Bukobawadau

MAKONDA AAPISHWA RASMI

Dar es Salaam. Licha ya baadhi ya watu kubeza uteuzi wake, Mkuu  wa Wilaya ya Kinondoni Paul Makonda ameapishwa leo jijini Dar es Salaam na kusema kuwa atatekeleza majukumu yake kwa mtindo alioupa jina la STK, akimaanisha atafuata Sheria, Taratibu na Kanuni.
Huku akiwa ameambatana na mkewe, Makonda amesema kazi yake ni kumsaidia kazi Rais Jakaya Kikwete tu si mtu mwingine, kusisitiza kuwa hakuwahi kufikiria kuwa kuna siku atateuliwa kuwa mkuu wa wilaya.
Wakati Makonda akieleza hayo,  Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki ametaja sababu nne zilizomfanya Rais Kikwete kumteua mkuu huyo wa mkoa na kusisitiza kuwa kwa kazi alizokwisha fanya, alistahili kuteuliwa muda mrefu.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye ni Katibu wa Chipukizi na Uhamasishaji wa UVCCM aliapishwa jana katika ofisi za Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, kabla ya kuanza kwa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya mkoa huo. Baada ya kuapishwa aliingia katika kikao hicho akielezwa kuwa ameshakuwa mjumbe rasmi.
Makonda ni kati ya wakuu wa wilaya wapya 27 walioteuliwa na Rais Kikwete takribani wiki moja iliyopita. Mbali na uteuzi huo, rais Kikwete aliteungua uteuzi wa wakuu wa wilaya 12 na kuwabadilisha vituo vya kazi wengine 64.
Akizungumza mara baada ya kuapishwa Makonda amesema, “Namshukuru Mungu kwa kumpa Rais Kikwete macho ya kuniona na hatimaye kuniteua kuwa mkuu wa wilaya.”
Amesema, “Aliniona nafaa ndiyo maana alifanya hivyo. Sikuwahi kufikiria kama kuna siku nitateuliwa kuwa mkuu wa wilaya.”
Akieleza mambo mawili muhimu atakayoyafanya alisema, “Kwanza, nafasi niliyopewa ni mpya na ni tofauti na ile ya ubunge. Mbunge anachaguliwa na wananchi ila hii yangu ni ya kuteuliwa. Nimepewa nafasi hii kumsaidia kazi Rais Kikwete si mtu mwingine. Nitafanya kile ambacho kinatakiwa kufanywa na mkuu wa wilaya.”
Akieleza jambo la pili alisema, “Nitafanya kazi kwa mtindo wa STK; yaani nitafuata sheria, taratibu na kanuni. Ninafungua milango kwa watu wote, wakiwemo wananchi wa wilaya ya Kinondoni.”
Kabla ya kuanza kutaja sifa nne za Makonda, Said Meck Sadiki alisema, “Mengi yamesemwa baada ya rais kukuteua. Ila kwa jinsi ninavyokufahamu ulitakiwa kuwa mkuu wa wilaya kabla ya uteuzi huu." 
Amesema sifa ya kwanza ya Makonda ni uongozi alionao ndani ya UVCCM, kwamba alipewa kwa sababu ni mtendaji kazi hodari na pia umemfanya awe na uzoefu.
“Pili, Makonda ni msomi mzuri sana katika hilo hakuna mwenye shaka kabisa. Tatu, umekuwa mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba. Huwezi kuteuliwa kuwa mjumbe wa Bunge hili kama hauna uwezo, watu walikupima na kukuona kuwa uko vizuri na una uwezo mzuri tu,” amesema.

Amesema sifa ya nne ya mkuu huyo wa wilaya ni uongozi aliokuwa nao akiwa anasoma chuoni, “Miaka ya nyuma umewahi kuwa rais wa Vyuo Vikuu. Wasomi hawawezi kukupa nafasi ya kuwaongoza hivi hivi tu. Ni wazi kuwa walitambua utendaji kazi wao mzuri.”
Sadiki amesema Makonda ana sifa nyingi zaidi ya hizo, kumtaka ahakikishe anatekeleza na kusimamia ilani ya CCM na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Wanasema mzigo mzito mpe mnyamwezi akubebebe. Wewe ndiyo mnyamwezi wa wilaya ya Kinondoni. Pamoja na yote simamia haki za wananchi na hakikisha wanazipata, tena bila kujali kabila, itikadi, dini wala rangi zao,” alisema Sadiki.
MWANANCHI
Next Post Previous Post
Bukobawadau