Bukobawadau

HAFLA YA UFUNGAJI RASMI WA KAMBI YA WATOTO (ARIEL CAMP )ILIYOANDALIWA NA SHIRIKA LA AGPAHI MJINI BUKOBA JUNE 19,2015

Mgeni Rasmi katika ufungaji wa kambi ya watoto (Ariel Camp) iliyoandaliwa  na shirika la AGPAHI, Mh. John Mongella akiwahutubia waalikwa na watoto walioshiriki hafla hiyo.
 Sehemu ya Watoto wanao hudumiwa na shirika la AGPAHI wakimsalimia Mgeni Rasmi katika hafla ya ufungaji kambi iliyofanyika Ijumaa June 19,2015 katika hoteli ya ELCT  Bukoba.
Baadhi ya waalikwa wakati wa utambulisho.
 Baadhi ya wafanyakazi wa shirika la AGPAHI kutoka kushoto (Liberator Kagenzi na Cecilia Yona)
Madaktari kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania -kutoka kushoto ni Dr. Festo Manyama na Dr. Maimuna Ahmed wakimsikiliza Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mh. John Mongella.
 Hotuba fupi ya mheshimiwa Mgeni Rasmi John V. K. Mongella
·        Mkurugenzi Mtendaji wa AGPAHI,
·        Mganga Mkuu (M) - Kagera,
·        Waganga Wakuu (M) – Shinyanga na Simiyu
·        Meneja wa Miradi wa AGPAHI – Shinyanga & Simiyu,
·        Madaktari kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania,
·        Wafanyakazi wa AGPAHI,
·        Walezi wa Watoto,
·        Wadau mbalimbali wa Afya na Haki za Watoto,
·        Watoto wa Kambi ya Ariel,
·        Waandishi wa Habari,
·        Wageni Waalikwa,
·        Mabibi na Mabwana.

Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa Rehema kwa  kutuwezesha kukutana pamoja siku ya leo. Pia, napenda kuushukuru uongozi wa AGPAHI kwa kuandaa kambi hii ya watoto na kunikaribisha kushiriki katika siku hii muhimu ya kufunga rasmi kambi ya watoto iliyofanyika kwa muda wa wiki moja. Ninayo furaha kubwa sana kuwa nanyi hapa na nachukua fursa hii kuwakaribisheni Mkoa wa Kagera.

Vile vile, ninapenda kuwashukuru wageni waalikwa kwa kuweza kufika hapa, hii inaashiria kuwa mnatambua na mnathamini umuhimu wa kuwajali watoto hawa.

Ndugu wageni Waalikwa,
Nimefahamishwa kwamba, shirika la AGPAHI lilianza huduma za malezi na kuwakutanisha watoto katika vikundi baada ya kuanzishwa kwa Shirika lenyewe mwaka 2011. Nawapongeza kwa kuunda vikundi vidogo vidogo vya watoto katika vituo vya kutolea huduma za afya ambapo hadi sasa, mmenieleza mna jumla ya vikundi vipatavyo 35 vya watoto kwenye mikoa ya Shinyanga na Simiyu vyenye jumla ya watoto 1541.

Kutokana na kuundwa kwa vikundi hivi, AGPAHI iliweka utaratibu wa kuendesha kambi ili kuwakutanisha watoto kutoka kwenye vikundi mbalimbali kwa lengo la kujifunza kuhusu afya na stadi za maisha na pia kubadilishana uzoefu. Pia, kambi hizi huwajenga vijana na kuwafanya mabalozi wa huduma za watoto katika jamii. Kambi hizi za watoto zimekuwa zikifanyika mara moja kwa mwaka na kambi hii ni ya Tano kufanyika. Kambi mbili za mwanzo zilifanyika mkoani Mwanza na kambi ya tatu na ya nne zimefanyika mkoani Kilimanjaro; na kambi ya tano mkoani Kagera.

Wageni Waalikwa,
Nimefurahishwa na jitihada hizi za shirika la AGPAHI kwani zinawajenga watoto kisaikojia na kuboresha afya za watoto katika nyanja mbali mbali. Kupitia mkusanyiko huu, nawaomba wadau wengine wa afya na haki za watoto kuiga jitihada hizi, kwa kuwapa huduma stahiki na kuwalea watoto wetu katika maadili yanayokubalika.

Vilevile, nachukua fursa hii, kuwasihi watoto mzingatie masomo ikiwa ndio msingi mkuu wa maisha ya baadae. Nimefahamishwa kuwa, shirika la AGPAHI hivi punde litawapatia mahitaji ya shule ikiwemo sare za shule na madaftari ili muweze kusoma vizuri. Pia nawaomba mzingatie kanuni za afya ikiwemo ufuasi mzuri wa dawa kama mnavyoelekezwa na wataalam wa afya na endeleeni kuwa wanachama wazuri katika vikundi vya watoto vinavyosimamiwa na AGPAHI.
 Natambua kuwa katika kipindi cha wiki moja mmeweza kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo - stadi za maisha na mabadiliko ya tabia kutokana na msukumo wa kundi, taarifa sahihi kuhusu VVU na UKIMWI, usafi binafsi, elimu ya ujana, mahusiano na Uzazi wa Mapango, ufuasi mzuri wa dawa, lishe, jinsi ya kuwasiliana, huduma na msaada wa kisaikolojia. Pamoja na mafunzo mliyojifunza katika kambi hii, mmeongeza wigo wa jiografia yenu kwa kusafiri kuja Mkoa wa Kagera na kufanya matembezi ya kwenda kwenye kiwanda cha sukari cha Kagera, kuona mto Kagera, makumbusho ya vita vya Idd Amin hadi mpaka wa Tanzania na Uganda.
Pia, napenda kuwashukuru walezi ambao wamesafiri na watoto kutoka mikoa ya Shinyanga na Simiyu. Naomba mpeleke shukrani kwa walezi wengine waliobaki kwa kazi nzuri wanazozifanya za kuunda vikundi vya watoto, kuwalea watoto katika maadili mazuri ya kitanzania na kuwaelimisha juu ya huduma za afya.
Mwisho napenda kuwaaga watoto na walezi na nawatakia safari njema mnaporudi nyumbani. Pia, nawatakieni masomo mema. 
Baada ya kusema hayo machache, sasa napenda kutamka rasmi kuwa, Kambi ya Ariel mwaka 2015 mkoani Kagera imefungwa.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA!
MC muongozaji wa shughuli hii Bw. Emilian Ng'wandu.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la AGPAHI Bw. Laurean .R.Bwanakunu kwenye ufungaji rasmi wa Kambi ya Ariel.
 Afisa Mawasiliano  wa shirika la AGPAHI, Jane Shuma akitolea jambo ufafanuzi.


Hotuba fupi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la AGPAHI Bw. Laurean .R.Bwanakunu kwenye ufungaji rasmi wa Kambi ya Ariel, leo Ijumaa June 19,2015
Ndugu,
·        Mgeni Rasmi, Mkuu wa Mkoa wa Kagera,
·        Mganga Mkuu (M) - Kagera,
·        Waganga Wakuu (M) – Shinyanga na Simiyu
·        Madaktari kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania,
·        Meneja wa Mradi wa AGPAHI – Shinyanga & Simiyu,
·        Wafanyakazi wa AGPAHI,
·        Walezi wa Watoto,
·        Wadau mbalimbali wa Afya na Haki za Watoto, (MDH, ICAP, JHPIEGO, Red Cross, World Vision Kagera, HUYAWA (Huduma ya Watoto), Tumaini Children Centre, Uyacho Orphanage Centre, TADEPA na TACDEN)
·        Watoto wa Kambi ya Ariel,
·        Waandishi wa Habari,
·        Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana.


Habarini za asubuhi !
Ndugu Mgeni rasmi, Awali ya yote napenda kutoa shukrani kwako kwa kuacha shughuli zako na kuja kujumuika na sisi hapa kwenye Kambi ya Ariel (Ariel Camp). Tunasema asante sana!
Pia napenda kuwashukuru sana walezi waliokuja na watoto toka Simiyu na Shinyanga. Vile vile napenda kuwashukuru wafanyakazi wenzangu wa AGPAHI na wadau wengine kwa jitihada zao za hali na mali katika kuandaa kambi hii ya watoto. Hii ni mara ya kwanza kwa AGPAHI kuandaa kambi hii katika mkoa wa Kagera, tunafarijika sana kuwa hapa.
Ndugu Mgeni rasmi, Shirika la AGPAHI ni shirika lisilo la kiserikali linaloendeshwa na watanzania na watanzania wenyewe ndio sisi hapa. Kuanzishwa kwa shirika linaloendeshwa na watanzania ilitokana na dira ya serikali ya Tanzania na ile ya wafadhili  yaani serikali ya Marekani kutaka wazawa (serikali pamoja na mashirika yasiyo ya serikali) kuendesha miradi mbalimbali inayoshughulikia masuala ya VVU na UKIMWI na masuala ya afya ya mama na mtoto ili kuwa na miradi endelevu.
Shirika letu linatoa huduma katika mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Geita. Huduma zitolewazo ni pamoja na tiba na matunzo, kuzuia maambukizi ya virusi toka kwa mama kwenda kwa mtoto na huduma za uzazi wa mpango.  Hadi mwezi Machi mwaka huu, AGPAHI imeweza kuandikisha wateja 96,638 (wanaume 34,342 na wanawake 55,975) kwenye huduma za matunzo ambapo 6,321 ni watoto walio chini ya umri wa miaka 15 na hii sawa ni asilimia 7.
Vilevile AGPAHI imeweza kuwaanzishia dawa wateja wapatao 63,048 (wanaume 21,555 na wanawake 36,969) kwenye huduma za tiba ambapo watoto ni 4,524 ambayo ni sawa na asilimia 7.
Dira ya shirika ni kuhakikisha tunatokomeza maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa watoto na kuondoa UKIMWI kwa watoto. Katika kutekeleza azma hiyo shughuli mbalimbali zinatekelezwa ikiwa ni pamoja na kuwapatia watoto huduma za matunzo na matibabu pamoja na huduma za kisaikolojia. Katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu, kuna jumla ya watoto 694,454 kati yao watoto 6,321 wanaishi na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi.
Mgeni Rasmi, shirika la AGPAHI lilianza huduma za malezi na kuwakutanisha watoto katika vikundi vidogo vidogo baada tuu ya kuanzishwa kwake. Vikundi hivi vipo katika vituo vya kutolea huduma za afya (yaani CTC) ambapo hadi sasa tuna jumla ya vikundi vipatavyo 35 (vikundi 19 kwa mkoa wa Shinyanga na vikundi 16 kwa mkoa wa Simiyu). Vikundi hivi vina jumla ya watoto 1,541.wanatoka katika vituo mbalimbali kwenye halmashauri zote za mikoa ya Shinyanga na Simiyu. 
Katika kipindi hiki cha wiki moja, watoto wameweza kujifunza mambo mbalimbali kama vile: Usafi binafsi; Stadi za maisha na Mabadiliko ya tabia kutokana na msukumo wa kundi; Taarifa sahihi kuhusu VVU na UKIMWI; Haki na wajibu watoto; Huduma na msaada wa kisaikolojia; Jinsia, mahusiano ya kimapenzi na Uzazi wa Mpango; Ufuasi mzuri wa dawa na Kuweka wazi hali yako (disclosure).
Katika wiki hii ya kambi, watoto pia wameweza kupata huduma ya kisaikolojia pamoja na kuhudumiwa na madaktari wa watoto kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto Tanzania.

Mbali na mafunzo, watoto pia wamefanya matembezi na kuona mto Kagera, Kagera sugar factory, kuona na kuelezewa maeneo ya vita vya IDD AMIN na pia wamefika Mutukula (mpaka wa Tanzania na Uganda).
Ningependa kutambua washindi wa Shindano la Mr and Miss Ariel camp ambalo lilifanyika jana usiku. Washindi wetu walikua James Jackson (Mr. camp) kutoka Zahanati ya Bugarama (MSALALA) na Anastazia Daniel (Miss Camp) kutoka Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Naomba wasimame na tuwapigie makofi.

Ndugu mgeni rasmi, napenda kutoa shukrani zetu kwa Watu wa Marekani kupitia shirika lao la CDC ambao ndio wahisani wa kambi hii.   Hata hivyo tuna wafadhili wetu wengine kama EGPAF, UNFPA na USAID ambao nao wanatusaidia katika kazi zetu. Pia shirika letu linafanya kazi kwa karibu sana na ofisi ya Waziri Mkuu –TAMISEMI na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA!
LAUREAN RUGAMBWA BWANAKUNU
 Mgeni Rasmi akikabidhi zawadi kwa watoto
Dada Edwiga Zumba akitoa maelezo kwa mgeni Rasmi jinsi  watoto walivyo elezea miti yao ya maisha.
 Dr.Festo Manyama akipokea cheti cha ushiriki kutoka AGPAHI.
 Dada Holo Bassu,mhudumu kutoka zahanati  ya Itinje mara baada ya kupokea cheti cha ushiriki.
 Kaka Mbanga Kaijunga kutoka zahanati ya Negezi nae akipokea cheti chake cha ushiriki.
 Zoezi la kukabidhi vyeti vya ushiriki likiendelea kwa Wahudumu kutoka  katika vituo mbalimbali vya afya vinavyoshirikiana na  shirika la AGPAHI.

 Mwandishi wa habari kutoka Tanzania Daima Irene Mark akipokea cheti cha ushiriki.
Mwandishi Enjoy  Mavuri  kutoka kampuni ya The Guardian akipokea cheti cha ushiriki
 Mama Grace Buberwa akitazama cheti chake cha ushiriki alichopewa na AGPAHI.
 Wafanyakazi wa AGPAHI katika picha na mfanyakazi wa ELCT Hotel Bukoba (Aristides Musheshe)
 Dada Liberator Kagenzi akiendelea na kazi
 Msaikologia Jasson Lwankomezi akiteta na watoto.
 Dr.Haruna kutoka hospital ya mkoa nae alikuwa mmoja wa waalikwa.
 Mwanahabari Irene Mark mbele ya Camera yetu.



Next Post Previous Post
Bukobawadau