliza Katibu Mwenezi wa CCM, Nape Nnauye, nasikia anasema zee hili limezeeka vibaya, zee hili lina kono sijui limekaaje, sijui lile linaongeaje! Ilmradi tu ni maneno ya kashfa na matusi kwa kwenda mbele.
Sio kwamba wapinzani hawawezi kutukana, ila kinachoangaliwa ni kazi iliyopo mbele yao. Kwa nini wapoteze muda kutukana wakati wanacho cha kuwaeleza wananchi? Asiye na cha kueleza ndiye anayelazimika kujaza pengo kwa mitusi.
Mtu anayeonekana anaukashfu uzee tunawezaje kusema anaunufaisha upande anaoupendelea? Maana atakuwa anawakashfu kuanzia wazazi wake, viongozi wake na wapenzi wa chama chake waliomzidi umri,  kwa vile hakuna upande unaokosa watu wa aina hiyo.
Kwa tunaofuata hoja mara moja tunaelewa kwamba pale mtu anapopungukiwa hoja anaamua kupajazia kwa tusi. Lakini je, tusi linaweza likaziondoa kero zinazotajwa?
Kwa mtindo huo kweli tushawishike na kuamini kuwa CCM inatafuta kero za wananchi? Na kama kweli inazitafuta tukubali kwamba itazitatua?
Kero zilizoishinda kwa miaka 60 kweli itazitatua kwa mtindo uleule ambao umezifanya kero hizo zikarundikana mithiri ya Mlima Kilimanjaro?
Kwa nini tusiamini kwamba Chadema ndiyo inaweza ikazitatua kero hizo baada ya kupagundua zilikorundikana na kukielewa chanzo cha kuzifanya zikarundikana? Huyo ni mganga mpya aliyekuja na dawa mpya baada ya kulielewa tatizo.
Tuchukulie kwamba mtu anasumbuliwa na maradhi fulani kwa muda mrefu, mganga yule ambaye kashindwa kumsaidia kwa muda wote anakuja na dawa ileile iliyoshindikana kuleta nafuu akidai kuwa itasaidia, kusudi mgonjwa asiitamani dawa mpya inayoletwa na mganga mpya. Kukubaliana na mawazo ya mganga aliyeshindwa ni nini zaidi ya kujitakia donda ndugu?
Ieleweke kwamba huu sio wakati wa kuuziana mbuzi kwenye gunia, hii ni karne ya uwazi. Chama chenye umri wa miaka 60 hakiwezi kusema sasa hivi ndipo kinasikiliza kero za wananchi. Kwa umri kilo nao na kwa namna kilivyojijenga, ikiwa ni pamoja na kutumia mabavu kuviondoa vyama vingine ili kibaki peke yake na kuendesha nchi kiimla, kilipaswa kuwa kinazielewa kero za wananchi hata zile ambazo hazijajitokeza.
Kujifanya kinaulizia kero za wananchi kwa wakati huu ni kutaka kukwepa aibu na kutokubali kushindwa.
Vyama vya upinzani, au tuseme Chadema, kama mleta mada alivyotaka iwe, ndivyo tunavyoweza kuvifikiria katika utatuzi wa kero za wananchi zilizotamalaki kwa sasa. Sio chama ambacho kimeshindwa kwa miaka 60.
Kwa wakati huu CCM isingekuwa inajifanya kusikiliza kero, ingekuwa inatafuta wapi paboreshwe baada ya kero zote kuwa zimefutika. Imeshindwa. Kwahiyo hayo ya kero za wananchi iviachie vyama vya upinzani ili navyo vionyeshe ni kitu gani vinaweza kukifanya kuhusu kero hizi zilizorimbikizwa na CCM kwa zaidi ya miaka 50.
Nimalizie kwa kusema kwamba anachokifanya Kinana na timu yake ya kina Nape, ni sawa na muziki wa zilipendwa, kwa maana ya kwamba sio kitu kipya wanachokionyesha na kukifanya. Kwa watu wenye kutafakari hiki ni kitu kilichopitwa na wakati na sasa kimekwama, sababu kilianza kufanyika tangu mwaka 1957.
Jibu langu kwa swali mtoa mada ni kwamba, nadhani ni hekima na haki tukamuombea dua ya mafanikio Slaa.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau