Bukobawadau

DIAMOND PLATNUMZ NI KIOO CHA WASANII KATIKA JAMII YETU

NA PRUDENCE KARUGENDO
MKOA  wa Kigoma ni hazina kubwa ya vipaji hapa nchini Tanzania. Tangu zamani kulishuhudiwa vipaji vingi toka mkoani humo hasa vya wanamichezo na wasanii. Mfano kwa upande wa kandanda tutaona kwamba mkoa huo ulitingisha sana kwa vipaji vya wanasoka.
Kina Manara, Kitwana Manara, Sunday Manara, Kassim Manara na ndugu zao wengine wanatoka Kigoma. Baadaye kikafuatia kizazi cha kina Edbili Lunyamilla, Nteze John, Omari Mavumbi, Itutu Kigi na wengineo wengi.
Kwa upande wa wasanii wa muziki Kigoma imetoa watu wengi wenye majina makubwa katika sanaa hiyo,  kama Shem Kalenga, Hassan Rehan Bitchuka, Marijani Rajabu, Zahir Ally Zorro, Banana Zorro, Wema Abdallah, Nyota Waziri na wengineo wengi.
Kwa upande wa muziki wa kizazi kipya Kigoma imefanya kufuru. Imetoa vijana wengi wa muziki huo wakiongozwa na mtaalamu wa muziki, kwa maana ya kutunga, kuimba, kucheza kila ala ya muziki na kutengeneza muziki, Emmanuel Bizimana Ntavyo, maarufu kimziki kama Bizman. Vilevile wapo wengine wengi wa muziki wa kizazi kipya, kama kina Ally Kiba, Banana Zorro, Jacqueline Ntuyabaliwe, maarufu kama K-Lynn na wengine wengi.
Lakini pamoja na wote hao makala hii ni mahususi kwa moja ya vipaji hivyo vya mkoa wa Kigoma ikiwa imemlenga chiriku wa muziki wa kizazi kipya kwa sasa hapa nchini, Nassibu Abdul, maarufu kama Diamond Platnumz.
Diamond kadhihirisha kipaji cha sanaa ya muziki kutokana na mafanikio aliyoyapata kwa kipindi cha muda mfupi alioutumia katika sanaa hiyo. Naweza kusema kwamba ni kipindi kisichozidi miaka mitatu. Hiyo ni tofauti na kipindi alichokitumia mfalme wa muzuki wa pop duniani, Michael Jackson, kuwa kileleni mwa mafanikio. Michael Jackson alitumia zaidi ya miaka kumi kufika kileleni, kati ya 1967 – 1979.
Lakini ndani ya miaka mitatu Diamond ameweza kuibeba Tanzania na kuiweka kwenye chati ya kimataifa kwenye fani hiyo ya muziki wa kizazi kipya. Na ninaposema ngazi ya kimataifa sina maana ya kuvuka tu mipaka ya nchi na kuingia nchi za jirani kama Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zambia, Malawi, Msumbiji wala Kongo, kama ambavyo wameweza kufanya wasanii wengine wa muziki huo wa hapa nchini, ninamaanisha kimataifa kwa maana halisi. Nalenga nchi za mbali na Tanzania.
Muziki wa Diamond kwa sasa unapigwa kwenye nchi mbalimbali za Afrika kuanzia Afrika Kusini, Afrika ya Kati, Mashariki na Afrika Magharibi, ukiondoa nchi za Kiarabu kwa upande wa Afrika Kaskazini, ambako sina uhakika kama muziki wa kizazi kipya una mashabiki kulingana na utamaduni wa Kiarabu ulivyo.
Kwa maana hiyo Diamond kaiweka Tanzania kwenye chati ya kimataifa kwa maana halisi kimuziki. Kwa  sasa msanii huyo anakula sahani moja na wasanii wa kimataifa kama kina Peter Okoye na Paul Okoye, Wanigeria wanaounda kikundi cha P Square, ambao mara kadhaa wamemuomba watoe naye vibao vya pamoja. Pia yuko kwenye kiwango cha wanamuziki kama Youssou N’Ndour wa Senegal na wengine wa aina hiyo.
Kwa eneo hili la Afrika Mashariki, nashindwa kumtofautisha Diamond na mwanamuziki wa Uganda, Joseph Mayanja, maarufu kama Chameleone. Kwa sasa wanamuzi hao wanafanana kwa kwa mambo kadhaa nitakayoyajadili hapa chini.
Tanzania iliwahi kuvuma sana duniani miaka ya nyuma kupitia kwa wanamichezo, hususan wanariadha, kina Filbert Bayi, aliyewahi kuwa bingwa wa mbio za mita 1500 duniani, ambaye mpaka sasa anashikilia rekodi ya mbio hizo kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola aliyoiweka mjini Christchurch nchini New Zealand mwaka 1974. Wengine ni Seleman Nyambui, Adventina Mtakyawa, Juma Ikangaa, Gidmas Shahanga na wengine wengi.
Lakini kutokana na umri kuwatupa mkono nyota hao,  jina la Tanzania limefifia katika tasinia ya michezo na kuifanya nchi yetu isahaulike kabisa kana kwamba haipo kwenye nyanja ya michezo na burdani!
Hivyo Diamond ni kijana aliyedhamiria kulipandisha tena jina la nchi yake kupitia tasinia ya burdani. Na niseme kwa uhakika kabisa kwamba ameweza. Hilo linashadidiwa na tuzo mbalimbali za kimataifa anazozipata kwa sasa kwa upande huo wa burdani baada ya kushindanishwa na wasanii wengine wa kimataifa toka nchi mbalimbali.
Kitu cha kipekee nilichokigundua kwa Diamond na kuhisi kwamba pengine ndicho kinachochochea mafanikio yake ni tabia yake ya kusikiliza ushauri na kuufanyia kazi.
Wakati fulani nilimpa changamoto, ambayo vilevile niliwahi kuitoa kwa Joseph Mayanja (Chameleone) wa Uganda nilipokutana naye Jijini Mwanza, Mei mwaka jana, kwamba kwa kiwango alichopo hapaswi kuendelea kuimba muziki kwa kutumia mtindo wa “play back”, kwa maana ya kuimba kwa kufuatiza muziki uliorekeodiwa tayari,  kwamba anatakiwa kuwa na vyombo vyake na kupiga muziki wa moja kwamoja pasipo kutumia CD. Diamond kanielewa na kusema kwamba hilo analifanyia kazi kwa bidii kubwa.
Kitu kingine ni namna anavyoendesha mahusiano na jamii aliyomo. Kawaida kuna dhana ya kwamba wasanii ni watu wasioeleweka vizuri ndani ya jamii, wahuni, na huo kuwa mwanzo wa neno usanii, kwamba fulani kanifanyia usanii ikiwa na maana ya kanifanyia uhuni.
Lakini hilo ni tofauti kabisa kwa Diamond. Yeye anapenda sana kuwasaidia wenye mahitaji kulingana na hali halisi ilivyo. Kipindi fulani kwa mfano, kwa kuuthamini mchango wa Baba wa Muziki hapa nchini, Marehemu Muhidini Mwalimu Gurumo, aliamua kumpatia msaada wa gari jipya. Huo ni usanii kwa upande wa pili anaouonyesha Diamond tofauti na upande uliozoeleka kwa jamii.
Diamond anasema kwamba amejipangia kila mwezi kuwa anatembelea vituo vya watoto yatima na kutoa misaada mbalimbali kadri inavyowezekana. Huo ni mchango mwingine katika jamii anaoufanya kijana huyo.
Anawashauri vijana wenzake, hasa wasanii, wanaojiingiza kwenye ulevi uliopindukia pamoja na matumizi ya madawa ya kulevya waache mambo hayo mara moja. Anasema kwamba mambo hayo yanaharibu vipaji na wakati mwingine kusababisha kupoteza maisha. Anasema ili kukilinda kipaji chake yeye anahakikisha anaepukana na mambo hayo yasiyo na maana na yaliyo hatari kwa maisha ya binadamu.
Diamond anasema kwamba alizaliwa Septemba 22, 1990, Kigoma, na kwamba kabila lake ni Mmanyema.
Anasema kwamba kilichomfanya aingie kwenye muziki ni kipaji chake kilichojitokeza tangu akiwa shule ya msingi. Eti alikuwa akipendelea kuimba kwenye kwaya ya shule na burdani nyingine za shuleni.
Huyo ndiye Nassibu Abdul, au ukipenda Diamond Platnumz, ambaye wasanii wengine vijana wanapaswa wamtumie kama kipimo ya mafanikio katika usanii huo wa muziki wa kizazi kipya wanaoufanya. Bilashaka watakaofuata mwenendo wake watafanikiwa kama yeye alivyo.
0784 989 512
Next Post Previous Post
Bukobawadau