Bukobawadau

MSIMAMO WA SITTA NI WA KWAKE AU KAAGIZWA?

Na Prudence Karugendo
NILIDHANI  Mheshimiwa Samuel Sitta alipoapa kuwa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba alifanya hivyo kuleta imani yake kwa wananchi kuwa ataiongoza shughuli  aliyokabidhiwa akiwa ameilinda, kwa uwezo wake kitaaluma, akiwa amefuata utaratibu na sheria za sheghuli hiyo zinavyoelekeza, mpaka shughuli yenyewe itakapokamilika.
Lakini sasa yanayofanyika chini ya uongozi wake wakati shughuli hiyo ikiendelea yananifanya nijiulize kwa nini Sitta alikubali kula kiapo! Maana ameamua kukibadili kabisa  alichokabidhiwa na kuleta kingine, cha kwake, tofauti na kiapo chake kinavyomuelekeza, kana kwamba alikabidhiwa shughuli hiyo iwe mali yake binafsi!
Shuguli hiyo ninayoisema ni ya kuongoza Bunge Maalumu la Katiba. Bunge hilo limeundwa kwa ajili ya kuandika Katiba ya nchi,  baada ya kuyapitia na kuyajadili maoni ya wananchi yanayotaka Katiba yao iwe na mwonekano wa namna gani,  yaliyomo kwenye rasimu iliyokabidhiwa kwa Bunge hilo linaloongozwa na Sitta.
Hicho ndicho kitu ambacho Sitta na wajumbe wa Bunge hilo waliapa kukifanya wakiwa wameyaheshimu matakwa ya wananchi.
Lakini sasa, badala yake, Sitta anaonekana kuliongoza Bunge hilo kufanya kitu kilicho nje kabisa ya kiapo chake! Mbali ya kuridhia kuondolewa vifungu kadhaa vya maoni ya wananchi kwenye rasimu, jambo linaloonekana ni kutowaheshimu wananchi ambao ndio wenye Katiba, Sitta kadiriki kufanya kazi nyingine kabisa nje ya kiapo chake!
Kaanza kukusanya upya maoni toka kwa makundi mbalimbali ya wananchi, kazi iliyokwishafanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya kiapo, yeye anaamua kuirahisisha na kuifanya nje ya kiapo. Sitta kaapishwa kuijadili rasimu na ikiwezekana kuiboresha, si kukusanya upya maoni ya wananchi maana hiyo si kazi yake.
Katika kuhalalisha kinachojionyesha kama uchakachuaji wa maoni ya wananchi, rasimu, Sitta katamka kuwa rasimu sio msaafu. Nadhani kwa hapo maana yake ni kwamba alikuwa nayo haki ya kuyachakachua maoni ya wananchi kadiri atakavyo kwa vile maoni hayo sio jambo lililokuwa na kinga ya Kimungu.
Aidha, Sitta aliongeza akisema kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu sio mazuzu, kauli inayoonekana imejaa utata mwingi. Sababu kama kataja mazuzu ina maana yeye kwenye fikra zake kaishawaona hao mazuzu, ingebidi atueleze ni kina nani? Au tuseme mfumo mzima uliobariki wazo la upatikanaji wa Katiba Mpya, baadaye ikaundwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba pamoja na wananchi waliotoa maoni, ndio umejaa mazuzu?
Sababu kitendo cha wewe kujiona sio zuzu na hivyo kuamua kuifumua kazi nzima uliyokabidhiwa kwa kiapo ili ukaiboreshe bila kupunguza kilichomo, kinaonyesha waliokukabidhi kazi hiyo ndio mazuzu!
Hiyo imejidhihirisha kufuatia msisitizo wake wa kuwa rasimu aliyokabidhiwa ilionekana kujaa mapungufu, kwahiyo, kwa tafsiri yangu, wasiokuwa mazuzu wakaamua kuifumuoa na kuiunda upya badala ya kuiboresha kama walivyoapishwa kufanya!
Lakini kama mchakato huu wa kuandika Katiba Mpya unasimamiwa na sheria maamuzi hayo ya Sitta ya kukiuka maoni ya wananchi yanatokana na kifungu kipi cha sheria? Sababu sasa kinachofanyika sio kuboresha kilichopo kama sheria inavyosema, maana kilichopo ni rasimu iliyotengenezwa kutokana na maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Sitta akaapa kuizingatia katika kuandika Katiba mpya.
Lakini badala yake anakusanya upya maoni ya wananchi, bilashaka kwa namna inavyompendeza yeye binafsi na sio kama anavyoona inafaa. Neno kufaa linatumika kwa ajili ya umma. Ni kwa vipi atatushawishi tukubali kuwa anaboresha kulingana na kiapo chake?
Bunge Maalumu la Katiba linakusanya maoni ya wananchi! Kama ulikuwepo uwezekano wa Bunge hilo kukusanya maoni na kuyafanyia kazi ili ipatikane Katiba Mpya kwa nini rais hakushauriwa kutojihangaisha kuunda Tume ya Mabadiliko ya Katiba kusudi lenyewe liweze kuyakamilisha yote kwa pamoja?
Na kwa jinsi mambo yanavyoenda, kufanyika bila dalili zozote zinazoonyesha kuwa kuna kiapo kinachowazuia watu wasitoke nje ya mipaka fulani wanapotekeleza shughuli waliyopewa, kulikuwepo na sababu gani ya kuwaapisha watu katika shughuli kama hii?
Kama madai ya Sitta ni ya kweli, naye kala kiapo, kwa nini baada ya kuona rasimu imejaa mapungu mengi asishauri Bunge livunjwe ili mchakato ukaanze upya? Au kama hilo lisingewezekana kutokana na kufungwa na sheria iliyoliunda Bunge hilo, kwa nini yeye asijiuzulu katika kuonyesha msisitizo. Sababu hakuna sheria inayomzuia mtu kufanya hivyo tena ikiwa ni kwa manufaa ya umma, kuliko kujifanyia mambo yaliyo nje ya sheria kwa madai ya kuunufaisha umma.
Katika mazingira ya aina hii tunawezaje kuitarajia Katiba Mpya itakayomlazimisha mtu aape kuilinda? Sababu kinapopatikana kwa kukiuka kiapo kinawezaje kikamhitaji mtu ale kiapo ili kukilinda?
Tukiufuatilia msimamo wa Sitta ulivyo, kwamba mambo ya kisheria sio msaafu, tunaweza tukajiuliza kwa nini tuhangaike kuandika Katiba? Sababu sidhani kama tunaweza kuipata Katiba iliyo na kinga ya Kimungu, kwa maana ya msaafu. Tutaishia kupata Katiba ambayo kila mmoja wetu anaidharau kwa msimamo huohuo,  kama wa Sitta,  wa kwamba taratibu zilizoundwa na mwanadamu sio maelekezo ya Mungu, nani atakayeiheshimu Katiba Mpya?
Lakini inawezekanaje watu wenye akili timamu tushindwe kujiwekea taratibu na kanuni za kuendesha maisha yetu na kuziheshimu eti kwa vile sio maelekezo ya Mwenyezi Mungu? Sisi tutakuwa ni viumbe wa aina gani?
Kwa mpangilio huo tunawezaje kuwa na sheria? Sababu kwa hoja hiyo ya Sitta, ambaye ni mwanasheria kitaaluma, sheria zote tunazozitumia zinatokana na utaratibu tuliojiwekea na kujitengenezea sisi wenyewe, sio maagizo ya Mungu kusema kwamba tumeyatoa kwenye misaafu.
Hivyo Sitta, akiwa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la kuandika Katiba Mpya ya nchi yetu, anapojiona ana haki ya kuuchakachua utaratibu wote uliotokana na mapendekezo ya wananchi kwa vile eti utaratibu huo sio msaafu, anataka kutuonyesha nini? Kwamba Katiba itakayopatikana haitakuwa na ulazima wa kuheshimiwa kwa vile sio msaafu? Au kwa vile yeye kawa mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba tayari anajiona kageuka na kuwa na nguvu za Kimungu kiasi kwamba atakachokipitisha yeye tayari kitakuwa na baraka za Mungu kikiwa kama msaafu!
Hatahivyo yeye Sitta anadai kwamba yanayosemwa kuwa anakwenda kinyume cha utaratibu wa sheria iliyoanzisha mchakato wa Katiba Mpya yanasukumwa na chuki dhidi yake, sijui chuki gani! Kwa nini wananchi wamchukie kama angekuwa anafanya mambo kulingana na matakwa ya walio wengi? Na kwa nini wasimseme kama wanaona anayoyafanya yamelenga kukinufaisha kikundi cha wachache akiwa amewaweka walio wengi pembeni?
Niseme kwamba mawazo ya aina hiyo hayajaanzia kwa Sitta, tukiiangalia historia ya nchi mbalimbali duniani tutaona kwamba walikuwepo waliokuwa na mawazo kama hayo ya Sitta. Inabidi historia hiyo tuizingatie kusudi ituwezeshe kutorudia makosa.
Mfano mzuri ni wa nchi ya Afrika Kusin. Katika nchi hiyo iliandikwa Katiba mwaka 1902 ambayo haikuwahusisha wananchi walio wengi, ikaonekana ni Katiba ya upande mmoja wa watawala weupe. Pamoja na Katiba hiyo kudumu kwa karibu miaka 100, haikuzuia kuandikwa Katiba nyingine ya mpito mwaka 1993 iliyoweka mazingira ya usawa kwa watu wote wa nchi hiyo.
La kuzingatia ni kwamba kwa kipindi chote cha Katiba ya kwanza wananchi wa Afrika Kusini walilazimika kuishi bila amani wakati ilikuwa ni lazima Katiba inayowahusisha wananchi wote ipatikane. Si bora wangelipa kodi Januari wakaishi kwa amani kuliko kuishi kwa kujificha maporini lakini wakaja kukamatwa Disemba na kuilipa kodi pamoja na viboko juu! Huo ni usemi uliokuwa na hekima ya aina yake, “heri kulipa kodi Januari kuliko kulipa Disemba”.
Kama kweli mfano huo tunauelewa, kwamba kwa hali yoyote lazima ipatikane Katiba inayotokana na matakwa ya wananchi, hata kama itachelewa, kwa nini tukubali kufanya mambo ya kupoteza muda?
Kwa kulitilia hilo maanani, hatunabudi kujiuliza kwamba msimamo huo alionao mwanyekiti wa Bunge Maalumu, Samuel Sitta, ni wa kwake mwenyewe kadri mawazo yake yanavyomtuma au naye anapata shinikizo toka kwingine kuyafanya hayo?
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau