Bukobawadau

“TWEYAMBE” NA MATUMAINI MAPYA KWA ZAO LA KAHAWA

Na Prudence Karugendo
BAADA ya kuteseka, kuhujumiwa, kufisidiwa, kutapeliwa nakadhalika, kwa muda mrefu, wakulima wa kahawa wa Kamachumu, Muleba, mkoani Kagera,  wameamua kuanzisha Umoja wa Wakulima wa Kahawa ambao wameupa jina la Tweyambe, au kwa kimombo “Tweyambe Coffee Growers Association”.
 “Tweyambe” ni neno la Kihaya lenye maana ya kujihimu  kwa pamoja, kuweka nguvu pamoja katika kujihangaikia na kujiondoa kwenye ufukara.
Umoja huo umetokana na wakulima hao wa kahawa kufanyiwa mambo machafu sana kwa muda mrefu na uongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika cha KCU (1990) Ltd. ambacho ndicho kinachoshughulikia zao la kahawa katika wilaya za Muleba, Misenye, Bukoba Mjini na Vijijini,  na wao kubaki wakikitegemea kuanzia kwenye vyama vyao cha msingi.
 
Wakulima hao wanasema kwamba mfumo wa ushirika, tangu unaanzishwa,  ulikuwa mzuri na wenye manufaa kwa wakulima hasa wa mazao ya biashara, lakini eti baada ya mfumo huo kuingiliwa na wajanja, au waliokuwa wakiuendesha ushirika kujanjaluka na kuyageuzia kwao manufaa yote ya ushirika, huku wakiwaacha wakulima wanafanya kazi ya kuwazalishia wao tu bila wakulima wenyewe kupata chochote, ushirika ukabaki kwenye mazoea tu bila kuwanufaisha wakulima kwa namna yoyote ile.
 
Wakulima wa Kamachumu wanatoa mfano kwamba walikuwa wakilitegemea zao la kahawa  liwawezeshe kukabiliana na matatizo mbalimbali ya kiuchumi, kama vile kusomesha watoto, kuwa na makazi bora, malazi bora, kupata huduma bora za kiafya nakadhalika. Lakini eti kwa sasa mambo yamegeuka na kuwa ya ovyo, hawawezi kulitegemea tena zao hilo liwaondolee matatizo ya kiuchumi. Hawawezi kuwapeleka watoto shule kwa kutegemea kahawa, hawezi kuwa na mawazo ya kujenga nyumba bora kwa kutegemea kahawa na mambo mengine mengi ambayo yamekwama kutokana na uchumi wao kuwa mbovu.
Eti wamefikia kiasi cha kuliona zao hilo la biashara kama mateso kwao, mateso ni pale wanapolazimika kuishughulikia  kahawa bila kuyaona manufaa yake.
 
Lakini eti pamoja na mambo kuwa hivyo hawawezi kusema kwamba sasa zao hilo limeisha thamani yake, eti thamani ya kahawa bado ni ileile ya tangu zamani. Tofauti wanayoiona ni ya namna viongozi wa ushirika wa sasa wanavyonona kuliko wale wa zamani, eti hiyo inawapa mawazo kuwa thamani ya kahawa kwa sasa inaishia kwa viongozi wa ushirika tu badala ya kumfikia mkulima.
 
Sababu eti kila anayechaguliwa kwenye uongozi au kuajiriwa kwenye ushirika akiwa mlalahoi, baada ya nusu mwaka anageuka na kuwa bwanyenye akiwacheka na kuwadharau wakulima wenzake ambao ndio waajiri wake! Eti bila kahawa kuwa na thamani,  kama inavyodaiwa kwa sasa,  hali isingekuwa hivyo na vi wachache wangeutamani uongozi katika ushirika.
 
Kwahiyo wakulima wa kahawa wa Kamachumu kupitia kwenye chama chao cha msingi wakajaribu kulionyesha tatizo hilo la thamani ya kahawa yao kuunufaisha tu uongozi wa ushirika, lakini uongozi wa chama kikuu ukatumia nguvu kubwa, nguvu inayotokana pesa ya wakulima wanaushirika, kuwanyamazisha wanaushirika hao wa Kamachumu.
 
Archard Felician Muhandiki ni mwakilishi wa Chama cha Msingi cha Kamachumu, kutokana na mtu huyo kuujali sana uwakilisha wakulima bila kutaka kuwasaliti kwa kujiunga upande wa uongozi  na kuwahujumu, akaonekana ni mtu hatari kwa ushirika anayepaswa kupigwa vita kwa kila namna!
 
Kwa maoni anasema, eti  jinsi inavyochukuliwa na ushirika kwa ujumla, kwa upande wa Kagera, ushirika maana yake ni pale kiongozi anapojinufaisha na jasho la wakulima anapopata fursa ya kufanya  hivyo. Eti mtu yeyote anayesita kuwahujumu wakulima wakati yuko kwenye nafasi ya uongozi katika ushirika, safu nzima ya uongozi wa ushirika inamchukulia kuwa si mwenzao na ikibidi inamzulia kashfa kuwa anauhatarisha ushirika!
 
Eti kuna wakati imesemwa kwamba yeye, Muhandiki,  haupendi ushirika, kisa hataki uongozi ufanye ufisadi kwa pesa za wakulima! Eti anayeonekana anaupenda ushirika ni yule aliye tayari kushirikiana na viongozi wenzake wa ushirika kuiba pesa za wakulima, huyo ndiye mpenzi wa ushirika kwa mtazamo wa viongozi wa ushirika waliojiweka wazi kwa ufisadi wa pesa za wakulima.
 
Kwahiyo Bwana Muhandiki naye hafichi chochote, anasema kama ushirika maana yake ni kuwaibia wakulima basi yeye haupendi ushirika wa aina hiyo. Na eti yuko tayari kulieleza hilo kwa kila mkulima kama ambavyo amekuwa akijitolea kutoka Dar es salaam, kwa usafiri wa ndege kwenda na kurudi Bukoba, kuhudhuria mikutano ya Chama Kikuu cha KCU (1990) Ltd..
Anasema malipo ya juu kwa kila mjumbe kuhudhuria vikao vya KCU (1990) Ltd. kwa mara moja ni shilingi laki tano,  wakati yeye anatumia mpaka shilingi milioni mbili zake mwenyewe kuhudhuria vikao hivyo. Lakini anasema hizo laki tano wanazopewa wajumbe wanaokwenda kwenye mkutano wa chama kikuu zinawatosha kuwasaliti wakulima wenzao wanaowawakilisha, eti kulingana na maisha ya kijijini yalivyo kwa sasa kwa wajumbe wengi hizo ni pesa  nyingi mno!
 
Ukweli huo ndio uliowafanya wanaushirika wa Chama cha Msingi Kamachumu kufanya uamuzi wa kuuondoa madarakani uongozi wa chama hicho lakini uongozi huo ukakingiwa kifua na uongozi wa Chama Kikuu,  kiasi cha KCU (1990) Ltd. kutumia pesa za wakulima kuweka wakili wa kuutetea mahakamani uongozi wa chama hicho cha msingi! Swali walilonalo wanaushirika wa Kamachumu ni la kwa nini wao  waushitaki uongozi wa chama chao cha msingi, kutokana na uovu unaoufanya dhidi ya wanachama,  lakini ujitokeze uongozi wa chama kikuu kuyajibu mashitaka hayo kwa kumweka wakili wakati hauhusiki na mashitaka hayo?
 
Baada ya kuona hivyo wanaushirika hao wakaamua kuachana na aina hiyo ya ushirika wa kuhujumiana na kuamua kuanzisha kitu kingine kabisa nje ya ushirika uliozoeleka, ilmradi kutafuta njia za kujinufaisha na zao lao la kahawa.
Chama kilichotangulia kufanya kitu cha aina hiyo,  kuukataa ufisadi unaofanywa na uongozi wa chama kikuu, ni Chma cha Msingi Magata, nacho cha wilayani Muleba, ambacho kwa sasa kinajitegemea baada ya kuitua chini KCU (1990) Ltd. iliyogeuka mzigo mzito usiobebeka.
 
Umoja unaopangwa kusajiliwa ni Tweyambe. Ni aina ya ushirika ambao wanasema wataulinda kwa makini ili usiingiliwe na virusi vya ufisadi. Wataweka ukomo wa uongozi ili kumwezesha kila mwenye uwezo wa kuongoza apate nafasi hiyo bila kulazimika kutoa rushwa.
 
Pia wanasema kwamba muundo wa uongozi wanaoutaka kwenye umoja wao sio kama ule wa chama kikuu cha ushirika, ambapo uongozi wa chama kikuu unatumia mapato yote ya chama na hata  pesa  ya kukopa kujinufaisha wenyewe,  wakati wakulima hawapati kitu. Wao wanataka kama kuna ziada itakayopatikana iwafikie wanaumoja wote.
 
Tweyambe wanapanga kuhakikisha kahawa yao inakuwa safi kiasi cha kuiwezesha kupata soko kirahisi na kuwarudishia faida kwa muda mfupi. Eti hawatahitaji kuwa na mlolongo wa viongozi watakaolazimika kula mapato yote yanayotokana na jasho lao kama ilivyo kwa chama kikuu cha ushirika.
 
Kitu kingine ni kwamba, hata kama waliotoa wazo hilo la kuwa na umoja wa Tweyambe ni watu wa Kamachumu, sio lazima kwamba umoja huo unapaswa uwe wa kwao peke yao. Eti wanawakaribisha wadau wote wa zao la kahawa katika mkoa wa Kagera kwenye umoja huo ili waunganishe nguvu zao pamoja dhidi ya ufisadi unaolikabili zao lao la kahawa mkoani humo.
 
Tweyambe wanasema kwamba ufisadi katika ushirika umetamalaki kote ambako ushirika umeweka mizizi. Eti kibaya zaidi ni Sheria ya Vyama vya Ushirika ambayo inaonekana kuulinda  huo kwa kutotaka wanaohujumu ushirika washitakiwe mahakamani. Eti haiwezekani mtu afanye wizi halafu umpelekee kesi ya wizi huo akaishughulikie yeye na kujiadhibu mwenyewe.
 Eti kwa kufanya hivyo sheria hiyo ni kama inaulea ufisadi ndani ya ushirika, kitu kinachoufanya ushirika usieleweke vizuri nini malengo yake. Kwamba kama malengo ya ushirika ni kuwainua na kuwaendeleza wakulima basi sheria ingekuwa wazi kwamba wanaokwenda kinyume na malengo hayo ya ushirika washitakiwe mara moja na ikibidi wafungwe au pamoja na kufilisiwa mali zao ili kujaribu kufidia jasho la wakulima.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau