Bukobawadau

UGUMU WA MAISHA NA YATIMA

 MWISHONI mwa mwaka 1983, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alilihutubia Taifa wakati anapokea maandamano ya wakazi wa jiji la Dar es salaam yaliyokuwa mahususi kuunga mkono operesheni maalumu ya kupambana na watu waliojulikana kama wahujumu uchumi. Katika hotuba yake hiyo Mwalimu alisema kwamba kulikuwa kumeanza kujitokeza kundi au tabaka la watu ambao walikuwa wameota pembe na kuanza kujiona kama vile wana serikali yao, kwa hiyo akatumia nafasi hiyo kuwataarifu watu hao kuwa kuanzia wakati huo watambue kuwa serikali yao imepinduliwa rasmi na serikali ya Tanzania.
 
Kwa asilimia kubwa watu waliokuwa wamelengwa na mapinduzi hayo yaliyoendeshwa kwa mtindo wa vita na kupewa jina la vita dhidi ya wahujumu uchumi, ni wafanyabiashara. Vita ile iliwafunda wafanya biashara, wakajirudi wakitambua kuwa kuna mamlaka juu yao ambayo kwake iliwabidi wao kuwajibika.
 
Siri ya mafanikio ya vita ile ni kwamba kwa wakati ule ulikuwepo mgawanyo unaoheshimika katika makundi yaliyokuwa yanatengeneza jamii yetu. Jamii yetu ilikuwa imegawanyika katika makundi makubwa mawili ambayo ni ya wakulima na wafanyakazi. Katika makundi hayo ndimo tulimotegemea kuwapata wanasiasa ambao baadaye  waliokuwa wanapata nafasi za kuwa viongozi wetu.
Vile vile lilikuwepo kundi lingine ambalo ni la wafanyabiashara.   Kundi hilo lililokuwa na uzito kutokana na nguvu za kiuchumi lilizokuwa nazo lakini likikosa kujiamini kufuatia laana liliyoipata baada ya Azimio la Arusha lililotanabahisha kuwa nchi hii ni ya makundi mawili ya mwanzo, wakulima na wafanyakazi.
 
Ikumbukwe kwamba Azimio la Arusha liliwajengea wananchi moyo wa kujiamini bila kujali tofauti zao za kiuchumi,  moyo ulioendelezwa hadi kufikia tajiri na masikini kuanza kuitana ndugu. Zaidi ni kwamba haikutegemewa mtu mwenye nguvu za kiuchumi zinazojionyesha wazi ajipenyeze kwenye safu ya uongozi wa wananchi. Sababu ingebidi ajieleze ni njia gani alizozitumia kuupata utajiri kitu ambacho wengi hawakuwa tayari kukifanya. Wakati ule kuupata uongozi ilikuwa inahitaji usafi wa maadili sawa na mwanadamu anayeuhitaji Ufalme wa Mbinguni anavyohitajiwa kuwa na usafi wa roho. Kwahiyo fumbo lile la “tajiri kuingia mbinguni ni sawa na ngamia kupita kwenye tundu la sindano” ndivyo ilivyokuwa kwa matajiri wa hapa nchini kuweza kupata upenyo wa kuingia kwenye uongozi wa nchi.
 
Kwa maana hiyo wafanyabiashara walibaki kuuangalia uongozi wa nchi na kuuheshimu wakiamini kuwa hiyo ni karama ya watu wengine kama nao walivyokuwa na ya kwao ya biashara. Ila walioutamani uongozi iliwabidi kuukana utajiri kama Kristo alivyowambia matajiri kwamba mwenye kutaka kumfuata, kwa maana ya kuutamani Ufalme wa Mbinguni,  agawe mali zake zote kwa masikini kisha amfuate yeye.
 
Mwenendo huo ulidumisha nidhamu katika jamii yetu, watu wakauthamini utu kuliko vitu, matajiri na wafanyabiashara wakiendesha shughuli zao kwa uangalifu wakihofia kuwa pindi wakijisahau mamlaka iliyo juu yao, serikali,  inawawajibisha mara moja.
 
Tunaweza kusema kwamba wakati ule wananchi walikuwa na kinga, walikuwa na pa kukimbilia, walikuwa na mtetezi. Baadaye ukaja wakati wa methali ya sikio la kufa. Watu wenye nguvu za kiuchumi taratibu wakaanza kujisahau,  ndipo serikali ikabidi iwavute sikio kwa kuwakumbusha kuwa hawakupaswa kujenga himaya ndani ya himaya nyingine, himaya yao ikapinduliwa na serikali. Kwa muda watu hao wakaufyata.
 
 Sasa hivi habari hiyo imebaki kwenye kumbukumbu za kale.  Mambo ya leo ni kinyume kabisa cha hayo tunayoyasimulia.  Himaya ile iliyopinduliwa katika mapiduzi tuliyoyaita ya wahujumu uchumi imeishajijenga upya na sasa ndiyo inayoonekana kukalia kiti cha enzi ndani ya serikali yetu. Nani atabisha kuwa kwa hivi sasa serikali haikushikwa na wale wenye nguvu za kiuchumi pamoja na wafanyabiashara? Hali ya mambo inaonekana kugeuka kwa nyuzi 190 kwa maana ya kuyakumbatia tuliyokuwa tunayakataa.  Pale tulipotakiwa kuukana utajiri ili kuupata uongozi, sasa kuupata uongozi bila utajiri ni muhali.
 
Hebu tuiangalie serikali iliyo madarakani kwa sasa.  Ni mtu gani katika safu ya uongozi wa serikali hii, kwa mfano, aliyetokana na makundi niliyoyataja mwanzo ya wakulima na wafanyakazi? Tukimuondoa Rais, Makamu wake na Waziri Mkuu, ni nani mwingine atakayesimama na kusema kwamba si mfanyabiashara? Na katika hali hii tunaushangaaje ugumu wa maisha? Iwapo watu ambao serikali ilikuwepo kuwadhibiti ili wasilete ugumu wa maisha kwa wananchi ndio sasa wameishika serikali na kuidhibiti barabara,  kuuliza tena ugumu wa maisha si ni sawa na kuufuata usemi wa vijana wa kuuliza au kuyashangaa makofi Polisi?
 
Inaeleweka kabisa kwamba wenye nguvu za kiuchumi mtaji wao ni hela, wanapotamani kitu hela yao ndiyo inayoongea. Wanapotamani kulinda maslahi yao ni lazima hela yao iongee. Njia mojawapo ya kulinda maslahi yao wameona sasa ni kuingia kwenye siasa na kupata uongozi ili kuidhibiti serikali ambayo hapo nyuma ilikuwa inawadhibiti wao.
Kwa upande wao mambo yametengamaa. Kwa upande wa walalahoi ili mambo yatengamae ni lazima wahakikishe wanapata uongozi bora utakaojali maslahi yao kwa kuyatilia maanani matatizo waliyo nayo. Na katika kufanikisha hilo mtaji pekee walio nao ni kura zao. Ili kumpata kiongozi ambaye angeweza kusimamia maslahi yetu walalahoi ilibidi tuwe waangalifu na kura zetu. Lakini bahati mbaya tukakubali kurubuniwa na mtaji wa wenye nguvu za kiuchumi kupitia katika mbinu mbali mbali zilizobuniwa kama ile ya takrima na nyinginezo, tukakubali kuyasaliti maslahi yetu na kuwapitisha waliokuwa wanaenda kuyalinda maslahi yao. Kwa hili tumejipiga wenyewe tusilie na mtu.
 
Hebu ona sasa yanayotokea, ugumu wa maisha kwa walalahoi ni neema kwa wenye nguvu za kiuchumi. Mathalan, tuchukulie ugumu wa maisha ulioanza kujitokeza kila baada ya kupitishwa kwa bajeti ya nchi.  Wakati walalahoi  wanakipata cha moto hali ni kinyume chake kwa wenye nacho. Kwa wenye nacho ni wakati wa mavuno ya neema. Nadhani hii inakamilisha ule usemi wa kwamba mwenye kidogo atanyang’anywa na kuongezewa mwenye kingi.
 
Sasa hivi kuna balaa na neema ya upandaji wa bei ya petroli, ni balaa kwa walalahoi na neema kwa wenye nacho. Wenye vyombo vya usafirishaji wametumia nafasi hiyo ya kupanda kwa bei ya petroli kupandisha gharama za usafirishaji kwa kiwango ambacho hakina uwiano hata kidogo na upandaji wa bei ya mafuta hayo. Sio kwamba jambo hilo halijulikani kwa wale tuliowatuma wakatuwakilishe, wanalijua sana na pengine kulishangilia badala ya kulilaani. Ni wabunge wangapi hawanufaiki nalo kwa maana ya kutokuwa na vyombo vya usafirishaji? Sababu naamini walio wengi kama siyo wakurugenzi wa makampuni ya usafirishaji basi watakuwa wanamiliki japo daladala kadhaa. Nani amkumbushe mwenzie madhila wanayoyapata walalahoi?
 
Nitajaribu kuonyesha jinsi wenye nacho wanavyojineemesha na upandaji wa gharama za maisha kwa kutumia mfano wa usafiri katika jiji la Dar es salaam. Tuseme asilimia sabini ya wakazi wa jiji la Dar es salaam wanaishi kwa kipato kisichozidi shilingi elfu mbili kwa siku,  na ili waweze kukipata kiasi hicho inawalazimu wengine kupanda mabasi (daladala) yasiyopungua manne kila siku. Jaribu kufikiria machungu anayoyapata mwananchi wa aina hii inapopandishwa nauli ya daladala hata kwa shilingi kumi tu. Kwa hiyo uchungu wa kupanda kwa bei ya petroli wanaupata watu hawa ambao wengi wao hawatarajii kumiliki chombo chochote cha moto maishani mwao.
 
Upande wa pili,  wenye kumiliki vyombo vya moto kwa ajili ya usafiri,  hasa wale wenye daladala,  wanakuchukulia kupanda kwa bei ya mafuta kama habari njema wanayokuwa wameisubiri kwa hamu ili kuboresha vipato vyao katika biashara zao za usafirishaji.
Tuseme daladala aina ya DCM linalofanya safari fupi kati ya Segerea na Mnazimmoja linafanya mizunguko 14 kwa siku,  saba kwenda na saba kurudi. Tukilikadiria abiria 50 kwa kila safari moja litakuwa limebeba abiria 700 kwa siku, hicho ni kiwango cha chini kabisa sababu hakigusi abiria wanaoteremka njiani na kupanda wengine. Kwa abiria 700 mwenye daladala anakuwa amepata shilingi 350,000 kwa nauli ya shilingi 500/=. Baada ya kutoa hela ya  dizeli ambayo haizidi lita 40 kwa bei  ya  2140/= sawa na shilingi 85,600/= alikuwa anajihakikishia kipato kisichopungua shilingi 264,400/= kwa siku.
 
Fikiria huyo akilinganishwa na mtu anayehangaika kutwa nzima kupata sh. 2000/= uwiano uko wapi?
 
Kwa mtazamo huo nani atabisha kwamba kupanda kwa gharama ya maisha siyo neema kwa wenye nacho? Nani awasemee walalahoi wakati waliowachagua kuwasemea wanaonekana kuneemeka na matatizo yao? Watanzania waliowengi wamegeuka yatima kipindi hiki,  hawana wa kumlilia.
Na Prudence Karugendo
 
0784  989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau