Bukobawadau

TAARIFA MAALUM KUHUSU KAMPUNI YA NDEGE YA TANZANIA (ATCL)

Zitto Kabwe
Mheshimiwa Spika, Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) ilianzishwa mwezi Novemba 2002 baada ya Serikali kubinafsisha lililokuwa Shirika la Ndege la Tanzania (Air Tanzania Corporation, ATC); katika Shirika hilo, Shirika la Ndege la Afrika Kusini (SAA) lilinunua hisa asilimia 49 ndani ya ATC. Hata hivyo ubia kati ya ATCL na SAA ulikabiliwa na matatizo ya kiuendeshaji na kulazimika kusitishwa mwezi Agosti 2006 na ATCL kurejeshwa tena Serikalini kwa asilimia 100.
2.8.1 Hali halisi ya ATCL kwa sasa
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Taarifa ya Msajili wa Hazina kwa mwaka wa fedha unaoishia Juni 30, 2013 na kwa kuzingatia Taarifa ya Wizara ya Uchukuzi, imebainika kuwa ATCL kwa sasa ina Ndege moja tu aina ya Dash 8 – Q 300, Wafanyakazi 142 na Jengo la ATC House lililoko mtaa wa Ohio, Dar es Salaam huku ikiwa na madeni makubwa kama itakavyofafanuliwa hapo baadae.
2.8.2 ATCL imefikaje hapo ilipo kifedha na kuwa na Madeni makubwa?
Mheshimiwa Spika, baada ya kuvunjika kwa mkataba wa ubia baina ya SAA ana ATC, mnamo mwezi Machi 2008, Wizara ya Miundombinu kwa wakati huo iliingia katika makubaliano na Kampuni ya China Sonangol kuwa Kampuni hiyo ya China ingeleta ndege mpya 7 kwa ATCL ikiwamo Ndege 5 aina ya Airbus ambazo zingewasili mwaka 2012 na 2013.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Msajili wa Hazina na Uongozi wa Wizara ya Uchukuzi, Wakati ATCL ikisubiri ndege hizo mpya, Kampuni ya China Sonangol iliitambulisha Kampuni ya Wallis Trading Inc kwa ATCL na kisha Kampuni hizi mbili (Wallis Trading Inc na ATCL) zikaingia mkataba wa Ukodishaji ndege aina ya Airbus 320 kwa kipindi cha miaka 6 kwa Malipo ya USD 370,000 kila mwezi.
Mheshimiwa Spika, huu ndio ulikuwa mwanzo wa mwisho wa ATCL, kwani baada ya Ndege hiyo kuwasili ilifanya kazi kwa muda wa miezi sita tu na baadae ilifungiwa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kwa kushindwa kutekeleza matakwa ya usafiri wa anga. Ndege hiyo ilipelekwa kwa matengenezo makubwa mwezi Julai, 2009 nchini Ufaransa na haijawahi kurudi hadi leo wakati ambapo Serikali kama mdhamini wa ATCL anadaiwa fedha nyingi na Kampuni ya Wallis.
Mheshimiwa Spika, kutokana na deni la ATCL kwa Wallis linalofikia USD 42,459,316.12 hadi tarehe 31 Oktoba, 2011 na kufuatia majadiliano mbalimbali baina ya Serikali na Kampuni hiyo, Serikali imekwishalipa jumla ya USD 26,115,428.75 hadi sasa wakati bakaa inayodaiwa ni USD 23,996,327.82.
Mheshimiwa Spika, Kamati inasikitishwa sana na upotevu huu wa fedha za Umma ambao umetokana na mkataba mbovu ulioingiwa na watumishi wa Umma wasiokuwa waaminifu na uchungu na Taifa lao. Mabilioni ya fedha yanaoendelea kulipwa kwa Kampuni ya Wallis kwa huduma ya ndege iliyofanya kazi hapa nchini kwa miezi sita tu na kisha ndege hiyo kupelekwa Ufaransa kwa matengenezo ni fedheha kubwa kwa wazalendo wa Taifa letu. Aidha, Taarifa zinasema ndege hiyo ikiwa Ufaransa ilipakwa rangi na kukodishwa kwa Shirika la ndege la nchi ya Guinea wakati Serikali yetu ikiendelea kulipia tozo ya ukodishaji wa ndege husika.
Mheshimiwa Spika, ni wakati sasa kwa Serikali kuamua kwa dhati kushughulikia suala la ATCL kwa mapana yake ikiwa ni pamoja na kuangalia uhalali wa kulipa deni la Wallis (ambalo lipo chini ya dhamana ya Serikali, hivyo ni fedha za Umma) ambaye kimsingi naye alikiuka makubaliano ya Mkataba kwa kukodisha ndege iliyokuwa imekodishwa tayari kwa ATCL. Aidha, ni muhimu wahusika wa uingiaji wa mkataba husika wakafikishwa kwenye vyombo vya sheria ili haki itendeke.
Mapendekezo kuhusu deni la USD 23,996,327.82 ambalo ATCL inadaiwa na Wallis Trading Inc.
KWA KUWA, Serikali haikunufaika na mkataba wa kukodisha ndege aina ya Airbus kutoka kwa Kampuni ya Wallis baada ya ndege hiyo kugundulika ni mbovu ndani ya miezi sita na kupelekwa kutengenezwa kwa muda mrefu,
NA KWA KUWA, Serikali inaendelea kulipa tozo ya ukodishaji wa ndege hiyo ambayo haifanyika kazi,
HIVYO BASI, Kamati inapendekeza yafuatayo;
a) Serikali kuangalia uhalali wa kulipa deni la Wallis ambaye kimsingi naye alikiuka makubaliano ya Mkataba kwa kukodisha ndege iliyokuwa imekodishwa tayari kwa ATCL.
b) Serikali ihakikishe inawafikisha kwenye vyombo vya Sheria ili haki itendeke kwa wahusika wa uingiaji wa mkataba huo unaoendelea kuipa hasara Serikali kwani hadi sasa hakuna kesi iliyopelekwa mahakamani mahususi kwa waliongia mkataba husika
Next Post Previous Post
Bukobawadau