Bukobawadau

SAWAKA YAKABILIWANA CHANGAMOTO LUKUKI

SHIRIKA la Saidia Wazee Karagwe (SAWAKA), Mkoa wa Kagera, linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa huduma za afya, ushirikina, ukosefu wa vipato na kukosekana kwa mfuko wa jamii ya wazee.

Hayo yalisemwa jana mjini hapa na Mwanasheria wa shirika hilo, Ruthi Hole, wakati alipokuwa akiendesha semina iliyofanyika ukumbi wa Parokia ya Rwambaizi kuhusiana na sheria za ardhi na mirathi.

Hole, alisema wazee wanakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa huduma za afya, ushirikina, ukosefu wa vipato na kukosekana kwa mfuko wa jamii wa wazee, ambako kumesababisha maendeleo ya Taifa kurudi nyuma, ikiwa pamoja na wazee wengi kutojua sheria na taratibu ambazo zingeweza kuwasaidia kutatua matatizo.

Alisema tatizo kubwa ni wazee wengi kutojua kusoma na kuandika, ambako mara kwa mara vipato vyao vinapungua wakati wa kuuza mazao kwa kupewa fedha kidogo zisizostahili kwa mauzo hayo.
Alieleza kwamba wazee wengi wanakuwa na hali ngumu ya maisha kutokana na kutojishughulisha, ikiwa ni pamoja na vijana wao kushinda vijiweni kunywa pombe na utumiaji wa dawa za kulevya, hivyo kuwapa mzigo mkubwa wazazi wao kwa kuwategemea kwa mahitaji yao.

Aidha, alishauri kutokana na changamoto hizo, ni jukumu la jamii kuhakikisha wanakuwa na ushirikiano katika kuchukua uamuzi sahihi kutatua matatizo hayo na kuitaka serikali kuweka mikakati ya kuwashirikisha wazee katika bajeti kwa sababu inakosa takwimu nzuri ili kuweza kuwasaidia wazee hao.

Na Mbeki Mbeki Kagera
Next Post Previous Post
Bukobawadau