Bukobawadau

LEMA:VIJANA JIANDAENI KISAIKOLOJIA

MBUNGE wa Arusha Mjini, Godbless Lema, (CHADEMA), amesema Serikali ya Chama Cha Mapinduzi, (CCM), imeshindwa kutatua tatizo la ukosefu wa ajira kwa vijana nchini, hivyo akawataka vijana wanaohitimu elimu wajiandae kisaikolojia kukabiliana na tatizo hilo ambalo linazidi kuongezeka siku hadi siku.

Pia, alisema Serikali imeshindwa kuboresha mitaala ili elimu inayotolewa shuleni na vyuoni iwafanye wanaohitimu waweze kujiajiri badala ya kutumia muda mwingi wakizunguka na vyeti vyao mitaani kutafuta ajira, ambazo kimsingi hazipo na zikiwepo hutolewa kwa kujuana.

Lema, aliyasema hayo juzi alipokuwa akizungumza kwenye mahafali ya tatu ya Chuo Cha Tumaini Arusha, (ATC), ambako wanachuo 113
walihitimu kwenye fani za utalii, hotelia, ualimu, biashara, lugha za kimataifa na kompyuta.

Alisema kuwa ni vema vijana ambao wako shule na wale wanaohitimu, wajipange wakijua watafanya nini ili wajiingizie kipato na ikiwezekana wawaajiri wengine.

“Hapa nimeambiwa mmejengwa vizuri kitaaluma, sasa niwaombe jambo moja, ukitoka hapa usijielekeze kukimbilia kwenye makampuni makubwa kwa ajili ya kuajiriwa, amua mimi sasa najiajiri ili baadaye niwaajiri wenzangu,” alisema Lema.

Alisema kuwa, kuna matajiri wengine wanamiliki hoteli kubwa jijini hapa, si kwa kuwa wana elimu kubwa, bali waliamua kuwa wanajiajiri, wakaamini wanaweza, wakajituma kwa bidii kisha wakafanikiwa, hivyo nao wakiwa na nia hiyo watafanikiwa.

Kwa upande wake, mkuu wa chuo hicho, Ernest Mollel, alisema kuwa kwa sasa wanatafuta eneo ili waweze kukipanua chuo hicho, ambacho kwa sasa kiko kwenye jengo la Moleli jijini hapa.

Kwa upande wake, Diwani wa Levelos, Ephata Nanyaro, (CHADEMA),
eneo kilipo chuo hicho, alimpongeza Mollel kwa kuamua kuwekeza kwenye kutoa mafunzo ya kuwawezesha vijana kujiajiri.

Na  Grace Macha
Grace Macha
Next Post Previous Post
Bukobawadau