Bukobawadau

MAELEZO YA MGOMBEA WA BAVICHA TAIFA FRANCIS BONIFACE MARWA

 UTANGULIZI
Ndugu zangu watanzania,
awali ya yote niwashukuru sana, ninyi nyote mtakaobahatika kukutana na huu ujumbe wangu mahususi ndani ya mitandao hii ya Kijamii, magazetini ama kupitia chombo kingine chochote kile cha habari ambacho nitaweza kumudu gharama zake ili kuifanikisha azma hii ya kuwafikishieni ujumbe wangu, juu ya nini hasa kimenisukuma kuingia katika kinyang'anyiro hiki cha kuiwania nafasi ya "Mratibu wa Hamasa" BAVICHA ngazi ya Taifa.

Natambua macho yote ya watanzania ndani ya mipaka ya Taifa letu, yameelekezwa kwenye chaguzi za Chama chetu zinazoendelea Nchini kote hivi sasa, ama wapo wanaozitakia mema, na wapo wanaozitakia shari, ili kesho wapate jambo la kuupotoshea umma, kupitia majukwaani, na vijiwe vyao vya kahawa, uji, Draft na Pool table.
Kutokana na hayo yote,
na mengine mengi zaidi, ndio sababu wengi wetu hususani sisi vijana, tumechukua maamuzi magumu ya kuomba nafasi za uongozi ndani ya Taasisi hii pendwa kuliko zote Nchini, ili tupate fursa za kuitetea na kuilinda kama mboni ya Jicho.

Baraza letu la Vijana (BAVICHA),
ni moyo wa Chama hiki, na hii ndio sababu, upo ulazima wa kuijenga na kuiimarisha BAVICHA na iwe imara, yenye misimamo isiyoyumbishwa na dola, tena yenye maamuzi magumu kwa maslahi ya Chama na wazalendo wa Taifa hili kwa ujumla wao, ambao ndio walipa kodi.

NIMEFANYA NINI NDANI
YA CHAMA

Nimeichukua rasmi Kadi ya
Chama mwaka 2001 huko kwetu Serengeti Mara, mwishoni mwa mwaka 2009 kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa nikiwa Shuleni Kidato cha Pili, nikachaguliwa kuwa Katibu Mwenezi wa Chama ndani ya Kata yangu. Baada ya kukabidhiwa majukumu hayo ya kuibeba dhamana ya Chama, licha ya kwamba nilikuwa Shuleni, nilijituma kadri ya uwezo wangu kukijenga na kukieneza Chama ndani na nje ya kata yetu, kupitia michezo ya Shule za Sekondari, kwa kukutana na watu Sokoni, minadani na hata pia kupitia Vikundi rika vya Maendeleo huko vijijini, ambavyo huko kwetu Mara tunaviita "Saiga".

Uchaguzi ulipotangazwa rasmi,
tukawaandaa wagombea wetu, na tukaingia msituni kupambana, baada ya uchaguzi, tukashinda wenyeviti wawili wa vitongoji kati ya watatu waliopo kijijini kwetu, cha kushangaza, CCM wakashinda nafasi moja ya kitongoji, ila wakamtangaza Mwenyekiti wa Kijiji kigumashi, jambo lililonikera sana, haijawahi kunitokea.

Baada ya uchaguzi huo wa Serikali za mitaa, ikafata zamu ya uchaguzi wa Serikali Kuu, madiwani, wabunge na Rais.
Hapa sasa, ilikuwa ni patashika nguo kuchanika, kwa kuwa walitunyang'anya nafasi ya Mwenyekiti wa Kijiji kwa mabavu, ikabidi tuwaandae vijana wenzetu kuhusu namna ya kukabilisna na uchaguzi Mkuu uliokuwa mbele yetu ili kuhakikisha kwamba Diwani wetu wa CHADEMA anashinda nafasi hiyo.

Licha ya kwamba ilikuwa
ndio mara yetu ya kwanza kuwasimamisha wagombea wa CHADEMA ndani ya Kata yetu na Jimboni kwetu tangu Nchi ipate uhuru, lakini nadhibitisha hili hadharani kwamba,
Kata yetu ya Nyansurura ambayo mimi ndiye Kiongozi wa Chama mwenye dhamana ya Uenezi, ni miongoni mwa Kata 6 pekee zinazoongozwa na CHADEMA kati ya Kata 28 za Jimbo la Serengeti huko Mkoani Mara.

Jimboni kwetu (Serengeti) nako
pamoja na kwamba ndio uliokuwa mwanzo wa kumsimamisha mgombea wa CHADEMA kwa nafasi ya Ubunge, nilikuwa miongoni mwa vijana walioshiriki kikamilifu katika kumpambania mgombea wetu, mpaka hatua ya mwisho.
Nafarijika sana kutamka kuwa,
pamoja na masahibu mengi tuliyokumbana nayo katika kipindi chote cha uchaguzi, tulifanikiwa kupata kura 19,700 ambazo ni sawa na 41% ya kura zote, ili hali mgombea wa CCM akatangazwa kigumashi kwa 54% ya kura zote, huku mwenzetu wa CUF akipata 5% ya kura zote.

Licha ya kwamba mpaka leo hii sikuwahi kukata au kukatishwa tamaa na mtu yeyote yule, lakini nimeendelea kuwa mwaminifu, mtiifu, mwadilifu, mjukumikaji katika shughuli zote za kichama popote pale zinapotokea ndani ya mipaka ya Nchi yetu, na hata wakati mwingine nimeendelea kuwa msiri sana kwenye mambo muhimu na nyeti ya Chama chetu, tena mambo yanayohitaji vikao maalumu vya Chama ili kuyazungumza, ili kuilinda heshima na hadhi ya Chama chetu, maana ninaamini kuwa wasakatonge watabana sana ila mwisho wao utakapofika wataachia.
Nje ya Jimbo na Katani kwetu,
nimekuwa miongoni mwa vijana wenye nia na moyo wa dhati katika kukipigania Chama masaa 24.
Ninaendelea kushiriki harakati zote za kukijenga na kukieneza Chama hiki, kila ninapokutana na harakati hizi ndani ya Nchi yetu.

Ninaendelea kushiriki Mikutano mbalimbali ya kukijenga Chama, nimekuwa nikishiriki katika midahalo, matamasha na makongamano mbalimbali yaliyofanyika Nchini kwa ajili ya kutoa elimu kwa watanzania,
juu ya mchakato wa Katiba mpya unaoendelea Nchini hivi sasa, mchakato ambao Chama changu ni miongoni mwa Taasisi zinazoitetea Rasmu ya Tume ya Jaji Warioba, yenye maoni ya wananchi yaliyokusanywa kwa mujibu wa Sheria.

Nitaendelea kukitetea, kukijenga na kukilinda Chama hiki kama Mboni ya Jicho, popote nitakapokuwa, iwe ndani au nje ya mipaka ya Nchi yetu.
NITAFANYA NINI NDANI YA
BAVICHA TAIFA NA CHAMA
KWA UJUMLA

Sote tunatambua kuwa,
CHADEMA bila Mabaraza haya ya BAVICHA, BAWACHA na WAZEE tena yaliyo imara, ni sawa na Bunge la Katiba bila Tundu Lissu, Halima Mdee na Jussa Ladhu wa Zanzibar.

Kwa kushirikiana na Viongozi wenzangu wa Baraza na Chama kwa ujumla, tutakwenda kuangalia namna bora ya kukitafutia wigo mpana kitengo hiki cha hamasa Nchini, ili huduma iweze kuwafikia walengwa kwa haraka na wepesi zaidi, tofauti na ilivyo sasa
kwa mfano kwamba, mtu wa Uhamasishaji aliyeko Makao Makuu ya BAVICHA Taifa, ndiye atakayefika Songea, Pemba, Mwanza, Tabora, Lindi au Tarime, ndipo huduma ya hamasa iwafikie wananchi wa eneo hilo husika.

Hapa namaanisha nini,
namaanisha kwamba, kwenye kitengo hiki cha hamasa ndani ya BAVICHA Taifa, tutafanya ugatuaji wa madaraka kutoka Makao Makuu ya Baraza na kukasimisha mamlaka hayo katika ngazi zote za uongozi wa Chama, kuanzia Taifa, Kanda, Mikoani, ndani ya Wilaya/Majimbo, Kata/Shehia, Matawi na Misingi.

Utaratibu huu mpya nitakaokwenda kuuanzisha,utafanikiwa kwa kutoa elimu kwa watu maalumu watakaoteuliwa na wataalamu wa mafunzo ya Chama kwa kushirikiana na Baraza, ili kusudi, baada ya wao kupata mafunzo hayo kutoka kwa wataalamu wa mafunzo wa Makao Makuu ya Chama, nao watapelekwa kwenye Kanda.
Baada ya watu wa Kanda kupata mafunzo hayo ya Uhamasishaji, nao watapelekwa Mikoani, ili kusaidia kutoa elimu kwa watu wa Wilaya/Majimbo, nao watu hawa wataipeleka elimu hii ya hamasa kwa watu wa Kata zao, na hawa wa Kata watakwenda kutoa elimu ngazi ya Matawi na hawa wa Matawi nao, watatusaidia kuipeleka elimu hii ya hamasa kwa watu wa ngazi ya msingi.
Ndugu zangu watanzania,
yapo mengi naamini kwa kushirikiana nanyi, naamini nitayafanya, ila kikubwa zaidi, natambua ni uaminifu, uwazi, uwajibikaji, uadilifu, heshima na utii wa kanuni na taratibu za Chama chetu, zilizoainishwa katika Katiba yetu ya Chama.

Nihitimishe kwa kuwatakia kila la kheri ninyi nyote mnaoendelea na chaguzi za ndani ya Chama, sio tu kwa wale wa ngazi za Wilaya/Majimbo, hata pia ninyi wa chaguzi za ngazi za Mikoa.
Ahsanteni sana!!!
Francis Boniface Marwa,
Mgombea wa nafasi ya
Mratibu wa Hamasa
BAVICHA Taifa 2014.
0785881009/07678810090
01/09/2014.
*****************

Aluta Continueeee........
Next Post Previous Post
Bukobawadau