Bukobawadau

Richmond iliondoka na Lowassa Escrow itamuachaje Pinda?

Na Prudence Karugendo
SAKATA  la wizi wa pesa za Akaunti ya Tegeta Escrow limefumua mambo mbalimbali na kuyaweka wazi pasipo wahusika kujua kuwa wanachokifanya kinatoa picha tofauti na waliyoikusudia.
Mojawapo ya vitu vilivyojiweka wazi ni kwamba nchi imeonyesha namna inavyoendeshwa kiuigizaji. Hiyo ni kutokana na mambo yanayoonyesha ni ya muhimu, na yanayotakiwa kuwa muhimu kweli kwa uendeshaji wa nchi  kutotiliwa maanani wala kuzingatiwa.
Mfano, nchi inaye Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), huyu anatambuliwa kikatiba na kisheria. Anachokiona na kukisema kwa upande huo kinatakiwa kiheshimiwe na kuzingatiwa. Vinginevyo nchi inaweza kujikuta imeangukia kwenye usemi wa “mali bila daftari hupotea bila habari”.
Lakini,  kimaigizo,  ripoti zake zinaonekana zimeanza kudhalilishwa na kukebehiwa na baadhi ya watu wasio na taaluma katika fani hiyo ya udhibi na ukaguzi! Na hata kama wanayo taaluma hiyo lakini hawako kwenye nafasi ya kuionyesha dhidi ya alichokifanya yeye CAG, kwa vile kimamlaka hawana sifa hiyo.
Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kafanya ukaguzi na kugundua kwamba pesa ya Akaunti ya Tegeta Escrow ni mali ya umma, akaonyesha kwamba pesa hiyo imechotwa kifisadi kwa njia za wizi na watu wanaojifanya kuwa pesa hiyo ni ya kwao.
Katika hilo naamini kabisa kwamba hakuna mtu mwingine wa kutuambia vinginevyo. Sababu aliyewekwa kikatiba kushughulikia suala hilo ni CAG, na si mwingine.
Kama hilo tunalitilia shaka ina maana gani ya kuendelea kuwa na nafasi hiyo ya CAG ambayo tunailipia kwa pesa za kodi zetu?
Sasa anapotokea profesa wa miamba, Sospeter Muhongo, tena aliyelazimisha ukaguzi wa CAG kufanyika kwenye eneo analoliongoza kutokana na utendaji wake wenye mashaka, akasema ripoti ya CAG siyo sahihi anadhamiria kuonyesha kitu gani? Kama profesa huyo haonyeshi kwamba nchi inaendeshwa kimaigizo ni kitu gani anatuonyesha?
Muhongo ni profesa wa miamba na Waziri wa Nishati na Madini, CAG ni mtaalamu wa ukaguzi na mahesabu na ni Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabau za Serikali, fani na nyadhifa mbili tofauti kabisa.  Kama CAG angekuwa mwalimu kama  Muhongo bilashaka naye angekuwa profesa katika fani yake kama alivyo Muhongo. Kwahiyo kwa nini neno profesa linamtia Muhongo kiburi na jeuri kiasi cha kuziona taaluma na nyadhifa nyingine ni za ovyo na ana uwezo wa kuziingilia namna atakavyo yeye?
Suala lililopo kwa sasa ni wizi wa pesa za umma. Muhongo anaonekana kuubariki wizi huo kwa madai ya kwamba pesa hizo siyo za umma, lakini ukaguzi umefanyika na kubainisha kuwa pesa hizo ni za umma. Hatahivyo Muhongo bado anasisitiza kuwa sio pesa za umma!
Tumueleweje Muhongo? Au kwa vile ni profesa hataki kukaguliwa kama utaratibu ulivyo? Uprofesa wa miamba unamfanya azidharau taaluma za watu wengine! Hili lingekuwa ni suala linalohusiana na miamba nisingekuwa namshangaa hata kidogo, sababu angekuwa yuko jikoni kwake. Lakini sivyo ilivyo, hili ni suala la mahesabu na wataalamu wa kazi hiyo wapo.
Maigizo mengine yamejionyesha kwa baadhi ya wabunge kuikebehi ripoti na maoni ya PAC chini ya uenyekiti wa Zitto Kabwe. Hiki ni chombo cha Bunge ambacho kinapaswa kuakisi mwonekano wa Bunge zima. Sasa wanapotokea baadhi ya wabunge wakaonekana wanakinzana nacho tuwaeleweje? Ina maana hao wana Bunge lao tofauti na hili la kwetu au wanataka tu kutuaminisha kuwa wanafanya maigizo?
Ikumbukwe kwamba Kamati hiyo ya PAC ndiyo inayochunguza na kutoa maamuzi kwa niaba ya Bunge kwa upande wa Hesabu za Seerikali.
Katika suala hili la Tegeta Escrow Account Kamati hiyo haikutoa mapendekezo yake kulingana na inavyopendelea yenyewe, isipokuwa mapendekezo yake yametokana na ripoti ya CAG ambayo imechambua ukweli na kuuweka wazi.
 
Ni ripoti hiyo iliyoifanya PAC ipendekeze ni nini cha kufanya kufuatia ukweli huo ulioonyeshwa na CAG. Lakini sio lazima mapendekezo ya PAC yafanane na ya CAG neno kwa neno. Sababu CAG katoa ripoti ya ukaguzi wa alichokigundua na kukiona na baadaye kulikabithi Bunge. Bunge nalo kupitia kwenye Kamati yake ya kudumu (PAC) likatoa hukumu. Baada ya hapo kilichoendelea ni kama maigizo ya kutaka kuipindua hukumu hiyo, yaani kulivua Bunge dhima yake ya kuisimamia serikali.
Kingine kinachodhihirisha maigizo yanayofanyika Bungeni ni baadhi ya wabunge kuchangia kwenye suala la wizi wa pesa za “Tegeta Escrow Account”  bila kukielewa wanachokichangia.  Sababu wapo wanaouliza ni sababu gani PAC imependekeza waziri mkuu, Mizengo Pinda, awajibike. Hao wanaoonyesha kwamba nafasi ya waziri mkuu inamfanya aliyeikalia abaki kama sanamu tu lisiloweza kuhangaika kushughulikia yaliyo chini yake!
Nadhani kumtetea waziri mkuu kwa namna hiyo ni kumtukana na kumdhalilisha, waziri mkuu sio sanamu. Yeye ni msimamizi wa shughuli za kila siku za serikali. Kwahiyo hakuna namna yoyote ambayo madudu ya kuwaumiza wananchi yanaweza yakafanyika ndani ya serikali yeye akaruka kwa madai ya kwamba hayatambui wala hahusiki.
Mambo yote yanayofanyika chini yake, awe anayajua au hayajui, moja kwa moja yanamgusa yeye na ndiye mwenye kuwajibika. Huo ndio usimamizi kwa maana halisi, vinginevyo hatuna sababu ya kuwa na nafasi hiyo ya waziri mkuu.
Ikumbukwe waziri mkuu aliyemtangulia Pinda, Edward Lowassa, aliwajibika katika mazingira yanayofanana fanana na haya aliyomo waziri mkuu wa sasa, Pinda. Sasa kama mazingira ni yaleyale, inawezekanaje yawe haramu kwa Lowassa lakini kwa Pinda yawe halali?
Hatahivyo ukubwa wa kashfa iliyomfanya Lowassa kuwajibika, kimuonekano, haufikii hata nusu ya ukubwa wa kashfa ambayo Pinda kang’ang’ana nayo na kuona kuwajibika ni kitu ambacho hakiwezekani kwake! Hilo linathibitishwa na yaliyotokea Bungeni ambapo kikao cha Bunge kimevunja rekodi tangu nchi yetu ijitawale,  ya kuendeshwa hadi saa tano usiku suala likiwa, pamoja na mambo mengine, kujaribu kumnusuru waziri mkuu asiwajike.
Suala la waziri mkuu kuwajibika inabidi tulitazame kwa kuziangalia nchi kama India, Japan na nyingine za aina hiyo ambako jambo la waziri mkuu kuwajibika kwa kujiuzulu,  hata kama ni baada ya kukaa madarakani kwa wiki moja tu kutokana na mambo kwenda mrama chini yake,  ni jambo la kawaida kabisa.
Bilashaka hiyo ni moja ya mambo yanayozifanya nchi hizo ziwe mbele yetu kwa mbali kiuchumi. Lakini sisi tunamng’ang’ania waziri mkuu ambaye kila kukicha kunatokea madudu chini yake yenye muonekano wa kuuteketeza uchumi wa nchi na kuwatia wananchi mashakani! Hiyo nini maana yake? Tuseme kwamba tunaupenda sana ufukara?
Kwa vyovyote vile Pinda anapaswa awajibike kama kweli anaipenda nchi yake na kuwathamini wananchi wenzake. Mbali na hiyo itaonekana hata uwaziri mkuu wa Pinda nacho ni cheo cha maigizo kama niliyoyataja hapo juu. Sababu cheo chenye dhamana ya kuwatumikia wananchi kisicho na kuwajibika hakionyeshi kinawezaje kuwahakikishia wananchi kuwa kina manufaa kwao. Mtu ambaye hayuko tayari kuwajibika kwa vyovyote vile hawezi kuwahakikishia wananchi kuwa atawalinda.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau