Bukobawadau

HALMASHAURI ZASHAURIWA KUPUNGUZA UTEGEMEZI WA RASILIMALI ZA KUKABILI MAAFA

Na. Mwandishi Maalum.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Mhe. Halima Dendego amezitaka Halmashauri za mkoani humo kupunguza utegemezi wa rasilimali za kukabili maafa kutoka kwa wafadhili wa nje badala yake zitumie rasilimali zilizopo mkoani humo katika kujenga uwezo wa kukabili maafa kwa kulipa kipaumbele suala la Kupunguza Athari za Maafa katika  mipango na programu za maendeleo.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa Mpango wa Kujiandaa Kukabili Maafa Mkoani Mtwara ulioandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya uratibu wa shughuli za maafa, tarehe 24 Aprili, 2015, mkoani Mtwara, Dendego alibainisha kuwa Halmashauri zinaweza kupunguza utegemezi wa rasilimali za kukabili maafa, kwa kuondokana na mtazamo wa kukabili maafa uliozoeleka ambao unatenganisha kwa kiasi kikubwa hatua za utoaji wa misaada ya kibinadamu, kurudisha hali na shuguli za kawaida za maendeleo.
“Majanga ya mafuriko, Ukame, na mlipuko wa kipindupindu yamekuwa yakizisumbua Halmashauri zetu mara kwa mara. Tunaweza kutumia rasilimali zetu  kukabili majanga haya badala ya kutegemea wafadhili wa nje, kwa kutumia rasilimali zetu tunaweza kutoa elimu kuhusu athari za ujenzi na kuendesha shughuli za uchumi katika maeneo hatarishi, umuhimu wa usafi wa mazingira matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame pamoja na kuzuia ujenzi katika maeneo hatarishi” alisema Dendego

Aliongeza kuwa, Upunguza Utegemezi wa rasilimali za kukabili maafa unawezekana kwa kuwa na jamii yenye kuhimili maafa kwa Kuzuia, kupunguza athari  na kujiandaa kama vipaumbele katika menejimenti ya maafa katika ngazi zote. Ili kuhakikisha kunakuwa na jamii hiyo, kila Halmashauri inapaswa kukaa na wadau wote katika halmashauri husika na kuainisha maeneo ya kushughulikia kwa haraka na kuwa  na mgawanyo bayana wa majukumu.
“Juhudi za jamii ni nguzo muhimu katika kujiandaa kukabili maafa, juhudi hizo zinajumuisha kuainisha na kutekeleza hatua zinazoweza kuchukuliwa kujiandaa kukabiliana na maafa yanayoweza kutokea ghafla kama mafuriko na yale yanayochukua muda mrefu na wa kati  kama ukame na janga la mabadiliko ya tabia nchi” alisema Dendego.
Awali akiongea katika uzinduzi huo Mkurugenzi Idara ya Uratibu Shughuli za Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu Brig.Jen Mbazi Msuya alifafanua kuwa kuandaliwa kwa mpango  huo ni jitihada  zinazochukuliwa na  serikali za kujenga uwezo katika ngazi za Halmashauri kukabiliana na maafa.





Next Post Previous Post
Bukobawadau