Bukobawadau

UHUSIANO WA TZ NA ISRAEL

Uhusiano na Israel, Tanzania iepuke jazba
Na Prudence Karugendo
ILIWAHI kutokea Tanzania ikavunja uhusiano wake wa kibalozi na Israel katika mazingira ya kiutu, mazingira yaliyoonyesha kwamba Israel iliusahau sana utu na kufanya ma bo yaliyoonyesha unyama zaidi. Lakini nchi hiyo ilipojirudi mambo yakabadilika, uhusiano baina ya mataifa haya mawili ukarudi kwenye hali yake ya kawaida.
Nimeshawishika kulijadili hilo kufuatia maandamano yaliyofanywa hivi majuzi na kundi la wau Jijini Dar es salaam, wakiitaka serikali ya Tanzania ivunje tena uhusiano wake na Israel, shinikizo linalofuatia hali mbaya inayoendelea kwa sasa kati ya Israel na Palestina.
Machafuko hayo yamesababisha roho za mamia ya watu kupotea bila sababu yoyote ya lazima.
Ninaposema roho za watu simaanishi za upande mmoja tu, kama baadhi ya watu wanavyolazimisha ionekane, roho za watu zinazopotea ni za pande zote mbili, Irael na Palestina.
Kwahiyo siwezi kuyaangalia machafuko hayo kwa kuuhurumia upande mmoja tu hata kana ndio unaopoteza sana roho za watu. Upande wa pili nao inabidi uangaliwe na kuhurumiwa pia, hata ukionekana unapoteza roho chache za watu, upotevu wa roho ni upotevu wa roho hata iwe ya mtu mmoja, hauna mbadala, roho iliyotoka hairudi.
Ninachokiona kuwa kinakosewa na watu wengi ni kule kuonyesha huruma kwa upande mmoja ulio mnyonge, eti kwa vile unapoteza roho nyingi za watu kutokana na unyonge wake bila kujali kuwa ni upande huo unaoanzisha uchokozi! Imani yangu ni kwamba mnyonge anapoleta unyongaji atanyongwa.
La kustaajabisha ni kwamba wanapouawa Wayaudi inaonekana ni sawa tu, watu hawapigi kelele! Hivi watu wanataka Wayaudi nao wakubali kuwa ni halali wao kuuawa! Wanataka Wayaudi wakiuawa wasijibu!
Kama ni hivyo,  ni nini maana ya kuwa na nguvu na akili za kuzitumia nguvu hizo? Tuseme mtu anaaminika alivyo na nguvu sana katika kundi fulani la watu, lakini anatokea mtoto mdogo  anaamua kumkojolea makusudi na mtu huyo asifanye kitu kwa kuhofia kuonekana ametumia nguvu zake vibaya! Hizo ni nguvu au utahira?
Nakumbuka kama miaka mitano iliyopita niliandika katika gazeti hili, Rai, nikiupinga ubabe wa nchi ya Marekani, makala hiyo niliipa kichwa cha habari “Marekani ni taifa nyamaume”. Saa chache baada ya gazeti hilo kutoka nikapigiwa simu toka ubalozi wa Marekani nikiambiwa kwamba balozi wa nchi hiyo hapa nchini anaomba tuonane.
Yeye balozi alitaka tukutane popote ambako ningeona panafaa, nikaamua tukutane ofisini kwake. Tuliongea tukaelewana kabisa. Moja ya mambo tuliyogusia ni kama haya ya nchi duni kuichokoza  nchi yenye maguvu kwa imani ya kwamba nchi duni ikianza kutandikwa itaanzisha kelele za kwamba inaonewa.
Balozi akatoa mfano wa Tanzania kuitandika Uganda, Vita ya Kagera  1978 – 79, mpaka kufikia kumtoa Idd Amin madarakani. Akauliza, “kwa maana hiyo hata Tanzania tuseme ni taifa nyamaume?”. Kusema ukweli swali hilo lilinifanya nipate kigugumizi, ila kama yupo ambaye angeweza kukabiliana na swali hilo tofauti na mimi ningemkaribisha kwenye mdahalo huu aonyeshe ni namna gani angejieleza.
Machafuko yanayoendelea kati ya Israel na Palestina yametokana na unyama wa makusudi wa Wapalestina walipowaua vijana watatu wa Kiyaudi, Naftali Fraenkel, Gilad Shaer na Eyal Yifrah, bila kosa lolote. Mimi nilikitabiri ambacho kingejiri, ndicho hiki sasa.
Tatizo ni kwamba baadhi ya watu hawataki kabisa kukiangalia kiini cha tatizo bali ukuaji wa tatizo lenyewe. Na ni vigumu kupata tiba ya tatizo usilotaka kujihangaisha kujua kiini chake au kukikwepa makusudi kiini hicho. Hivyo utaishia kutibu dalili za tatizo huku tatizo lenyewe likidi kujiimarisha, hiyo ni sawa na kazi bure.
Kama mataifa yangekilaani kitendo kiovu na cha kinyama cha Wapalestina kuwaua vijana hao wa Kiyaudi ambao hawakuwa na kosa lolote, mpaka Israel ikaamini kuwa kimelaaniwa vya kutosha huku Palestina ikitubu na kuahidi kutoruhusu kitendo cha aina hiyo kujirudia tena, bilashaka Israel nayo ingechukua maamuzi tofauti na ya sasa.
Lakini kwa kuona kitendo hicho ni kama kimebarikiwa na jumuiya ya kimataifa, Israel haikuwa na lingine la kufanya zaidi ya kulipiza kisasi huku ikijihami. Ikumbukwe anayeingia kwenye ugomvi haangalii pa kupiga ili kuepuka kumuumiza anayegombana naye, anachotaka aumie basi.
Na katika sakata hilo ndipo kikaingilia kikundi cha Hamas, chenye kila dalili za ugaidi.
Nasikitishwa na wanaoilaumu Israel wakiwa wameikwepa historia ama kwa makusudi, kwa usahaulifu au kwa kutokujua. Wayaudi ni jamii iliyopata misukosuko mikubwa sana ikiwa inalengwa kuhangamizwa kusudi ipotee kabisa kwenye uso wa dunia. Kinachoifanya jamii hiyo iendelee kuwepo mpaka sasa nayo ni maajabu mengine ya dunia!
Wapalestina, wakiungwa mkono na jamii yote ya Kiarabu, hawautambui uwepo wa taifa la Israel! Sasa nini kifanyike kama sio Israel kujihami na kushambulia kwa njia ya kulipiza kisasi pale inapobidi? Na kwa nini inapotokea hivyo walaumiwe wao tu bila kuwahusisha maasimu wao wanaotaka kuwahangamiza?
Mashambulizi dhidi ya Israel yanaendeshwa kwa njia za kigaidi; ugaidi naufananisha na ujambazi. Lakini walau lengo la ujambazi linaeleweka, kupata mali kwa njia haramu. Sielewi lengo la ugaidi ni nini!
Ugaidi sawa na ujambazi, unapaswa utokomezwe. Mfano hapa nchini kwetu ujambazi upo, kwahiyo tukisema tuutokomeze itaeleweka kuwa tunawaonea wanaofanya ujambazi?
Na inapotokea mzazi ana watoto majambazi, anawatetea kwa kutotaka wakamatwe na kuchukuliwa hatua wanazozisitahili, pengine kutokana na mzazi kujinufaisha na ujambazi huo, akikamatwa mzazi mwenyewe ili akaonyeshe waliko watoto wake majambazi atakuwa anaonewa kweli?
Je, wanaoutetea ujambazi huku wakijenga majumba na kuyazungushia uzio (fence) sawa na za magereza, kwa maana ya kujifunga wenyewe kwa kuhofia hujuma za majambazi tuwaeleweje? Kama unawatetea majambazi ya nini kuwahofia?
Hamas ni kikundi sawa na Boko Haramu, Al – Shabaab, Al – Qaeda nakadhalika. Hamas wanahifadhiwa na Palestina, nchi hiyo inaona furaha kikundi hicho kinapoishambulia Israwel bila kujali kinasababisha maafa kiasi gani katika nchi hiyo. Je, Israel isijilinde, isijibu mapigo? Na mapigo itayajibu vipi wakati Hamas wako ndani ya Palestina wakiwatumia watu kama ngao zao?
Nikumbushe kidogo Vita ya Kagera, 1978 – 79. Maaskari shupavu wa JWTZ walitaka kuiteka miji ya Uganda bila kuihangamiza, lakini askari wa Amin wakawa wanapandisha mizinga kwenye maghorofa na kuanza kuwashambulia askari wetu kwa chini! Ndipo ikabidi JWTZ waanze kuyaporomosha baadhi ya maghorofa kuelekea kupata ushindi.
 
Sasa wanaoilaumu Israel wanataka ifanye nini? Wanataka ikae tu ikubali kushambuliwa na magaidi bila kujitetea kwa vile magaidi hao yamejificha kwenye watu na kuwageuza ngao?
Kumbuka ofisi za ubalozi wa Marekani, Dar es salaam na Nairobi, mwishoni mwa miaka ya 1990,  zilishambuliwa na magaidi ambao hawana uhusiano wa mbali na Hamas. Watanzania na Wakenya ndio waliokufa kwa wingi, leo hii baadhi ya Watanzania wanataka magaidi wasisumbuliwe ili waendeleze biashara yao ya ugaidi kwa sitarehe!
Mimi sitaki Wapalestina wasio na hatia wauawe kama ambavyo sitaki Waisrael wasio na hatia wauawe kwa kushambuliwa bila sababu yoyote. Kwahiyo la kufanya ni kutafuta kiini cha mashambulizi ya Wapalestina, hasa kikundi cha Hamas, dhidi ya Israel ni nini. Maana mashambulizi ya Waisrael dhidi ya Wapalestina yanaeleweka sababu zake, ni kujibu mapigo.
Kinachopaswa kupingwa na kulaaniwa kwa nguvu zote ni ugaidi pamoja na mataifa yanayoufuga ugaidi. Tusijifanye tunaihurumia Palestina wakati inao mradi wa kufuga ugaidi unaotusumbua hata sisi tusiohusika na mizozo yao.
Ni lazima tuishauri nchi hiyo iachane na mradi huo ili amani ipatikane katika eneo hilo kusudi roho za watu wasio na hatia zipate kulindwa.
Israel haiwezi kuwa na nguvu ambazo haitakiwi kuzitumia kujilinda dhidi ya ugaidi. Utakuwa ni uchizi kuwa na nguvu ambazo huwezi kuzitumia kujihakikishia usalama.
Hapo ndipo nayaona madai mengine kama kituko, kwamba Hamas inaishambulia Israel kusudi nchi hiyo inayoshambuliwa ikubali kukaa kwenye meza ya mazungumzo, kichekesho kweli. Yaani Israel ikubali kukaa meza moja na Hamas kuzungumza kwamba yenyewe ni taifa ambalo halipo katika ramani ya dunia!
Kitu kingine ni kuwa madai ya kwamba Hamas ni kikundi kinachotumiwa na Palestina kutetea maslahi ya Wapalestina hayawezi kuingia akilini hata kidogo. Sababu hata kama Israel ikiamua kukubaliana na Palestina kwa kila kitu, mpaka kufikia taifa hilo kujifuta kabisa, haiwezekani huo ukawa ndio mwisho wa Hamas. Lazima itatafutwa sababu nyingine ya kikundi hicho kuendeleza ugaidi na mauaji ya watu wasio na hatia.
Hebu tuitazame Nigeria inavyosumbuliwa na Boko Haramu, Al – Shabaab ilivyoisambaratisha Somalia na kisha kuigeukia Kenya, ina maana nako huko kuna Israel?
Kwahiyo Watanzania wanaodai kwamba Tanzania ivunje uhusiano wa kibalozi na taifa hilo teule, kwa mujibu wa vitabu vitakatifu, inawabidi watafakari kwanza kabla ya kuendeleza madai yao hayo.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau