Bukobawadau

JESHI LA NIGERIA LAWAOKOA MABINTI 293

Jeshi la Nigeria limesema limewaokoa watoto wa kike mia mbili na tisini na tatu kutoka katika kambi ya Boko Haram iliyoko katika msitu wa Sambisa, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Jeshi hilo limesema watoto hao waliokolewa si kati ya wale waliotekwa mwaka mmoja uliopita na kundi la kiislamu katika eneo la Chibok.Jeshi limeiambia BBC kwamba wanawake na watoto hao wa kike walikutwa katika kambi nne tofauti ambapo silaha pia zimekamatwa,Msemaji wa jeshi amesema waliwapata wasichana hao baada ya kuziharibu kambi hizo.
"ni muda mfupi tu uliopita, wanajeshi wetu wameingia katika msitu wa Sambisa, kutokea upande wa Alafa, ambapo walikuta kambi nne zinazomilikiwa na wapiganaji na kuziharibu, hapo ndipo walipogundua kuwa kuna wasichana wapatao mia mbili na wanawake tisini na tatu."
Kwa sasa jeshi limezuiwa kutoa utambulisho wa wasichana hao. Hata hivyo, jeshi limethibitisha kwamba wasichana hao sio wale wanafunzi waliotekwa katika mji wa Chibok.
"tuko katika mchakato wa kuwachunguza hawa wasichana ili tuweze kubaini utambulisho wao, lakini kitu kimoja nataka nikiweke wazi kwa umma, tunapotaja idadi ya wasichana mia mbili, tayari watu wanaanza kufikiria wasichana mia mbili wa Chibok waliotekwa mwaka jana, hawa sio wasichana wa Chibok, tutaendelea kuwajuza kadri muda unavyokwenda iwapo kutakuwa na taarifa zozote. "

Next Post Previous Post
Bukobawadau