Bukobawadau

MBUNGE AJIVUA UANACHAMA CHADEMA

Sumbawanga. Mbunge wa Mpanda Mjini, Said Arfi ametangaza kujivua uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza mjini Mpanda katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika Uwanja wa Shule ya Msingi Kashaulili, jana Arfi aliwaeleza wananchi wa Mpanda kuwa uanachama wake ndani ya Chadema utakoma mara tu baada ya kuvunjwa Bunge Julai 9.
Pia, alitumia mkutano huu kuwaaga wananchi wa jimbo hilo akisema hatagombea tena nafasi hiyo aliyoitumikia kwa miaka 10.
Arfi alifafanua kuwa hayuko tayari kugombea jimbo hilo kupitia chama chochote cha siasa na kauli hiyo imelenga kuondoa uvumi uliokuwa umeenea kwamba alikuwa na nia ya kugombea kupia ama ACT – Wazalendo au CCM.
Alisema amekuwa akishangazwa na kauli ambazo zimekuwa zikitolewa na baadhi ya wanachana na wapenzi wa Chadema kuwa hajafanya lolote kwenye chama hicho.
Alisema kama kuna mtu anayekifahamu vizuri chama hicho ni yeye, hivyo haoni sababu za watu kumbeza.
Alisema alikuwa ameamua kukaa kimya na kuwa akiamua ‘atamwaga mboga’ ili watu wafahamu upungufu ulioko ndani ya chama hicho.
Alisema hagombei katika jimbo hilo na kama kweli chama hicho kina nguvu, basi kilitetee, akisisitiza kuwa ana uhakika jimbo hilo litakwenda CCM kwa kuwa wananchi wa Mpanda Mjini walikuwa na mapenzi na mtu siyo chama.
Arfi aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema kabla kujiuzulu wadhifa huo, aliwahi kuhusishwa kusuka mpango wa kumwezesha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kupita bila kupingwa katika kinyang’anyiro uchaguzi wa mwaka 2010 katika Jimbo la Katavi kwa kuwashawishi baadhi ya wagombea kuondoka majina yao.
Hata hivyo, Arfi amekuwa akikanusha tuhuma hizo, hali ambayo pia ilisababisha kutokuelewana na baadhi ya viongozi wenzake na kusababisha kujiuzulu nafasi yake ya umakamu mwenyekiti.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na gazeti hili walionyesha kushtushwa na kauli ya mbunge huyo kujiondoa Chadema lakini wakasema ametimiza haki yake ya kikatiba kuchagua sehemu iliyo sahihi kwake.
Mmoja wa wananchi hao, Abdallah Hussein alisema: “Arfi amekuwa mvumilivu sana ndani ya Chadema lakini anayo ya moyoni sasa kwa muda mrefu amekaa kimya aliogopa ya Zitto Kabwe yasimtokee, sasa ameweka bayana msimamo wake acha tuheshimu mawazo yake.”
CREDIT:Mwananchi
Next Post Previous Post
Bukobawadau