Bukobawadau

WAFUGA NYUKI WA KAGERA KUTEMBELEA SHAMBA (MANZUKI) LA MH. PINDA

Wafuga nyuki kutoka mkoa wa Kagera watafanya ziara ya mafunzo kwenye manzuki ya Waziri Mkuu, Mh. Pinda iliyoko Dodoma mwezi ujao.  Akizungumza na Bukoba Wadau Media juu ya ziara hiyo, Mratibu wa Ushirika wa Wafuga Nyuki Kagera (Kagera Nyuki Mali Cooperative) Bwana Sadick Mwesiga amesema kuwa Ushirika umepata mwaliko wa kwenda kujifunza kwenye moja ya manzuki ya kisasa nchini. Mwaliko huu umepatikana baada ya kufanya mawasiliano kupitia kwa wasaidizi wa Waziri Mkuu.

Katika ziara hii Wafugaji wa Kagera watajifunza kwa kuona namna bora ya kufanya ufugaji wa kisasa kwa kutumia mizinga iliyoboreshwa. Pia watajifunza jinsi ya kuzalisha malkia wa nyuki, kutengeneza makundi ya nyuki na kuendesha manzuki kibiashara kwa mbinu za kisasa.

Ujumbe utakaofanya ziara Dodoma utajumuisha wafuga nyuki 20 wote kutoka Kagera.  wawapo Dodoma wafuganyuki hawa watapata fursa ya kulitembelea Bunge na kutambulishwa wakati wa vikao vya Bunge la Bajeti ya mwaka 2015/2016 kwa mwaliko wa Mbunge wa Bukoba Vijijini Mh. Jasson Rweikiza.

Kagera Nyuki Mali Cooperative ni Ushirika ulioanzishwa na wafuga nyuki mkoani Kagera kwa malengo ya kuwaunganisha wafuga nyuki ikiwa ni jitihada za kuyafanya mazao ya nyuki kuwa mazao mbadala ya kibiashara mkoani Kagera, kuongeza ubora na uzalishaji wa mazao ya nyuki kutoka Kagera, kuwahakikishia wafugaji nyuki masoko ya mazao ya nyuki yenye uhakika na yenye tija, kutafuta pembejeo na mitaji ya kuwawezesha wanaushirika kukukuza shughuli zao katika sekta ya nyuki na kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine katika kukuza sekta ya nyuki Tanzania.

Ili kufanya vema majukumu yake Ushirika umeanza zoezi la kuwatambua wafuga nyuki mkoani Kagera. Wadau wa sekta hii wanaweza kuwasiliana na ushirika kupitia nyukimali@gmail.com na simu namba 0767-988-173.
Next Post Previous Post
Bukobawadau