KANALI MASSAWE ASHIRIKI UJENZI WA MAABARA WILAYANI ILI KUHAKIKISHA MAABARA ZOTE MKOANI KAGERA ZINAKAMILIKA IFIKAPO NOVEMBA 30, 2014
Katika hali isiyokuwa ya kawaida Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu
Fabian Massawe ameonyesha mfano kwa watendaji wa Halmashauri za Wilaya ya
Karagwe na Kyerwa kushirikiana kwa pamoja kusaidiana na wananchi kuhakikisha
vyumba vitatu vya maabara kila shule ya kata vinakamilika ifikapo Novemba 30,
2014
Mkuu huyo wa mkoa alionyesha
mfano wa kwa watendaji na wananchi kwa kushiriki kusomba matofali na kuamua kupanda juu ya vitanda kushiriki
ujenzi wa maabara katika shule ya
Sekondari Mukile katika Halmashauri ya wilaya ya Kyerwa wakati akikagua ujenzi
wa maabara katika Wilaya hizo..
Katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa wa Kagera aliwaonya
watendaji wa Halmashauri hizo mbili kuhakikisha wanasimamia ujenzi wa maabara unakamilika kwa tarehe iliyopangwa la sivyo watapoteza kazi zao kabla yeye Mkuu
wa Mkoa na Mkuu wa Wilaya kufukuzwa kazi na Rais Kikwete.
Aidha aliwaonya viongozi wa siasa
ambao ni madiwani, wenyeviti wa vijiji na vitongoji wanaozembea kuhamasisha wananchi kushiriki
katika uchangiaji wa ujenzi wa maabara kuwa wasipotimiza wajibu wao yeye Mkuu
wa mkoa atawashitaki kwa wananchi ifikapo wakati wa uchaguzi wa Serikali za
Mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ili wananchi wasiwachague tena.
Kasi ya Ujenzi
Katika wilaya za Karagwe na Kyerwa kuna kasi kubwa ya ujenzi wa vyumba
vya maabara tatu kila shule ambapo
ujenzi huo unaonekana ifikapo Novemba 30, 2014 watakuwa wamekamilisha vyumba
vyote vya maabara kwani ujenzi upo katika hatua mbalimbali hasa kuezeka na
hatua za linta.
Chanagamoto
Kutokana na wananchi kuhamasishwa kuchangia ujenzi wa maabara katika
wilaya hizo kumekuwepo na changamoto za baadhi ya viongozi wa kisiasa
kuhamasisha wananchi kugomea uchangiaji huo na kupelekea kuleta madhara kwa
baadhi ya watendaji kujeruhiwa na na wananchi wakolofi kwa kukatwa mapanga.
Katika kata ya Nyakatuntu Afisa
Mtendaji wa kata Bw. Simon Kagaruki alijeruhiwa na baadhi ya wananchi kwa
kukatwa panga la kichwani wakati akikusanya michango toka kwa wananchi katika
kijiji cha Kyerere kitongoji Omukishambya na kujeruhiwa vibaya sana.
Kanali Massawe aligiza vyombo vya ulinzi na
usalama kuhakikisha wanawakamata watuhumiwa walihusika na kitendo hicho na
kufikishwa mara moja katika mkono wa sheria. Aidha aliwaagiza watendaji wa Kata
na vijiji kutumia Polisi kwenye vijiji vikorofi wakati wakikusanya michango ili
kuthibiti amani na utulivu katika maeneo hayo.
Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe
inatarajia kumkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Kagera Maabara 57 katika shule 19 ifikapo
Novemba 30, 2014. Aidha Halmashauri ya Wilaya Kyerwa inatarajia kukamilisha
maabara 63 katika shule 21 za sekondari na kukabidhi mwishoni mwa mwezi huu.
Na; Sylvester Rapahel