Bukobawadau

KATI YA KOMBA NA MBOWE NANI ALIPASWA KUHOJIWA NA POLISI?

NA PRUDENCE KARUGENDO
UKIUKAJI  wa haki za binadamu tuliokuwa tukiusikia kwa wenzetu, hususan nchini  Afrika Kusini enzi za makaburu, kuikandamiza haki ya walio wengi kwa manufaa ya wachache, sasa tunaushuhudia wenyewe hapa nchini kwetu!
 Vitendo vya kutumia mabavu ya dola kupita kiasi, kuwasakama na kuwakandamiza walio msitari wa mbele kutetea haki ya umma, kuwasambaratisha wananchi wanaowaunga mkono watetezi wao bila kujali kwamba wananchi hao hawana silaha yoyote ya kujihami,  au kama ni watoto, wazee, walemavu nakadhalika, ndiyo yanayojionyesha hapa kwetu kwa sasa!
Ikumbukwe enzi hizo za makaburu Tanzania ilikuwa msitari wa mbele kuyapinga na kuyalaani matendo hayo ya kinyama yaliyokuwa yanafanywa na makaburu dhidi ya wananchi wa Afrika Kusini. Sijui kwa sasa ambapo ukatili huo dhidi ya wananchi wapenda haki  umehamia Tanzania nani atakuwa msitari wa mbele kuupinga na kuulaani, pengine Afrika Kusini yenyewe!
Inapofikia mahali mwenye kuahidi uovu wa hatari akaonekana shujaa, lakini mwenye kuuliza kwa nini uovu uahidiwe akaonekana mhalifu na kuitwa akahojiwe na Polisi, tunawezaje kuitofautisha nchi yetu na Afrika Kusini enzi za makaburu?
Isipokuwa kuna tofauti kidogo inavyoonyesha unafuu kwa vyombo vya dola vya makaburu. Pamoja na vyombo vya dola vya Tanzania kujitahidi kuiga staili ya ukandamizaji wa makaburu lakini kuna mahali vinaonekana kuzidisha ukatili ambao makaburu hawakuwahi kuufanya.
Mfano,  kuua na kujeruhi wanahabari ni matukio ya kinyama ambayo hayakuwahi kufanywa na makaburu. Na kibaya zaidi hapa kwetu wanaosimamia unyama huo wanapandishwa vyeo kama motisha wa kazi hiyo ya kinyama wanayokuwa wameisimamia! Mfano mmojawapo ni wa aliyekuwa RPC wa Iringa, Michael Kamuhanda,  aliyepandishwa cheo toka SACP na kuwa DCP baada ya kusimamia na kufanikisha mauaji ya mwanahabari, Daudi Mwangosi, kule Nyololo, Iringa.
Hebu tuangalie yanayojaribu kufanana. Chama cha ANC, Afrika Kusini, kilichokuwa kikiungwa mkono na wananchi wazalendo walio wengi, kiliwatia makaburu tumbo joto na kuwafanya waanze kukitabiria kila lililokuwa baya. Lakini haikusaidia kitu sababu utabiri haukutimia mpaka makaburu walipolazimika kukipiga marufuku nchini mle.
Hapa kwetu kila chama cha upinzani kinachochomoza na kukikaba vizuri chama tawala kinasakamwa kwa aina mbalimbali na chama tawala na kuhakikisha nguvu za chama hicho pinzani zinapotea. Hiyo yote imekuwa tofauti kwa Chadema.
Pamoja na makada mbalimbali wa CCM kutabiri kwamba mwisho wa Chadema ni 2014, sasa ni mwezi wa 9 na Chadema ndio kwanza inaonyesha kuimarika kuliko muda wote uliopita, hasa baada kumalizika mkutano wake mkuu wa majuzi ambao mafanikio yake hayajawahi kuonyeshwa  na  mkutano wa chama chochote kingine cha upinzani toka mfumo wa vyama vingi urudishwe nchini.
Hata makamu wa mwenyekiti wa CCM, Philph  Mangula, amekiri kuwa kuna mambo amejifunza kwenye mkutano huo wa Chadema wakati akitoa salaamu kwa wajumbe wa mkutano huo.
Kutokana na mkutano huo kudhihirisha utabiri feki wa makada wa CCM, ni wazi kuwa CCM hawakuufurahia au kuyafurahia mafanikio hayo ya Chadema. Hivyo zikaanza kufanyika mbinu nyingine za kukisakama chama hicho katika jitihada za kutaka kukidhoofisha, mbinu zinazosukumwa na woga wa mabadiliko walio nao makada wa chama tawala.
Mara nyingi woga wa mabadiliko ya kisiasa  katika nchi nyingi unaletwa hasa na mambo mawili. Moja ni ubinafsi na pili ni uovu dhidi ya umma. Haijawahi kutokea woga wa aina hiyo ukatokana na uzalendo kwa nchi.
Yeyote aliye mzalendo atakuwa anafanya mema kwa nchi yake na kwa wananchi wenzake. Mzalendo wa aina hiyo hawezi kuyahofia  mabadiliko ya kisiasa nchini mwake hata kidogo. Sababu hana deni lolote kwa nchi yake wala kwa wananchi wenzake.
Mfano mzuri kwa hilo uko katika nchi zilizoendelea kama Marekani, Wingereza na nchi nyingine nyingi za Magharibi. Hata katika baadhi ya nchi za Mashariki ya Mbali zikiongozwa na nchi za India na Japan. Katika nchi hizo vyama vya siasa vyenye itikadi tofauti vinabadilishana uongozi wa nchi bila woga wowote, ni kwa sababu vinajiamini kuwa havina madeni ya uovu vinaoufanya vikiwa madarakani.
Katika siasa, hasa za bara la Afrika, kuna aina mbili ya wanasiasa. Wapo wanaofanya siasa kiuzalendo na wengine wakifanya siasa kama shughuli yao binafsi, wabinafsi. Aina hiyo ya pili ndiyo inayozalisha mafisadi, na ndiyo yenye kuhofia mabadiliko. Wanasiasa wote wa aina hizo mbili tunawatambua kwa matendo yao.
Mfano, mwaka 2005, aliposhinda Kikwete na kutangazwa rais wa Tanzania kwa kipindi cha miaka 5 ya mwanzo aliyekwenda wa kwanza kumpongeza kwa kumkumbatia alikuwa ni mpinzani wake katika uchaguzi huo, Freeman Mbowe. Kilichoonekana ni kwamba Mbowe hakuwa na kinyongo cha kuukosa urais sababu alichokuwa anawania kilitokana na msukumo wa uzalendo na sio ubinafsi. Sababu wapo walioonyesha moyo wa ubinafsi kwa kutoenda kwenye sherehe za kumtangaza rais mwaka huo.
Rais Kikwete naye  kwa moyo wake wa uzalendo, wakati anamalizia muda wake wa uongozi wa nchi, akakubaliana na upinzani kuiachia nchi Katiba Mpya. Ni uamuzi wa kiuzalendo. Lakini baadhi ya watu waliomzunguka wakiutanguliza ubinafsi katika chama chake, CCM, wakamlaumu kwa uamuzi wake huo,  wengine wakidai kwamba suala hilo halikuwa kwenye Ilani ya chama chao!
Mpaka wengine wamefikia hatua ya kumtukana rais kiaina wakijidai wanamtukana Jaji Warioba ilhali wakielewa kwamba Warioba alikuwa akifanya kazi aliyopewa na Rais Kikwete kuifanya kwa niaba yake kama msaidizi tena chini ya kiapo.
Ndiyo maana watu hao wabinafsi na watovu wa uzalendo wamediriki kuuchakachua uzalendo wa Kikwete kwa nchi yake kwa kuyabadilisha maoni ya wananchi kuhusu Katiba wanayoitaka kusudi  ibaki vilevile kama ilivyokuwa mwanzo, tena bila kuzingatia wala kujali  gharama kubwa iliyokwisha kutumika mpaka kufikia hapo.
Watu hao hawawezi kuijali gharama sababu hawana uzalendo unaowatuma kufanya hivyo. Kilichopo ni ubinafsi tu basi.
Baada ya mambo kuwa hivyo ndipo likajitokeza kundi la wazalendo na kujiita Umoja wa Katiba ya Wananchi, UKAWA. Kundi hilo linapinga juhudi zote zinazofanywa na walioukosa uzalendo na kuutanguliza ubinafsi.
Kwahiyo Ukawa kwa kuliona kundi la wabinafsi limeng’ang’ania kuendelea na mchakato ambao hata aliyeuanzisha, Rais Kikwete, kaishakata tamaa kuwa hauwezi kuzalisha kile alichokikusudia kwa wakati huu, likaamua kuususa mchakato huo.
Ndipo Chadema, kupitia kwenye mkutano wake mkuu, likatolewa tamko la kuwataka wananchi kuupinga ubadhirifu wa kutumbua bure pesa za walipakodi unaofanywa na wabinafsi hao pasipo lolote linalotegemewa kupatikana.
Kinachodhihirisha ubinafsi huo ni kwamba hata baadhi ya wale waliogoma kushuhudia Kikwete anatangazwa kuwa rais kwa mara ya kwanza, kutokana na hasira za wao kuukosa urais, leo hii nao wamo wakijifanya kukiendeleza kitu alichokianzisha Kikwete lakini akiwa hana imani tena kama kinaweza kufanikiwa! Kama huo sio ubinafsi ni kitu gani?
Tamko la kuupinga ubinafsi na ubadhirifu huo lililotolewa na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, linaonekana lilivyovaliwa njuga na mamlaka za juu za nchi likidaiwa ni la uchochezi. Mwenyekiti huyo ameitwa na kuhojiwa Polisi juu ya tamko hilo.
Nashindwa kupata uwiano kati ya tamko hilo la kuupinga ubadhirifu dhidi ya pesa ya walipakodi na tamko lililotolewa Bungeni na kada wa CCM, John Komba, la kutaka kuanzisha vita ya msituni iwapo matakwa yake hayatafanikiwa! Lakini Polisi haikuchukua hatua yoyote dhidi ya kauli hiyo ya kigaidi!
Badala yake Polisi inahangaika na kauli ya Mbowe ya kuwataka wananchi waandamane ili kutetea pesa yao inayoteketezwa na wabinafsi wasiowajali wananchi wenzao!
Kumbuka wagonjwa wengine wanakata roho kwa kukosa madawa, kisa hakuna pesa, wanafunzi wa elimu ya juu wanakosa kuendelea na masomo yao kisa hakuna pesa ya mkopo, walimu wanakosa vitendea kazi kwa kisingizio hichohicho. Wafanyakazi wa kima chini bado kipato chao kwa mwezi hakilingani na pesa inayofujwa kwa siku na mtu mmoja kule Dodoma nakadhalika.
Hata kama Katiba ingepatikana kweli, ina maana kuishughulikia kunawafanya wahusika wawe viumbe tofauti na Watanzania waliobaki kiasi cha kuwaachia wakatumbue pesa yote hiyo bila kuyajali niliyoyataja hapo juu?
Ni Mtanzania gani asiyeuona ubadhirifu huo? Hasa inaposemwa kwamba Katiba Mpya haiwezi kupatikana kwa kipindi hiki, lakini baadhi ya wananchi waliokosa uzalendo wakang’ang’ania kuendelea na zoezi hilo la kuikamua nchi yao bila huruma yoyote?
Kwahiyo tamko la maandamano ya amani kuupinga ufujaji huo linaonekana linahatarisha amani na usalama wa nchi. Lakini lililotolewa na mbinafsi Komba, la kwenda msituni kuanzisha vita, kwa wahusika hilo halitishii chochote kwa usalama wa nchi!
Kwenda msituni ni kuua utulivu na usalama wa nchi, ni kuua wananchi, kuua uchumi wa nchi na kuiua nchi yenyewe kwa ujumla. Lakini aliyetoa tishio hilo mpaka sasa anaonekana ni jasiri na shujaa!
Wakati kauli ya Komba inaonekana ni hatari kwa nchi na wananchi, kauli ya Mbowe ni hatari kwa ubadhirifu na ufisadi unaoendelea kuiteketeza nchi yetu.
Kitu kingine ni kwamba kauli ya Mbowe inalenga kulilinda kusudio la Rais Kikwete la kujiandikia historia pekee ya kuiachia nchi Katiba mpya na iliyo bora, kusudio ambalo baadhi ya wabinafsi hawalipendi na kuamua kulitengua.
Sasa kati ya Mbowe na Komba nani mbaya na nani adui kwa nchi yetu? Nani alipaswa ahojiwe na Polisi kama kweli hekima inatamalaki?
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau