Bukobawadau

BUNGE MAALUM LA KATIBA LAAHIRISHWA LEO SEP 2,2014

Hatimaye Bunge Maalum la Katiba (BMK) limehitimisha kazi yake baada ya kupitisha Rasimu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano inayopendekezwa Bungeni humo baada ya kuipitisha kwa idadi inayohitajika kwa Sura zote 19 na Ibara zote 289.
Akitangaza matokeo hayo, Naibu Katibu wa BMK, Dkt Thomas Kashilillah, amesema pande zote mbili za Muungano zimeridhia kwa theluthi mbili (2/3) kwa mujibu wa kanuni za upatikanaji wa Katiba hiyo.

Idadi ya Wajumbe wote wa Tanzania Bara walipaswa wawe 411, Wajumbe wote waliopiga kura walikuwa 335. Wajumbe ambao hawakupiga kura walikuwa 76. Kura za ndiyo zilikuwa kati ya kura 331 na kura 334. Kura za hapana zilikuwa ni kati ya kura 1 na kura 3. Kura ya ushindi kwa kila ibara ilipaswa iwe kura 274.

Dkt. Kashililah alisema kuwa kwa upande wa wajumbe 154 kutoka Zanzibar waliopiga kura, wajumbe zaidi 146 walipiga kura ya 'ndiyo' kuunga mkono Rasimu ya Katiba inayopendekezwa na wajumbe 7 hadi 8 wakitaa kwa kupiga kura ya 'hapana' katika baadhi ya Sura na Ibara.

Jumla ya wajumbe wote wa BMK ni 629, ambapp 419 wanatoka Tanzania bara huku 210 wakitoka Zanzibar.

Mwenyekiti wa Bunge hilo, Mhe. Samuel Sitta akasema yafuatayo:
Waheshimiwa kwa mujibu wa Kanuni ya 38, kanuni ndogo ya 8, ninao wajibu wa kuwatangazia rasmi, tulichokipitisha. Baada ya Katibu kunisaidia kusoma matokeo, mimi Samuel Sitta, Mwenyekiti wa Bunge Maalum, sasa nathibitisha leo tarehe 2.10.2014 hapa Dodoma, Bunge Maalum kwa kura zinazostahili limepitisha Rasimu ya Katiba inayopendekezwa.

Zoezi hilo la upigaji kura ambalo lilianza Septemba 29 mpaka Oktoba 2, siku matokeo yalipotangazwa, lilisusiwa na wabunge wengi wa upinzani, kwa madai kuwa baadhi ya vipengele vya awali vilivyopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyopewa kazi ya kukusanya maoni kutoka kwa mwananchi, vilikuwa vimeondolewa.

Kabla ya kupitishwa kwa rasimu hiyo, bunge hilo maalum la katiba lilikaa kama kamati kujadili mapendekezo katika Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na tume hiyo ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya uongozi wa Jaji Joseph Warioba.

Baada ya kamati hizo za bunge hilo kutoa mapendekezo yao, kamati ya uandishi ilikuwa na jukumu la kuandika upya Ibara za Sura za Rasimu ya Katiba zilizojadiliwa na Bunge Maalum na hatimaye kutoa taarifa kwa Mwenyekiti baada ya kukamilisha kazi hiyo.

Hivyo, Kamati ya Uandishi ilikuwa na jukumu la kuhakikisha kuwa mapendekezo ya marekebisho, maboresho au mabadiliko katika Rasimu ya Katiba yanakidhi matakwa na masharti ya Kanuni za Bunge Maalum za Mwaka 2014.
Hatma ya katiba hiyo itahitimishwa kwa kura ya maoni inayotarajiwa kupigwa na wananchi.
Mhe. Sitta pia alilivunja rasmi Bunge hilo na kusema kuwa Rasimu inayopendekezwa itakabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein hapo tarehe 8 ya mwezi huu.

Next Post Previous Post
Bukobawadau