Bukobawadau

MKOA WA KAGERA WAADHIMISHA SIKU YA KUPANDA MITI KITAIFA WILAYANI ‘MISSENYI MISITU NI MALI PANDA MITI'



Aprili Mosi kila mwaka huwa ni siku ya kupanda miti kitaifa na mwaka huu 2015 mkoa wa Kagera ulipewa heshima ya kuadhimisha siku hiyo ambapo iliadhimishwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi na kushirikisha wadau mbalimbali pamoja na wananchi wanaojihusisha na kupanda miti na kutunza misitu.
Maadhimisho hayo yaliyoongozwa  na mgeni rasmi Naibu Katibu Mkuu Celestine Gesimba kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii ambapo maadhimisho hayo yalianzia katika Kijiji cha Bugolola eneo la Omukajunguti kwa  kupanda miti 2100 kwa kushirikisha  washiriki wote na wananchi wa kijiji hicho.
Kauli mbiu ya siku hiyo ilikuwa ni “Misitu ni Mali Panda Miti.” Katika Hotuba yake Naibu Katibu Mkuu Bw. Gesimba alisema wizara yake siyo kwamba inahamasisha wananchi kupanda miti ili kulinda mazingira tu bali wananchi wapande miti ili kunufaika nayo kwani ni mali inayoingiza kipato kikubwa kwa mwananchi mmoja mmoja.
Bw. Gesimba alisema wananchi wanatakiwa kupanda miti kwa wingi kwani miti isipopandwa itasababisha maafa makubwa hapo mbeleni kama inavyoanza kuonekana kwa sasa mfano, ukosefu wa mvua au mvua kutonyesha kwa wakati, joto jingi, kuyeyuka  kwa theruji mlima Kilimanjaro.
Bw. Gesimba alimalizia hotuba yake kwa kusema kuwa kutotunza misitu kumesababisha baadhi ya sehemu kuwa jangwa au kusababisha  ugonjwa wa malaria mfano  Lushoto mkoani Tanga ambako hakukuwa na ugojwa huo miaka ya 1970 na 1990. Aidha alitahadhalisha misitu kutoweka kabisa kwani kila baada ya dakika sita (6) nusu kiolmeta ya misitu hutoweka duniani.
Bwana Jaffari Omary Afisa Misitu katika Ofisi ya Mkuu wa mkoa akitoa salaamu za mkoa wa Kagera alisema mkoa wa Kagera una jumla ya misitu 17 yenye hekta 341,756.35 pia eneo la misitu na vichaka ni kilometa za mraba 10,148 sawa na asilimia 35 ya nchi kavu ya mkoa mzima.
Mkoa wa Kagera una misimu miwili ya upandaji miti, msimu wa vuli ambapo wananchi hupanda miti kwa wingi kutokana na msimu huo kuwa na mvua za kutosha pia na msimu wa masika ambapo nao hutumika kupanda miti kwa wingi, alifafanua Bw. Jaffari Omary .
Meneja wa Wakala wa Huduma za Misitu Kanda ya ziwa Bw. Haji Khatibu akitoa salaam za Kanda ya Ziwa alisema kuwa kutokana na utafiti uliofanyika mwaka 2003 Kanda ya Ziwa  ilionekana kuwa misitu imebakia mapori tu  kutokana na uchomaji moto ovyo, mifugo mingi na wananchi kutoshiriki kuitunza misitu, uchomaji mkaa, kilimo na uvunaji wa mbao usiozingatia kanuni na taratibu.
 Aidha Bw. Khatibu alisema uharibifu wa miti unachangiwa pia na sera mbalimbali kuingiliana na alitoa mfano katika halmashauri za Wilaya kutoa maeneo ya hifadhi za misitu kwa wananchi kama viwanja vya kuishi na kuendesha kilimo jambo ambalo linapelekea uharibifu mkubwa katika maeneo hayo ya hifadhi.
Ili kukabiliana na changamoto hizo na kuzipatia ufumbuzi Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea kuwahasisha wananchi kushiriki katika kuilinda na kuitunza misitu kupita serikali zao za vijiji na vitongoji pamoja na mwananchi mmoja mmoja kutoshiriki katika vitendo ovu vya kuharibu misitu.
Aidha serikali imekuwa ikiendesha doria katika maeneo ya hafadhi za taifa ili kukabiliana na uvamizi wa maeneo hayo pia kukamata mazao ya misitu ambayo yanavunwa bila kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za uvunaji  na kuwachukulia hatua kali wahusika wanaokamatwa.
Mwenyekiti wa halmashauri ya Wilaya ya Missenyi William Katunzi akitoa shukrani zake kwa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuadhimisha siku ya kupanda miti kitaifa Wilayani missenyi alisema tayari kwa mkoa wa Kagera wananchi wanajua nini maana ya kupanda miti kwa sasa, wapanda miti kibiashara ili kujipatia kipato pia kulinda mazingira.
Takwimu za upandaji na utunzaji wa miti katika mkoa wa Kagera kwa miaka minne  mfululizo; mwaka 2011/2012  lengo la kupanda lilikuwa miti 12,500,000 Miti iliyopandwa ni 13,100,875 sawa na asilimia 105, Miti iliyopona ni 11,220,328 sawa na asilimia 89.7. Mwaka 2012/2013 lengo la kupanda lilikuwa miti 12,500,000 Miti iliyopandwa ni 12,755,042 sawa na asilimia 102, Miti iliyopona ni 11,081,519 sawa na asilimia 88.
Aidha mwaka 2013/2014 lengo la kupanda lilikuwa miti 13,000,000 Miti iliyopandwa ni 13,767,022 sawa na asilimia 85, Miti iliyopona ni 11,248,933 sawa na asilimia 88.4. Na mwaka 2014/2015 lengo la kupanda lilikuwa miti 13,000,000 Miti iliyopandwa ni 12,278,125 sawa na asilimia 98.4, Miti iliyopona ni 11,153,627 sawa na asilimia 90.8
Next Post Previous Post
Bukobawadau