Bukobawadau

KAMPUNI YA WATANZANIA WAZALENDO YAZALISHA MAWE YA DHAHABU MKOANI KAGERA KWA MARA YA KWANZA TANGU UHURU MWAKA 1961

 Profesa Sospeter Muhongo Waziri wa Nishati na Madini Akiwasili Katika Mgodi wa STAMIGOLD Biharamulo Kuzindua Uzalishaji wa Tofali la Dhahabu la Kwaza lililozalishwa na Kampuni ya Watanzania
 Shimo la Kanda ya Magharibi Ambalo STAMIGOLD Wanachimba Dhahabu kwasasa.
Profesa Muhongo Akionyeshwa Ramani ya Uchimbaji wa Dhahabu Katika Shimo la Kanda ya Magharibi.
 Profesa Muhongo Akikata Utepe Kuzindua Matofali ya Dhahabu Yenye Kilo 25 Katika Mtambo wa Kuchenjulia Dhahabu.
 Profesa Muhongo na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Wakizindua Mawe ya Dhahabu na Kuyaonyesha mbele ya waandishi wa Habari
 Picha ya Pamoja
 Profesa Muhongo na Ujumbe aliombatana nao Wakitembelea Mtambo wa Kuchenjulia Dhahabu.
Na Sylvester Raphael
Hatimaye Kampuni ya Watanzania wazalendo STAMIGOLD yaandika historia nchini kwa kuanza uzalishaji wa dhahabu katika mgodi uliokuwa ukijulikana kama TULAWAKA (African Barrick Gold) uliopo Wilayani Biharamulo Mkoani Kagera ambapo tayari dhahabu ya kilo 25 tayari imezalishwa.
Uzalishaji wa  tofali la kwanza  la dhahabu lililozalishwa na Kampuni ya Watanzania STAMIGOLD lilizinduliwa jana tarehe 21/08/2014 na Waziri wa Nishati na madini Profesa Sospeter Muhongo mgodini baada ya kutembelea na kujionea shughuli mbalimbali za uzalishaji  wa dhahabu katika mgodi huo.
Akitoa taarifa ya mgodi huo kwa Waziri Muhongo Meneja Mkuu Bw. Denice Sebugwao alisema STAMIGOLD ilianza uchimbaji na uchenjuaji wa dhahabu tarehe 15/07/2014 katika Kanda ya Magharibi na tayari mawe mawili ya dhahabu yamezalishwa yenye jumla ya kilo 25.
Profesa  Muhongo akizindua uzalishaji wa tofali la kwanza la dhahabu alisema kuwa Kampuni ya STAMIGOLD  ni Kampuni ya kwanza ya Watanzania kuzalisha dhahabu nchini, alisema tangu amalize chuo kikuu mwaka 1979 hajawahi kuona kampuni ya watanzania ikizalisha dhahabu.
Pia waziri huyo wa Nishati na Madini aliipongeza Kampuni ya STAMIGOLD kwa kuajili kampuni nyingine za Watanzania ili kukuza upeo mpana wa ajira. Kampuni zinazofanyakazi na STAMIGOLD ni SUMA JKT katika ulinzi na Kampuni nyingine ya kuchimba dhahabu inayoundwa na Wataalamu wa Kitanzania.
Profesa Muhongo alitoa angalizo kwa Kampuni ya STAMIGOLD kuwa wachape kazi  kwa nguvu siku zote kama walivyoanza na isifike mahali wakazembea na kupelekea kuiua kampuni hiyo. Pia  aliwahakikishia wafanyakazi kuwa wizara ya Nishati na Madini itahakikisha kampuni hiyo inasimama daima.
Kwa kuwa STAMIGOLD ni Kampuni ya Watanzania  Profesa Muhongo alisema kuwa serikali inataka kuonyesha mfano kupitia kampuni hiyo kuwa Watanzania wanaweza kufanya kazi kwa ubora zaidi na kuzalisha dhahabu itakayowanufaisha watanzania wote kwa ujumla.
Maagizo; Profesa Muhongo aliagiza wafanyakazi wa STAMIGOLD kutoutumia mgodi huo kama sehemu ya siasa na harakati isipokuwa uzalishaji wa dhahabu tu. Pia aliuagiza uongozi wa mgodi huo kuwasaidia wachimbaji wadogo ili kuongeza ajira kwa vijana.
Bodi ya STAMIGOLD iliagizwa  kuwa watumishi wote ambao wanakaimu wapewe madaraka kamili ili waweze  kuchapa kazi kwa uhakika zaidi.  Menejimenti ya mgodi huo ihakikishe inawalipa wafanyakazi mishara mizuri ili kuongeza ufanisi wa kazi na ushindani katika soko la wataalam. Mkuu wa mkoa wa Kagera naye aligizwa kuusimamia mgodi huo kwa karibu sana.
Mkuu wa mkoa wa Kagera Mhe. Massawe alimshukuru Profesa Muhongo na serikali kwa ujumla kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo katika mkoa wa Kagera. Alimshukuru Profesa Muhongo kwa kuisimamia vizuri wizara na kuliunda na kulisuka upya shirika la STAMICO.
Pia Mhe. Massawe alimhakikishia Profesa Muhongo kuwa ulinzi na usalama kuzunguka mgodi huo utaimarshwa kwa kushirikiana na wananchi ili kusiwepo na uharibifu na uvunjifu wa amani katika maeneo hayo.
Mgodi wa STAMIGOLD unalengakuisaidia Jamii inayouzunguka mgodi huokwa kusaidia shughuli mbalimbali za kijamii kama kukarabati barabara za vijiji vinavyozunguka mgodi huo, kusaidia katika upande wa afya  aidha kutengeneza na kugawa madawati katika shule zinazouzunguka mgodi huo.
STAMICO (State Mining Cooperation) ni shirika lililoanzishwa mwaka 1972 lengo likiwa ni kuendeleza sekta ya Madini. Shirika hili liliundwa tena upya na serikali mwaka 2008 ili kulipa uwezo wa kufanya kazi iliyo kusudiwa hapo mwanzo.
STAMICO ina miradi ambayo kwasasa inashughulika nayo ili kuleta faida kwa watanzania ikiwa ni kampuni ya ndani. Miradi hiyo ni mradi wa STAMIGOLD Biharamulo, Mradi wa Madini ya tini Kyerwa, Makaa yam awe Kiwira, Tanzanite Melalani, na Mgodi wa dhabu wa Buhemba
Next Post Previous Post
Bukobawadau