Bukobawadau

SAKATA LA MGANGA ALIYEMNYONGA MWANAFUNZI HUKO MULEBA

Ndugu Mujingwa John pichani ambaye ni  Mtuhumiwa wa mauaji akiwa na vifaa vinavyodaiwa kutumika katika mauaji na kuchimba kaburi chini ya kitanda.
  Pichani Waombolezaji wakisimulia matukio ya mauaji yaliyowahi kufanyika kabla ya tukio hili la kifo cha mtoto Fausta Geofrey(8)
KIFO cha Fausta Geofrey(8) mwanafunzi wa darasa la kwanza aliyenyongwa na kukatwa baadhi ya viungo kimeibua siri ya matukio ya kutisha yaliyowahi kufanyika kimya kimya katika Kata ya Muhutwe Wilayani Muleba.  
Mtuhumiwa wa mauaji ni Mujingwa John (20) mganga wa jadi mwenyeji wa kijiji cha Matera Wilayani Magu Mkoani Mwanza, ambaye kabla ya mauaji hayo alikuwa amekaa katik kijiji cha Bisole kwa siku tano.
  Mama mzazi wa Marehemu Fausta,Bi Geraldina Geofrey
 Pichani kulia ni Baba mzazi wa Marehemu Fausta,Geofrey Raphael
Nyuso za waombolezaji katika msiba huu zinasoma maswali mengi yasiyo na majibu,huku wakirejea katika matukio mengi ya kabla yake katika Kata ya Muhutwe ambayo watoto na watu wazima wamenyongwa na kunyofolewa viungo.

Hata hivyo tukio la kunyongwa kwa mwanafunzi huyu wa shule ya msingi Kitunga,na kukatwa mkono wa kushoto na baadhi ya viungo na hatimaye mtuhumiwa kuchimba kaburi chini ya kitanda na kumzika limewatisha zaidi wakazi wa Kata hii.

Taarifa ya Jeshi la Polisi ilikuwa imejaa maneno yenye harufu ya damu.Kwamba mtuhumiwa aliwapeleka kwenye mafiga na kuwaonyesha mkono na viungo vilivyokuwa vimebanikwa ili kutengeneza dawa ya uganga.


Rejea kwa Fausta alivyokuwa anaomba msamaha kwa kosa asilojua mbele ya panga lenye makali.Kabla ya kukata roho alitoa kilio kwa uchungu.Kilio na machozi yake viliwakilisha sauti za maelfu ya watoto wanaokufa kwa mateso.

 SIRI ZA MGANGA Mtuhumiwa alikuwa na siku tano tangu akaribishwe katika kijiji cha Bisole kama raia mwema ingawa alikuwa ni mwenyeji wa siku nyingi katika vijiji jirani kabla hajafukuzwa baada ya kuonekana kama binadamu asiyesomeka.
Kabla ya hapo tayari alikuwa amefukuzwa katika Kata ya Kagoma.ambapo Said Mikidadi mkazi wa kijiji cha Nyakashenye anasema Mujingwa John pia alifukuzwa na uongozi wa Kijiji baada ya matukio mengi yenye utata.
 

 Pamoja na kuwa mganga huyo aliishi peke yake alipanga nyumba mbili katika vitongoji tofauti vya Nyaibanga na Mushonde na hakuna mwananchi au uongozi wa serikali za mitaa uliojishughulisha kufuatilia nyendo zake.
Mwanafunzi huyo aliuawa katika nyumba alimopanga katika kitongoji cha Nyaibanga na mwili wake kusafirishwa na kuzikwa chini ya kitanda kwenye nyumba iliyopo kitongoji cha Mushonde katika kiijiji kile kile cha Bisole.

Kwa mujibu wa maelezo ya wananchi mganga huyo alipofika katika kijiji cha Bisole alikuwa anatafuta nyumba ya kupanga ambayo haina sakafu ya saruji na ambayo haikuwa na mwingiliano wa watu wengine.

Mmiliki wa nyumba ulipofukuliwa mwili wa marehemu Anitha Amos anasema mtuhumiwa alimfuata akimuomba aishi katika nyumba yake kwa maelezo kuwa nyumba aliyokuwa akiishi katika kitongoji kingine inavuja.

Mwanamke huyo aliamua kumpa nyumba hiyo tena bila malipo kwa kuwa haikuwa na mtu huku mmiliki wa nyumba nyingine Geraldina akiwa hana taarifa kuwa mganga huyo pia amepanga nyumba katika kitongoji jirani.
‘’Alikuja kwa unyenyekevu akisema nyumba aliyokuwa anaishi katika kitongoji kingine inavuja kwa kuwa nyumba yangu haikuwa na mtu na mimi nimeolewa nilimruhusu aishi bila malipo akinitunzia migomba’’anasema Anitha Kwamba kwa muda wa siku chache mtuhumiwa alimpenda sana mwanae wa miaka miwili aitwaye Rebeka na kuwa hakujua ni wakati gani mpangaji wake alikuwa anatumia nyumba hiyo kwa kuwa ameolewa mbali na hapo.
Kifo cha Beatha James Agost 29,mwaka 2012 mwili wa Beatha James(12) katika Kijiji cha Nyakashenye aliyepotea Septemba 6,ulipatikana ukiwa umeharibika karibu na Kambi ya Jeshi la Wananchi(JWTZ)Kaboya wilayani Muleba.
Ni katika kijiji kile kile ambapo mtuhumiwa wa mauaji ya Fausta alifukuzwa na kukimbilia katika kijiji cha Bisole na Polisi hawakufanya utafiti zaidi wa mauaji hayo zaidi ya kushuhudia mwili kichakani na kuruhusu mazishi yafanyike.
Kwa mujibu wa mlezi wa Beatha aitwaye Eudosia Salvatory,mwili wa mtoto huyo ulikuwa umenyofolewa ulimi,macho ngozi na sehemu za siri na Mariagoreth Ishengoma mkazi wa kijiji hicho alisema alimuona mtoto huyo akienda kununua maziwa kijiji jirani.
Pamoja na tukio hilo lililogubikwa na utata Polisi Mkoani Kagera kupitia kwa Kamanda wa wakati huo Philip Kalangi walikanusha kwa nguvu zote madai ya mwili wa Beatha kupatikana ukiwa umechunwa ngozi na baadhi ya viungo kuondolewa.
Kamanda Kalangi alisema uchunguzi wa mwili wa Beatha ulibaini kuwa ngozi ilitoka baada ya maiti kukaa muda mrefu porini huku mlezi wa mtoto huyo akishangaa kutoonekana kwa ngozi huku miguu ikiwa haijaharibika.
Mfululizo wa mauaji ya kutisha katika Kata ya Muhutwe yanawafanya hata polisi wasileweke kwa wananchi walio wengi wa eneo hili,wakiwatuhumu kutoyapa uzito tofauti na nguvu kubwa inayotumika kuwadhibiti vibaka.
Hata katika kifo cha Fausta hawakueleweka baada ya kusafirisha mwili wa mtoto huyo na kuutelekeza katika hospital ya Kaigara.Familia iliwapigia magoti kuwa hawakuwa na pesa za kukodi gari.Kauli mbiu ya polisi jamii haikuwa na nafasi katika msiba wa Fausta!

 

MAUAJI ZAIDI KIJIJINI MUHUTWE  
Hofu ya mauaji ya kikatiri katika Kata ya Muhutwe bado imetanda,na hakuna mwenye majibu ya kifo cha Eligidius Alianderi aliyekutwa amenyongwa mwaka jana na ,sehemu ya ngozi yake kuondolewa na mwili wake kutelekezwa barabarani.  
Katika mazingira yake yale mwaka jana,Kamu Chakupewa alikutwa amenyongwa na mwili wake kutelekezwa karibu na barabara ambapo Adelitus Triphone ni miongoni mwa wananchi walioshuhudia matukio yote na kuwa miili ya marehemu ilijaa utata. Kwa Mujibu wa mkazi wa kijiji cha Nyakashenye ilipotelekezwa miili hiyo Said Mikidadi anasema watu hao walikufa kwa nyakati tofauti ingawa katika mazingira yanayofanana na hakuna hatua zaidi zilizochukuliwa.  
Kwamba miili hiyo ilitelekezwa katika barabara ya lami usiku ili iweze kugongwa na magari kwa lengo la kupoteza ushahidi na tangu wakati huo hakuna mwananchi mwenye uhakika na maisha yake kwa kuwa hata walioaminika kuwa na marehemu hao mara ya mwisho hawakuwahi kuhojiwa Polisi.
Mwananchi huyo anasema viongozi wanachangia ukubwa wa tatizo hilo,kwa kuwa baada ya kukithiri kwa mauaji ya kutisha wananchi walifanya mkutano na kupiga kura za siri na matokeo yake hayakutumiwa na chombo chochote kuwabaini watuhumiwa.
Anasema kuwa hofu ya mauaji iliyogubika Kata hiyo imesababisha wazazi wasiwatume mbali watoto wao na hata wanapokwenda shuleni hawana uhakika na maisha ya watoto wao huku hatua ya kuendelea kufumbia macho matukio haya itasababisha wananchi kujichukulia sheria mkononi.
Pia hatua ya Polisi kupuuzia matukio haya ilisababisha wananchi mwaka jana katika Kata hiyo kumuua mtuhumiwa aliyekuwa na mwanafunzi wa shule ya Sekondari Zakia Rashid(16)vichakani ambaye kwa mujibu wa maelezo ya wananchi alikuwa ameishapoteza fahamu.
 
Mazingira hayo yalihusishwa na ushirikina pia mtuhumiwa hakuwa na undugu na mwanafunzi huyo ambapo kutokana na kukithiri kwa mauaji ya kutisha hata baada ya mtuhumiwa kuokolewa na polisi wananchi walivunja mahabusu ya Muhutwe na kumuua.  

VITUKO ZAIDI VYA MGANGA
Taarifa za kupotea kwa Fausta Geofrey ziliamsha hasira za matukio mengi ya mauaji katika Kata ya Muhutwe na wananchi walipiga ngoma na kukusanyika na kufikia uamuzi wa kumsaka mtoto huyo baada ya hata uongozi wa shule ye msingi Kitunga kudai kuwa hakufika nyumbani. Ni katika kipindi hiki cha utata alipoibuka Mujingwa John na tunguli zake akisema ana uwezo wa kutoa msaada wa kumtafuta mtoto huyo na kuwa alikuwa hai kwa kuwa alichukuliwa na mwanamke mmoja kwenda kufanya kazi.  
Kwa mujibu wa baba wa mtoto huyo Geofrey Raphael,baada ya shinikizo la wananchi lililomtisha mtuhumiwa aliwapeleka katika nyumba zote alizopanga na katika moja ya nyumba hizo alifungua mlango,akasogeza godoro na kuonyesha alipozikwa mtoto huyo.  

Katika maelezo aliyotoa Polisi mtuhumiwa alisema alimnyonga na kukata viungo vyake ili kutengeneza dawa ya uganga kwa ajili ya kujipatia utajiri na kuwa hilo lilikuwa tukio lake la kwanza kumwaga. Damu
CREDIT:Phinias Bashaya.





Next Post Previous Post
Bukobawadau