Bukobawadau

GARI LA KAMPUNI YA UWINDAJI WA KITALII LA KAMATWA NA BANGI

Jeshi la Polisi mkoani Arusha limekamata gari la kampuni ya Wengert Windrose safari inayojihusisha na uwindaji wa kitalii katika maeneo mbalimbali nchini likiwa linasafirisha madawa ya kulevya aina Bangi. 
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Arusha Lebaratus Sabas amesema  madawa hayo kiasi cha magunia 11 yamekamatwa katika wilaya ya  Longido majira ya saa tano usiku yakisafirishwa kwenda nchi jirani   kwenye gari namba T695 ARR mali ya kampuni ya Wengert Safaris   ikiwa inaendeshwa na dereva wa kampuni hiyo aliyetajwa kwa jina la  Frank Faustine.

Kamanda Sababs amesema polisi walilitilia shaka gari hilo ambalo kwa kawaida linajulikana kuwa linabeba wageni na baada ya kufanya upekuzi ndipo wakagundua kuwa kilichobebwa kwenye gari hilo sio wageni bali ni madawa hayo ya kulevya aina ya Bangi.

Akizungumzia tukio hilo meneja maendeleo ya jamii wa kampuni hiyo  ya Wengert safaris Bi Aurelia Mtuy amesema madawa yaliyoakamtwa  ni mali ya dereva na wala sio mali ya kampuni na amelishukuru jeshi la  polisi kwa hatua hiyo ambayo pia imeisaidia kampuni kubaini maovu yanayofanywa na baadhi ya madereva wao.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi pamoja na kulipongeza jeshi la  polisi kwa hatua hiyo wameitaka serikali na idara zinazohusika kupanua  wigo wa kuweza kubaini mbinu mpya za kihalifu hasa wa usafirishaji   wa madawa kwani wana mtandao mkubwa ukiwemo ya kutumia magari  ya makampuni, watu maarufu, na taasisi zikiwemo za serikali.
CHANZO :ITV
Next Post Previous Post
Bukobawadau