Bukobawadau

EDO KUMWEMBE:NDOA YA UKAWA NA LOWASSA

By Edo Kumwembe, Mwananchi
Jioni ya Januari 25, 1965 wakati Waingereza walipomzika Waziri Mkuu wao maarufu wa zamani, Winston Churchill katika makaburi ya St Martin’s Church, Bladon eneo la Oxford ilimaanisha kuwa Waingereza walikuwa wanamzika mmoja wa wanasiasa wazuri waliowahi kutoa tafsiri nzuri ya neno siasa.
Katika ubora wake, Churchill, mmoja wa wanasiasa bora wa muda wote duniani, aliwahi kusema; ‘Siasa ni uwezo wa kutabiri kitu ambacho kinaweza kutokea kesho, wiki ijayo, mwezi ujao na mwaka ujao, na baadaye bado uweze kuelezea kwanini hakikutokea.”
Usiku wa Julai 26, 2015 ambao Waziri Mkuu wa zamani wa Tanzania, Edward Ngoyai Lowassa alitinga katika ukumbi nadhifu wa Bahari Beach, Jumapili kuamkia Jumatatu kukutana na washirika wake wapya katika siasa – Chadema – ungeweza kumkumbuka Churchill kwa mambo mengi. Lakini hasa kwa kauli yake hiyo hapo juu.
Pande mbili ambazo kwa nyakati tofauti ziliwahi kuwa na hisia tofauti hatimaye zimekuwa pamoja. Upande huu uliwahi kusema Lowassa ni fisadi na hafai. Huu ni upande wa ndugu ninaowaheshimu akina Dk Willibrod Slaa, John Mnyika, Freeman Mbowe na wengineo. Upande ule mwingine wa Mheshimiwa Lowassa nao uliwahi kusema kuwa Chadema na wapinzani hawapo tayari kushika dola.
Watanzania wamepigwa butwaa na kushindwa kuamini kama kweli Lowassa angeweza kufupisha safari yake ya matumaini kutoka Simba kwenda Yanga, au kutoka Yanga kwenda Simba. Lakini haupaswi kushangaa sana kwa sababu hapa anazungumziwa mtu ambaye kwa miaka mitano sasa anahubiri sera ya kuwapeleka Watanzania katika nchi ya ahadi kupitia maamuzi magumu.
Alichofanya ni maamuzi magumu. Tumeongozwa na mawaziri wakuu kumi mpaka sasa, lakini hajawahi kutokea Waziri Mkuu ambaye alivuka mpaka huo. Unahitaji kuwa na roho ngumu. Lakini wanaomfahamu vizuri Lowassa hawajamshangaa.
Huyu ni mpambanaji ambaye kama aliweza kulirudisha jina lake kufikiriwa kuwa mgombea wa urais ndani ya chama chake baada ya matusi, kebehi, kejeli dhidi yake baada ya kuondoka kichwa chini katika Uwaziri Mkuu Februari 7, 2008, angeshindwa nini kuendelea kupambana licha ya CCM kuchinja jina lake wiki mbili zilizopita mjini Dodoma?
Hata hivyo, kuhamia kwake Chadema kunaleta taswira nyingi zenye mkanganyiko. Taswira ambazo zinamwacha Mtanzania wa kawaida akiendelea kumwamini Churchill ambaye Waingereza walimzika miaka 50 iliyopita.
Kwake yeye mwenyewe, hapana shaka, hii ilikuwa karata yake ya mwisho katika ndoto yake ya muda mrefu ya kuusaka urais wa Tanzania. Bado mwezi mmoja kutimiza umri wa miaka 63; Agosti 26 atatimiza umri huo.
Ndoto hizi zilianza mwaka 1995, wakati alipokwenda Dodoma kupeleka fomu za urais akiwa na Rais wa sasa ambaye anaondoka madarakani, Jakaya Mrisho Kikwete wakijulikana kama Boyz II Men. Wakati ule, mambo yalikuwa magumu kwa wote lakini mwaka 2005, rafiki yake kipenzi akafanikiwa kuishika nchi huku yeye akiwa nyuma ya mchakato mzima.
Kitendo cha CCM kukata jina lake ndani ya michakato ya chama iliyoongozwa na rafiki yake na kumnyima fursa ya kuwa mgombea wao, kilimaanisha kuwa Lowassa hakuwa na njia nyingine ya kutimiza ndoto hii binafsi kwa kusubiri miaka 10 mingine ambayo ingemkuta akiwa na umri wa miaka 73. Chadema au Ukawa ndiyo lilikuwa chaguo pekee mbadala kwa ndoto yake.
Mambo mawili yanaweza kujitokeza baada ya maamuzi haya. Kwa Lowassa mwenyewe; huu unaweza kuwa mwanzo wake, au mwisho wake. Ilitokea mwaka 1995 kwa Waziri wa Mambo ya ndani wa zamani, Augustine Mrema ambaye alihamia upinzani kwa ajili ya kusaka urais lakini akaambulia patupu.
Kuanzia hapo umaarufu wake ulishuka kwa kasi ya ajabu na sasa ameendelea kuwa mpinzani dhidi ya wapinzani wa chama ambacho yeye mwenyewe alikuwa akikishambulia tangu mwaka 1995, CCM.
Hapana shaka Lowassa amepima uwezekano huu. Ana washauri wake. Ana rafiki zake. Ana familia yake. Kwa chochote ambacho wamemshauri, endapo Lowassa atashindwa kufikia lengo lake baada ya Oktoba 25 basi jina lake litabakia kuwa historia.
Kwa Chadema, huu ulikuwa uamuzi wa kumtafuna jongoo kwa meno. Hapa wanamkaribisha mtu ambaye kwa nyakati tofauti waliwahi kuhoji uadilifu wake ndani ya Serikali na zaidi katika kashfa ya Richmond ambayo ilimpotezea wadhifa wake jioni ya Februari 7, 2008.
Chadema nao wamechukua maamuzi mazito kama ambayo Lowassa amechukua. Ndoa yao ni kamari. Kwao, Lowassa ni mtaji wa kisiasa ambao unaweza kuwaacha bila ya nguo baada ya Oktoba 25.
Kuanzia sasa na kuendelea, kuna kundi kubwa la watu litaanza kuhoji kama kweli chama chao kina dhamira ya kweli ya kuikomboa nchi hii kwa kumchukua mtu ambaye hata wao walihusika katika kummwagia tuhuma nyingi siku za nyuma.
Lakini hapohapo huenda vigogo wa chama hiki na washirika wenzao wa Ukawa wasijali sana maneno haya kama watafanikisha azma ya kuing’oa CCM kwa gharama yoyote au kuingiza kundi kubwa la wabunge wa upinzani.
Endapo haya mawili au moja kati ya haya litafanikiwa, Chadema itakuwa imenusurika na itaweza kuishi kwa kiburi katika siku za usoni. Lakini kama haya yote yakishindikana, umaarufu wa Chadema utapotea kwa kasi mithili ya samli inavyopotea katika kisu chenye moto.
Ndoa hii ni ngumu kwa kila upande. Lakini tofauti na wengi wanavyofikiri, ndoa hii ni ngumu zaidi kwa Chadema na Ukawa kuliko kwa Lowassa binafsi. Lowassa ni mwanadamu mwenye ndoto zake binafsi ambaye ameamua kuzifuata kwa gharama zozote zile. Anajiamini na anaitawala akili yake. Ni mtu imara kifikra.
Maisha yake, kama ilivyo kwa mwanadamu yeyote yule, ni maisha mafupi. Anapaswa kupigania ndoto zake. Lakini chama huwa kinaishi maisha marefu zaidi ambayo yanajitanabahisha kwa falsafa zake na misingi imara. Naamini mwanadamu anaweza kufuata njia fupi katika mafanikio, lakini si lazima chama kifuate njia fupi katika mafanikio.
Mwanasiasa maarufu wa zamani wa Italia, ambaye alikuwa mwanadiplomasia maarufu na mwanafalsafa, Niccolo Machiavelli aliwahi kusema kuwa siasa ha
ina uhusiano na maadili thabiti. Inawezekana Chadema wamechukua njia hiyo.
Lakini kwa sasa hakuna tunachoweza kufanya zaidi ya kufurahia maneno ya Churchill kuhusu siasa. Acha tusikie jinsi wanavyokana wale waliyoyasema kuhusu kila mmoja wakati huu wa ndoa yao ya kusisimua katika historia ya nchi.
Nawatakia kila la kheri Lowassa, Chadema na Ukawa. Mwisho wa siku, jioni ya Oktoba 25 wakati matokeo ya baadhi ya vituo vya kupigia kura yatakapokuwa yanatolewa, ni wazi mkondo mpya wa historia utakuwa umefunguliwa nchini.
Kuna kila sababu ya kuamini kuwa utakuwa mwanzo au mwisho wa Lowassa, mwanzo au mwisho wa Chadema, mwanzo au mwisho wa Ukawa. Lakini tusisahau kuwa unaweza kuwa mwisho wa CCM imara. Yote yanawezekana. Tuvute pumzi.
Next Post Previous Post
Bukobawadau