Bukobawadau

YATIMA WAOMBA UFADHILI WA ELIMU

Na Ashura Jumapili
WATOTO yatima waliohitimu elimu ya awali katika shule ya Tegemeo Kagazi, wameiomba Serikali na taasisi mbalimbali kuwapatia ufadhili ili wajiunge na elimu ya msingi.
Meneja wa Kituo cha Tumaini letu, Kachocho Timanywa, alisema watoto hao wanakabiliwa na changamoto ya kukosa vifaa za shule ambavyo ni madaftari, kalamu, sare na mifuko   ya kubebea daftari.
Alizitaja changamoto nyingine ni msaada wa kadi za huduma ya jamii (CHIF), kutokana na mwaka huu kituo hicho   kumepoteza watoto saba waliofariki kutokana na ukosefu wa huduma za afya zinazosababishwa na kipato duni cha walezi.
Alisema kituo hicho kina upungufu wa fedha za mahitaji ya lishe, upungufu wa matundu ya choo, upungufu wa viti, meza za kusomea na zana za kufundishia kwa vitendo.
Timanywa alisema pia wanakabiliwa na changamoto ya kushindwa kuwahudumia watoto wenye ulemavu na gharama za kuendesha kambi.
Meneja Biashara Benki ya CRDB Tawi la Bukoba, Manase Mbaga, alisema jamii inatakiwa kuacha ukatili kwa watoto na badala yake kuwalea kwa moyo wa upendo ili wapate faraja.
Katika mahafali yaliyoambatana na harambee zaidi ya sh. milioni 2 zilipatikana huku ahadi zikiwa sh milioni 2.1.
Next Post Previous Post
Bukobawadau