Bukobawadau

Mil. 207 zatumika kupunguza athari za ukame Kishapu

Mratibu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu wa Mradi wa Kuijengea Jamii Uwezo wa kupunguza Athari za Maafa kwa Mikoa iliyoathirika zaidi na Ukame, , Harrison Chinyuka  akisisitiza  jambo   wakati wa mafunzo ya menejimenti ya maafa kwa Wataalam na waratibu maafa mkoani Shinyanga tarehe 25, Juni, 2015.
 Mratibu Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa, Theodosia Mbunda akifanya majadiliano na washiriki wa mafunzo ya menejimenti ya maafa mkoani Shinyanga wakati wa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ofisi hiyo  kwa waratibu wa Maafa mkoani Shinyanga tarehe 25, Juni, 2015.
 Mshiriki wa mafunzo ya Menejimenti ya maafa mkoani Shinyanga, Pastor Mphoy akisisitiza jambo wakati wa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ofisi hiyo  kwa waratibu wa Maafa mkoani humo tarehe 25, Juni, 2015.
 Mkuu wa Huduma za Hali ya Hewa kwa Jamii, Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania, Hellen Msemo, akifanya majadiliano na washiriki wa mafunzo ya menejimenti ya maafa mkoani Shinyanga wakati wa mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Ofisi hiyo  kwa waratibu wa Maafa mkoani Shinyanga tarehe 25, Juni, 2015.


Na.  Mwandishi Maalum.
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu maafa imefanikiwa kupunguza athari za maafa yatokanayo na ukame wilayani Kishapu kwa kutumia jumla ya Shilingi milioni 207 kwa kutekeleza Mradi wa Kuijengea Jamii Uwezo wa Kupunguza Athari za Maafa yatokanayo na ukame wilayani humo kwa  kuijengea jamii uwezo wa kupata uhakika wa chakula na kipato.
Mradi huo umetekelezwa kwa mafanikio katika kata 3 za Mwamalasa, Masanga na Langana, ambapo vikundi vya maendeleo kumi (10)  vyenye  jumla ya wanachama 100 vimefanikiwa katika ufugaji wa   Mbuzi na kuku, kilimo cha viazi, mtama, mboga mboga pamoja, upandaji wa miti kwa  uhifadhi wa mazingira na utengenezaji mtandao wa maji safi na salama kwa matumizi ya binadamu.
Akiongea wakati wa mafunzo ya waratibu maafa na wataalum katika ngazi za kata, Shinyanga tarehe 25 Juni, 2015, Mratibu maafa Wilayani Kishapu, Ponsian Kuhabwa amefafanua kuwa fedha hizo zilizotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu  kwa menejimenti ya maafa ya ukame zimefanikisha kata 3 zinazotekeleza mradi huo kupata uhakika wa chakula na kipato.
Kuhabwa; “Fedha tulizozipata katika kipindi cha miezi sita ambacho tumetekeleza mradi huu  tumeweza kutoa mafunzo ya menejimenti ya maafa ya Ukame kwa wataalamu wa ngazi za kata, mafunzo ya Ugani, kununua pembejeo,  vifaa na dawa za mifugo, kupitia mradi huu tunao mbuzi 1050, kuku 1800  ikiwa awali walipatiwa mbuzi 550 na kuku 550 hali ambayo huzifanya kata hizo kutoathiriwa na ukame.”
Mkazi wa kijiji cha Masanga, kata ya Masanga, wilayani Kishapu, Magreth William, amebainisha kuwa ukame uliokuwa ukiikumba kata hiyo mara kwa mara, walikuwa wanapata athari za upungufu wa chakula pamoja na kutokuwa na kipato kutokana na mazao yao ya biashara kuharibikia mashambani.
William; “Tumeweza kupunguza athari za maafa ya ukame kupitia mradi huu kwa kuwa tunao uhakika wa chakula kwa kuwa tunalima mazao yanayo himili ukame kama mtama na viazi lishe lakini pia tunao uhakika wa kipato kwa kuwa tunafuga mbuzi na kuku hivyo pamoja na ukame unaendelea kujitokeza lakini kwa sasa hatuathiriki kama awali”.
Mradi wa Kuijengea Jamii Uwezo wa Kupunguza Athari za Maafa kwa Mikoa iliyoathirika zaidi na ukame unafadhiliwa na Benki ya Dunia na kusimamiwa na UNICEF chini ya uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Halmashauri husika wakiwa Watendaji wakuu wa mradi huo. Mradi huo unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 18, ulizinduliwa wilayani  Same, mkoani Kilimanjaro tarehe 11 Desemba, 2013.
Next Post Previous Post
Bukobawadau