PRESS STATEMENT- KATIBA na TALKING HINTS ZA KATIBU MKUU CHADEMA, DK. SLAA
Talking hints za Katibu Mkuu kwenye
press conference Oktoba 16, 2014.
Kamati Kuu
ilikuwa na jumla ya agenda kumi na moja, mengine tutayatoa kwa umma kadri muda
unavyokwenda.
Kwa leo
tutazungumzia masuala mawili ambayo yana sura ya utekelezaji, tena wa muhimu na
haraka; Mchakato wa Katiba Mpya na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa;
Katiba;
Tunawataka
Watanzania wanaopenda nchi yao sasa waache kulia lia, waache kunung’unika
pekee, waache kulalamika. Tuingie kazini. Sasa ni wakati wa kuingia kazini.
Wenzetu tangu
siku ya kupokea rasimu ambapo Kikwete si kama rais wa nchi, bali kama
Mwenyekiti wa CCM alianza kuipigia chapuo debe Katiba Inayopendekezwa. Sasa
tuingie kazini…
Kikwete kama
mwenyekiti wa CCM akitumia kofia ya rais wa nchi, baada ya kupokea rasimu ameendelea
kuipigia chapuo, anawaambia wananchi wasome Katiba inayopendekezwa waelewe,
sisi tunamwambia aache kuwadanganya Watanzania. Katiba si sawa na novel kwamba
kila mtu anaweza kuisoma tu na kuelewa, ingelikuwa ni rahisi namna hiyo
tusingekuwa na haja ya kuwasomesha akina Lissu (Tundu).
Tunahitaji
wananchi wetu wasaidiwe tafsiri hasa ya katiba yenyewe na maana yake, hadi yale
mambo ya ndani kabisa. Ndiyo kazi ambayo CHADEMA tunaanza kuanzia kesho
kuzunguka nchi nzima, ambapo timu ya kwanza itaongozwa na BAWACHA. Ujumbe
utakuwa ni Katiba Mpya na Uchaguzi wa Serikali za Mitaa. Tunataka kuwafafanulia
Watanzania kwa kina.
Wakati bado
tunapigania Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka kesho,
moja ya ujumbe wetu kuanzia sasa ni kuwataka Watanzania kujiandaa kufurika
vituoni kujiandikisha kwenye daftari la wapiga kura wa uchaguzi wa Serikali za
Mitaa ambalo litaanza kuandikishwa siku 21 kabla ya uchaguzi wenyewe.
Watanzania
wafurike kwa wingi. Wajiandikishe. Kuiondoa CCM kunahitaji vitendo. Tuingie
kazini.
Kwa mtindo
huo huo wa kuingia kazini sasa kwa vitendo, tutatembea nchi nzima sasa kuwataka
wananchi kujitokeza kwa wingi sana siku ya Desemba 14, kupiga kura kuwachagua
viongozi wa Serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji…
Tunawaagiza
vile vile viongozi wetu katika ngazi zote za chama, kuanzia kanda, mikoa,
wilaya, majimbo, kata, matawi na hadi misingi kuwaongoza Watanzania wote; 1.
Kujiandikisha, 2. Kupiga kura na 3. Kusimamia taratibu za kikanuni…
Tumeshabaini
na kila Mtanzania sasa anajua kuwa kuwa Rais Kikwete si mtu wa kuaminika
tena…ni mtu anayebadilika badilika na wala haoni haja ya kuomba samahani…
Na sasa
tumezidi kubaini kuwa Kikwete amefikia mahali pa kugeuka kuwa procurement
officer na tumenasa nyaraka ambazo zinaonesha kuwa katika kujigeuza ofisa
manunuzi huko yanafanyika maandalizi ya kufanya mapambano na wananchi badala ya
kuandaa maridhiano.
Nyaraka…
Tumepata
taarifa za ziara yake ya kwenda China. Siwezi kusema atakwenda tarehe ngapi
maana mimi si kazi yangu kutangaza tarehe za ziara za Kikwete ambazo sasa hata
tumechoka kuhesabu maana zimeshakuwa nyingi mno zaidi ya 300+ ndani ya miaka
kumi.
Kilichotushtua
si Kikwete kwenda ziara, maana siku hizi wala si habari tena, kilichotushtua ni
hicho kinachompeleka huko China…ukimsikiliza Kikwete kwenye mazungumzo anapenda
kuonekana mtu anayeoenda amani, mshikamano lakini si kweli.
Amejigeuza
Ofisa Manunuzi. Kwa miezi kadhaa sasa kumekuwa na jitihada za kupata helkopta
tatu mpya…zingelikuwa ni kwa ajili ya Jeshi letu la Wananchi nisingekuwa na
shida, shida inakuja namna zinavyotafutwa. Zinatafutwa kwa utaratibu ule ule wa
kifisadi uliotumika kununua ndege ya rais wakati ule na hata rada.
Tena
anamtumia kampuni moja hivi ambayo tumekuwa tukiituhumu katika ufisadi. Sasa
sisi tunahoji, hivi ni kwa nini Serikali ya CCM inashindwa kwenda kiwandani na
kufanya order ya manunuzi kiwandani moja kwa moja hadi itumie taratibu za
kifisadi au mafisadi kufanya kazi hizi…
Kikwete
anajua kuwa ninajua. Maana ameshalalamika kwa watu wake wa vyombo vya dola kwamba
taarifa hizi zimefikaje kwa Dokta Slaa…
Wametumia
fedha zetu za mikopo kutoka Ujerumani…ndege zinanunuliwa Ufaransa…anatuma
fisadi kwenda kufanya manunuzi hayo badala ya Serikali…
Kinachoonekana
na taarifa na sisi hapa tunahoji je ni kweli ndege hizo zinataka kutumika kwa
manufaa ya CCM?
Rais pia
ameomba kwenda Beijing kufuatilia mitambo ya Police Surveillance
System…wanataka mitambo hiyo ifike hapa kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka
2015…ujumbe huu umeandikwa na mtu anaitwa Mbelwa…Kairuki. Waandishi wa habari
mtakuwa mnajua huko Wizara ya Mambo ya Nje. Anamwandikia Waziri wa Mambo ya
Nje…ujumbe huu umeandikwa tarehe 7/10/2014…
Sasa hizo
ndege anayotaka kununua iko mji mwingine huko China si ule aliopangiwa katika
ziara yake, sasa imeagizwa irushwe hadi pale atakapokuwa ili eti Rais mwenyewe
aweze kuiona…nimeangalia kwenye budget component hiyo kitu hakuna. Kwa kawaida
vitu vya kijeshi huwa havitajwi kwenye bajeti, lakini kwenye randamana ungeweza
kuona mpango wa kununua kitu kama hicho. Hakuna.
Sasa kinachoonekana
ni kwamba kwa sababu wamejua mwaka 2015 wanaondoka madarakani, wanaanza
kujiandaa kwa mapambano badala ya maridhiano.
Nataka
kumwambia Rais Kikwete kwamba nchi haiongozwi kwa misuli, haiongozwi kwa
kutunishiana misuli. Wanataka kufanya kama walivyofanya majuzi kutunga Katiba
Mpya kwa mitutu ya bunduki.
Sasa tena
uchaguzi unakaribia wanaanza maandalizi ya mitutu…tunamwambia Kikwete sisi
tutakuwa wa mwisho kuona nchi hii inaingia katika vurugu. Ndiyo maana ili
kuepusha mambo mabaya yasitokee kila taarifa kama hii tukiipata tutapiga
kelele. Silaha kubwa ya mnyonge ni kupiga kelele.
Katika
mwendo huo huo wa Rais Kikwete kugeuka kuwa Ofisa Manunuzi, sasa amejigeuza
kuwa Bwana TCRA, wanapanga kukutana na Kampuni ya HUAWEI ya China ili wanunue mtambo utakaowekwa ikulu kwa
ajili ya kunasa simu za akina Dokta Slaa…
Mitambo hiyo
inapelekwa ikulu badala ya…ingepelekwa Usalama wa Taifa ningeelewa, ingepelekwa
kwenye Jeshi letu ningeelewa, lakini ikulu? Tunasisitiza hatuna tatizo kama
mambo haya ya ndege, helkopta au mitambo ya mawasiliano yangekuwa yanafanywa
kwa ajili ya ulinzi na usalama wa nchi, lakini ni tatizo kubwa kama rais ndiye
anakuwa Ofisa wa Manunuzi au Ofisa wa Mawasiliano, TCRA.
Sasa
wanatafuta na kuhangaika kutafuta kila njia ya kubaki madarakani.
Tunamuonya
Rais Kikwete kuwa hizo pesa anazotaka kuchezea kwa yeye kuwa Ofisa Manunuzi si
za mfukoni mwake. Aache kuchezea fedha za Watanzania. Tulimuonya pia hivi hivi
wakati alipochezea fedha za Stimulus Package. Kama anataka kutukamata atukamate
lakini sisi tutasema. Haya ndiyo mambo ya madhara ya katiba inayopendekezwa
MAAZIMIO YA KAMATI KUU YA CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO KUHUSU MCHAKATO WA KATIBA NA KURA YA MAONI KUHUSU KATIBA INAYOPENDEKEZWA
Dar es Salaam,
Oktoba 16, 2014
UTANGULIZI
Kamati Kuu ya Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) imekutana katika kikao chake cha kawaida
na kujadili, pamoja na mambo mengine, mchakato wa Katiba Mpya. Kamati Kuu
imepata taarifa ya kina juu ya mchakato ulivyoendeshwa katika hatua mbali mbali
wakati wa kutungwa kwa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na marekebisho yake na,
baadaye, Sheria ya Kura ya Maoni.
Aidha, Kamati Kuu imepata taarifa ya mchakato
ulivyokuwa katika hatua ya kuundwa kwa Tume ya Mabadiliko, kukusanya maoni ya
wananchi na kuandaliwa kwa Rasimu ya Kwanza na ya Pili ya Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania.
Vile vile, Kamati
Kuu imepata na kujadili taarifa ya kina juu ya mchakato wa Katiba katika hatua
ya uteuzi wa Bunge Maalum na baadaye ndani ya Bunge hilo. Mwisho Kamati Kuu
imepata uchambuzi wa kina wa Katiba Inayopendekezwa iliyopitishwa na Bunge
Maalum tarehe 2 Oktoba, 2014.
Uchambuzi
huo utatolewa kwa vyombo vyote vya habari na kwa wananchi wa Tanzania kama
taarifa hapo baadae.
Baada ya mjadala
mrefu na wa kina, Kamati Kuu imeridhika kwamba mchakato wa Katiba katika hatua
zake zote ulitawaliwa na nia mbaya iliyokuwa na lengo kuu la kuhakikisha kwamba
hakuna mabadiliko yoyote ya maana yatakayofanyika kwenye mfumo wa kikatiba na
kiutawala ambao umekuwepo katika nchi yetu kwa zaidi ya miaka hamsini.
Ø Mchakato
wa kutunga Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ulitawaliwa na ubabe na usiri
uliohakikisha kwamba mchakato wa Katiba unadhibitiwa na Serikali na Chama cha
Mapinduzi;
Ø Uteuzi
wa wajumbe wa Bunge Maalum kutoka ‘Kundi la 201’ ulifanywa na Rais Jakaya
Kikwete kwa lengo la kuhakikisha wajumbe wengi zaidi wa Kundi hilo wanatoka CCM
na washirika wake. Kwa sababu hiyo, zaidi ya asilimia 82 ya wajumbe wa Bunge
Maalum kutoka Kundi la 201 walikuwa wanachama wa CCM waliochomekwa katika
makundi na taasisi mbali mbali;
Ø Sambamba
na idadi hiyo ya wajumbe wa Kundi la 201, asilimia 72 ya wajumbe wa Bunge
Maalum waliotokana na Kundi la Wabunge na Wawakilishi wa Zanzibar walikuwa
wanachama wa CCM;
Katika hatua ya
mjadala ndani ya Bunge Maalum, Kamati Kuu imeridhika kwamba mjadala huo
ulitawaliwa na ukiukwaji wa wazi wazi wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na
Kanuni za Kudumu za Bunge Maalum.
Ø Bunge
Maalum lilijigeuza ‘Tume’ na kuanza kukusanya upya maoni ya wananchi kuhusu
Katiba Mpya, wakati kazi ilikwisha kufanywa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba;
Ø Muda
wa kuwasilisha taarifa za Kamati mbali mbali ulifupishwa kutoka dakika sitini
hadi dakika ishirini na ule wa kuwasilisha maoni tofauti ulifupishwa kutoka
dakika thelathini hadi dakika kumi;
Ø Utaratibu
wa kupiga kura juu ya Katiba Inayopendekezwa kwa njia ya kifungu kwa kifungu uliondolewa
na badala yake kura zilipigwa kwa ujumla ya Sura za Rasimu, yaani kura
zilipigwa kwa Sura kumi za mwanzo na baadae kwa Sura tisa mwisho;
Ø Wajumbe
waliokuwa nje ya Ukumbi wa Bunge, au nje ya Dodoma na hata waliokuwa nje ya nchi
kwa sababu mbali mbali kama vile mahujaji na wagonjwa waliruhusiwa kupiga kura
ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa;
Ø Kura
za wajumbe waliopinga baadhi ya vifungu vya Katiba Inayopendekezwa na kukubali vifungu
vingine zilihesabiwa kuwa kura za kukubali Katiba Inayopendekezwa;
Katika
mazingira haya, mambo ya ajabu na yenye kuifedhehesha nchi yetu yaliyotokea ndani
ya Bunge Maalum yasingeacha kutokea.
Ø Wajumbe
Waislamu waliokwenda Makkah kuhiji na ambao uongozi wa Bunge Maalum ulieleza
mwanzoni kwamba wangepiga kura kwenye Ubalozi wa Tanzania nchini Saudi Arabia
hawakupiga kura Ubalozini na haijulikani walipigia wapi kura zao. Aidha, sasa
inajulikana kwamba Mahujaji hao – kama ni kweli walifanya hivyo - walipiga kura
siku moja kabla ya siku rasmi ya upigaji kura kwenye Bunge Maalum;
Ø Licha
ya Waheshimiwa Mohamed Raza na Salim Turky – wote wa kutoka Zanzibar - kuharibu
kura zao, kura hizo zilizoharibika zilihesabiwa kuwa kura halali za ‘Ndiyo’;
Ø Kura
za wajumbe waliokufa kama vile Marehemu Shida Salum zilihesabiwa kuwa kura halali
za ‘Ndiyo’;
Ø ‘Kura
za Maruhani’, yaani wajumbe wa UKAWA kutoka Zanzibar na za Wazanzibari wengine
waliojitoa na ambao hawajulikani majina yao hadi sasa zilihesabiwa kuwa kura halali
za ‘Ndiyo’;
Ø Mheshimiwa
Maulida Komu wa UKAWA ambaye alitajwa kwenye Gazeti la Serikali lililotangaza
majina ya wajumbe wa Bunge Maalum kuwa anatoka Zanzibar aligeuzwa na kuhesabika
kuwa anatoka Tanzania Bara, wakati Mheshimiwa Zakia Meghji wa CCM aliyetangazwa
kwenye Gazeti la Serikali kuwa anatokea Tanzania Bara alihesabika kuwa anatoka Zanzibar
na hivyo kupiga kura ya ‘Ndiyo’ kama Mzanzibari;
Ø Kura
za partly ‘Hapana’ na partly ‘Ndiyo’ zilizopigwa na wajumbe
wanne wa kutoka Zanzibar zilihesabika kuwa ni kura za ‘Ndiyo.’
Kamati Kuu
imeridhika kwamba, katika mazingira haya, theluthi mbili ya kura za Zanzibar
isingeacha kupatikana. Katika mazingira haya, na kwa kipimo chochote, Kamati
Kuu imeridhika kwamba upigaji kura ya kupitisha Katiba Inayopendekezwa ulikuwa
batili - na matokeo ya upigaji kura huo - yaani Katiba inayopendekezwa haiwezi
kuwa halali.
Na katika mazingira
haya, ujasiri unaostahili kupongezwa wa Mwanasheria wa Zanzibar, Othman Masoud
Othman, na wajumbe wengine nane wa Zanzibar waliopiga kura ya wazi ya ‘Hapana’
kuikataa Katiba Inayopendekezwa licha ya shinikizo kubwa, matusi na vitisho vya
kila aina, usingeweza kuzuia uharamia huu wa CCM.
Kwa hali hii,
Kamati Kuu inaungana na vyama vingine vya siasa vya UKAWA, taasisi kuu za
kidini nchini kama vile Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC), Baraza la Kikristo
Tanzania (CCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT), Shura ya
Maimamu, Baraza Kuu la Taasisi za Kiislamu, n.k. kulaani matukio yote
yaliyotokea wakati wa mchakato wa Katiba katika hatua zake zote hadi sasa. Kamati
Kuu inapondeza na kuunga mkono taasisi, mashirika na vyama vya siasa pamoja na
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba waliosusia tukio la Rais Kikwete
kukabidhiwa Katiba Inayopendekezwa siku ya tarehe 8 Oktoba, 2014.
Aidha, Kamati Kuu
inatoa rai kwa taasisi na mashirika yasiyokuwa ya kiraia ambayo tayari
yameshaonyesha msimamo wa kuiunga mkono Katiba Inayopendekezwa kujifikiria upya
na kujiridhisha kama mashirika yao hayatumiki kuhalalisha mambo haramu ambayo
yamefanywa na CCM na washirika wao katika mchakato huu.
Kamati Kuu
imeazimia kwamba CHADEMA itaungana na vyama na taasisi zilizotajwa hapa pamoja
na umma wa Watanzania wenye nia njema na taifa kuhakikisha kwamba wanashiriki
katika kampeni kubwa na ya nchini ili kuhakikisha kwamba Katiba Inayopendekezwa
inapigiwa kura ya ‘Hapana’ katika kura ya maoni, ambayo ni hatua ya mwisho ya
mchakato wa Katiba.
Katika hili, Kamati
Kuu inatoa rai kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuhakikisha kwamba inatekeleza
ahadi yake kwa Watanzania kwamba Daftari la Kudumu la Wapiga Kura litaboreshwa
kabla ya kufanyika kwa kura ya maoni ili kuhakikisha kwamba kila Mtanzania
mwenye haki ya kupiga kura anajiandikisha kwenye Daftari hilo na anapata haki
ya kushiriki katika maamuzi ya jambo hili muhimu kwa taifa letu.
Kamati Kuu
inawakumbusha Watanzania kujiandaa kutimiza wajibu wao wa kihistoria wa kukataa
uchakachuaji wa maoni yao uliofanywa na CCM na washirika wake katika Bunge
Maalum. Kukataa uchakachuaji huu kitakuwa ni kitendo cha kizalendo cha kila
Mtanzania. Kunyamazia au kuunga mkono uchakachuaji huu itakuwa ni kuisaliti
nchi yetu na kuendeleza utawala wa kikandamizaji na wa kifisadi ambao umekuwa
janga la taifa letu kwa miaka mingi.
-------------------------------------------------------
Dr.
Willibrod P. Slaa
KATIBU MKUU