Bukobawadau

UNDUGU NA UHESHIMIWA

Kuuacha undugu ni dalili za kuyakaribisha maangamizi
NA PRUDENCE KARUGENDO
YALIANZA  kama masihara, mwanzoni mwa kipindi cha kwanza cha awamu ya pili ya uongozi wa nchi yetu, wawakilishi wetu, wabunge, kwa kusukumwa na kitu ninachoweza kukiita ibilisi wa umimi, wakaona kwamba haifai wao kuendelea kuitwa ndugu. Kwa kutumia kinga waliyowekewa na Katiba ya nchi wakaamua wao waitwe waheshimiwa! Kwahiyo wakawa wamejitenga na wananchi wanaowawakilisha, wananchi wakabaki ni ndugu wao wakajipachika uheshimiwa!
Ikumbukwe neno ndugu lilibuniwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere mwaka 1975, katika harakati zake za kuilinda na kuidumisha tunu ya nchi ya umoja na mshikamano wa wananchi. Sababu tunapoongelea tunu za nchi ni lazima tuelewe kwamba undugu ndiyo tunu ya kwanza ambayo kila nchi inapaswa ijivunie. Bila undugu tunu zote zilizobaki ni kazi bure.
Hata kama nchi imejaaliwa kila aina ya utajiri lakini bila undugu wa kupendana, kuthaminiana na kuchukuliana kwamba kila mmoja ni sehemu ya mwingine, utajiri ilionao nchi ni lazima  ugeuke balaa linaloisukuma nchi husika kuelekea kwenye maangamizi huku ikionekana ina umasikini unaonuka. Hakuna umasikini unaokaribiana na wa watu kutafunana wao kwa wao,  kwa maana ya kuuana, kutokana na kukosa hisia za kiundugu.
Katika hilo mifano ni mingi, nje ya bara letu la Afrika kuna nchi zilizojaaliwa utajiri wa asili ikiwa ni pamoja na akili za kuutambua na kuutumia utajiri huo, tuichukulie nchi mojawapo ya Urusi. Nchi hiyo iliwahi kuwa moja ya nchi mbili tajiri na zenye nguvu sana duniani ikishindana na Marekani. Lakini Urusi ilipokumbwa na ibilisi wa uhasama na kuusahau undugu ulioifanya ikafikia hapo ilipokuwa, tunayaona yanayoitokea kwa sasa. Kila siku ni kutengana na kudundana wao kwa wao huku ikimwaga damu na kuonyesha umasikini uliopitiliza!
Katika Afrika kuna nchi kama Kongo DRC. Hiyo ni nchi iliyojaaliwa utajiri wa asili kuliko hata nchi nyingi za Ulaya zinazojidai ni za dunia ya kwanza. Lakini kukosekena kwa undugu katika nchi hiyo kumeifanya ionekane ni masikini kupita kiasi. Kwa sasa nchi hiyo imegeuzwa uwanja wa vita isiyoeleweka maana yake ni nini!
Kwa hapa kwetu Tanzania undugu alioubuni Nyerere ulilenga katika kuwaweka wananchi pamoja na kuwafanya waonane wao ni kitu kimoja, wachukuliane ni watu wa familia moja, ili akipata mmoja wajione wamepata wote, akikosa mmoja wajione wamekosa wote. Undugu uliowaondolea wananchi mikogo ya mmoja kumkoga mwingine kwa vile mmoja kapata na mwingine kakosa.
Katika hali hiyo haikuwa rahisi watu kuoneana husuda kitu ambacho kingeweza kusababisha pengo kati ya aliyenacho na asiyekuwanacho, pengo ambalo ni kiini cha kijicho na mwanzo wa chuki miongoni mwa wananchi. Kawaida chuki ndiyo huzaa uhasama na hatimaye ugomvi, vita, wananchi kuanza kupukutishana roho zao wao kwa wao.
Kinyume cha neno ndugu ni ubwana na utwana, bwana hakubali kuwa ndugu na mtwana, na mtwana hakubali kuendelea na hali hiyo ya unyonge muda wote, hali ya kuwa chini ilhali akimuona mwenzake yuko juu akimkandamiza. Kwa vyovyote vile atafanya kila njia kujinasua huko chini alikokandamizwa.
Na hatua hiyo haifanyiki kwa maelewano, sababu aliye juu akiufaidi ubwana anatamani abaki hukohuko wakati aliye chini akitamani naye kuja juu, hapo ni lazima chuki iwepo na matokeo yake ni mapambano na kumwaga damu. Mmoja akitafuta haki yake ya uhai na utu na mwingine akitaka kuipoteza kabisa haki hiyo ya mwenzake.
Baada ya Nyerere kuziangalia tofauti hizo na kuamua kubuni neno ndugu akiwa ameshawishiwa na falsafa ya kiongozi mmoja wa kidini, Askofu Marehemu Christopher Mwoleka wa Jimbo Katoliki la Rulenge, ya “Ili wawe na umoja”, uheshimiwa ulibaki tu kwa watoa haki waliopewa dhamana ya kuzitafsri sheria za nchi, mahakimu na majaji. Wengine wote tukaanza kujitambulisha kama ndugu. Dunia nzima ilituheshimu kwa uamuzi huo
Kimantiki, watafsiri hao wa sheria waliachwa waendelee kuwa waheshimiwa ili wapate fursa ya kuitekeleza kazi yao kwa ufasaha bila ya upendeleo wala kuoneana. Sababu katika undugu ingewawia vigumu kuitafsiri sheria jinsi ilivyo. Fikiria hakimu au jaji jinsi ambavyo angeweza kumwambia ndugu yake kuwa kakosea kwa mujibu wa sheria hivyo anatakiwa kutumikia kifungo kwa muda fulani. Kutokana na hilo hao wakaachwa waendelee kuwa waheshimiwa kusudi uamuzi wao uendelee kuheshimika bila kuonekana umeegemea upande wowote kutokana na kushawishiwa na neno ndugu.
Lakini kiajabu wawakilishi wetu, kiulevi tu, ulevi wa madaraka ya nafasi tulizowapa, kama alivywahi kusema Mwalimu, wakaamua nao waitwe waheshimiwa! Niliwahi kuhoji, kama wao wabunge au wawakilishi wanataka wawe waheshimiwa, je, sisi wananchi tuliowatuma tuwe kina nani?
Sababu kazi wanayoifanya wabunge tulipaswa tuifanye sisi wenyewe, lakini kutokana na uwezekano huo kuwa finyu sana ndipo ikaonekana tuwachague baadhi yetu wakatuwakilishe baada ya kuitenga nchi katika maeneo ya uwakilishi ambayo katika lugha nyingine yanaitwa majimbo. Sasa uheshimiwa wao uliowabagua wananchi unatoka wapi?
Ajabu ni kwamba baada ya wawakilishi wetu hao kukataa kuendelea kuitwa ndugu, watumishi wengine wa umma nao wakadandia hapohapo, nao wakaanza kujiita waheshimiwa! Madiwani nao wakajiita waheshimiwa, watendaji wa tarafa, wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa nakadhalika, wote wakataka waitwe waheshimiwa! Neno ndugu lililokuwa linatuweka karibu na kutufanya wamoja likafa kifo cha kulazimishwa! Ni baada ya wananchi nao kuacha kulitumia baada ya kuona limepoteza maana, wakaanza tena kuitana mabwana!
Baada ya undugu kuuawa nini kingine tukitarajie cha kutufanya tuendelee kuwa wamoja? Madhara ya kifo hicho cha undugu tumeanza kuyaona. Zamani tulipokuwa tunatofautiana kwa hoja tulitafuta muafaka kwa wepesi tukiamini kuwa sote ni ndugu. “Ndugu hapa umekosea, hatunabudi kufanya hivi na hivi”. Heshima iliwekwa mbele, pamoja na kuitana ndugu tulijali sana tofauti za kiumri na wadhifa alionao mtu katika jamii yetu.
Lakini kufuatia kifo cha neno ndugu, sasa kijana akitofautiana na mzima, hata mtu huyo awe ni mzee na mwenye wadhifa wa aina gani, kijana anaamua kumuwasha mzee vibao hata iwe kwenye kadamnasi! Rejea ya Makonda na Mzee Warioba. Huko ndiko tuliko kwa sasa, maadili yamepotea au kufa kabisa yakiwa yamesindikizana na neno ndugu, ni katika maangamizi.
Hatuna tena umoja, heshima wala adabu. Ni heri ya wanyamapori, sababu kimaumbile wanyama wanayo maadili yao ambayo hawawezi kuyakaidi hata mara moja.
Umimi  umeyabadili maadili katika jamii yetu. Mabadiliko haya tunayoyaona, binafsi,  siamini hata kidogo kama yamelenga katika kuinufaisha jamii yetu, ninachokiona ni kwamba yamelenga kuzinufaisha nafsi fulanifulani bila kujali jamii imekaaje katika upana wake. Ni kila mmoja kupigania nafsi yake na ikibidi kukipora kilicho cha jamii!
Mfano, haiwezekani kwamba mtu kuwa na akaunti ya “vijisenti” Ughaibuni ni kwa faida ya Watanzania wote, hiyo ni kwa faida yake binafsi na familia yake. Na si ajabu vijisenti hivyo vinavyofichwa Ughaibuni vikawa vimepatikana kiharamu kwa gharama ya roho za Watanzania wote, na hiyo ikawa ndiyo sababu ya vijisenti hivyo  kufichwa nje ya nchi.
Fikiria Watanzania wanakufa kwa kukosa vitu kama mahospitali na madawa ambavyo vingeyanusuru maisha yao kutokana na magonjwa yanayotibika, kisa hakuna pesa ya kufanya vitu hivyo vipatikane, pesa imekwapuliwa na kufichwa ughaibuni ikidaiwa ni vijisenti!
Sasa Katiba ya nchi inatengenezwa  katika muundo wa kuubariki ujambazi huo uliokusudia kuyateketeza maisha ya wananchi, wakati huohuo wahusika wanajiuliza kwa nini wasifanye hivyo wakati wao ni waheshimiwa na wananchi ni walalahoi, kwani wana undugu nao wakati neno ndugu lilishapotea?
Ila tukae tukielewa kwamba kwa kulipoteza neno ndugu katika kujitambulisha tumepoteza tunu nambari moja ya nchi yetu, tunu zilizobaki zote zitakuwa ni kazi bure kuzizingatia, kilichobaki ni maangamizi tu.
0784 989 512

Next Post Previous Post
Bukobawadau