Bukobawadau

JENERALI ULIMWENGU:Tusipojifunza kutoka historia yetu hatutaweza kuona yajayo

MATUKIO ya kisiasa ya hivi karibuni, na ambayo yataendelea kwa muda hadi Uchaguzi Mkuu mwishoni mwa mwezi Oktoba, yanatoa mafunzo maridhawa kwa yeyote anayefuatilia nyendo za wanasiasa wetu. Baadhi ya mafunzo hayo si mapya, kwani tulikwisha kuyapitia katika wiki, miezi na miaka iliyopita, lakini halitakuwa kosa kama tukiyarejea.
Mosi, ni dhahiri kwamba nchi hii haina vyama vya siasa vinavyostahili kuitwa jina hilo, bali inavyo vikundi vya wanasiasa ambao shughuli yao kubwa ni kusaka madaraka kwa njia yoyote itakayowasaidia kupata nafasi za kutawala. Kwa hiyo kuhama kutoka chama kimoja na kuingia kingine si jambo la kushangaza.
Kuhamahama kwa wanasiasa kutoka chama hadi chama kungeshangaza iwapo vyama vingekuwa na falsafa na itikadi zilizojipambanua kwa maudhui yake. Kwa sasa vyama vyetu havina sifa hiyo.
Labda kinachoonekana leo hii hakijawahi kutokea kwa maana kwamba tukio kuu katika kuhamahama kwa msimu huu limekuwa ni kule kuhama kwa Edward Lowassa kutoka CCM na kujiunga Chadema. Hii ni kwa sababu huyu ndiye mtu aliyewahi kushika wadhifa mkuu katika serikali ya chama-tawala huko nyuma, na kisha akakihama chama chake na kujiunga na chama kinara cha upinzani nchini.
Ni kweli kwamba mwaka 1995aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya ndani na naibu waziri mkuu kabla ya kushushwa cheo katika serikali, Augustine Mrema, pia alihama kutoka CCM na kujiunga NCCR. Hata hivyo, Mrema alikuwa mdogo kwa nyadhifa alizokuwa kapewa akilinganishwa na Lowassa, na wala hakuwahi kuwa na nafasi yoyote ya maana kichama. Kwa hiyo tunaweza kusema kuhama kwa Lowassa hakujawahi kutokea.
Pili, tunashuhudia hamasa kubwa aliyosababisha Lowassa kwa kuhama kwake. Jumatatu ya wiki hii ilikuwa ni siku ya kihistoria kwa wakazi wa Dar es Salaam na kwa jinsi msafara wa Lowassa ulivyofunga barabara za jiji kwa muda kutokana na “mafuriko” ya watu waliomsindikiza.
Hili nalo si jipya kwani katika zama zake Mrema pia aliwahi kuwa na wasindikizaji kama hao. Hata mwanasiasa aliyejipachika cheo cha “mchungaji”, Christopher Mtikila, aliwahi kubebwa na gari lake kusukumwa wakati akiwatia hamasa “walalahoi” na “wavuja-jasho” akiwachochea wawakatae “magabacholi.”
Leo hii wanasiasa hao ni kama wamekwisha, kwani wamefifia kiasi kwamba ni vigumu kukumbuka kwamba waliwahi kuitikisa Dar es Salaam. Je, ni nini kinachowafanya watu wachemke na kuhemka kutokana na wanasiasa mara kwa mara, na nini hasa kinawafanya waonekane wanawapenda na “kuwaabudu” kiasi hicho?
Nitaieleza hali hii kwa mantiki ile ile ambayo naitumia kila mara kuelezea hali nyingine: Nchi hii imo katika zahma (crisis), na imekuwa katika zahma hiyo kwa muda mrefu. Mfadhaiko mkubwa walio nao wananchi unatokana na mambo mengi, maswali mengi yasiyo na majibu. Uchumi wa wananchi si mzuri, maisha yao ni duni, na mbele yao hawaoni dalili za matumaini.
Wananchi wanataraji kupata viongozi wa kuwaongoza kutoka hali hii, lakini hawawaoni. Mara kwa mara wanapewa matumaini hewa, na baada ya muda mfupi wanagundua kwamba wameghilibiwa. Lakini hawaachi na wala hawachoki kuwashabikia wanasiasa wengine kila anapojitokeza mwanasiasa mwingine akatamka maneno yanayoashiria uwezekano wa mabadiliko.
Ndivyo ilivyotokea katika mifano niliyotoa ya Mrema na Mtikila. Kwa kweli ningeweza kwenda mbali zaidi na kusema kwamba ndivyo ilivyotokea kwa marehemu Edward Sokoine katika kpindi kile nchi ikiwa chini ya uongozi wa Mwalimu Julius Nyerere na hali ya uchumi imegeuka kuwa shubiri kutokana na vikwazo vya kiuchumi vya mashirika ya fedha ya dunia.
Ndivyo ilivyo sasa na Edward Lowassa. Kwa sababu ambazo mimi binafsi sizielewi, watu wengi wanamuona Lowassa kama mkombozi fulani. Nasema sizielewi sababu zake kwa kuwa sijui ni nini Lowassa anaweza kufanya ili kubadilisha hali ya umasikini iwe ya neema, hali ya kukata tamaa iwe ya kujenga matumaini, hali ya udhaifu iwe ya ukakamavu na kujiamini.
Nasema hivi kwa sababu nimekuwa mwanafunzi wa historia ya dunia kwa muda mrefu kidogo. Katika kuidurusu historia, sijawahi kuona mtu mmoja, na awe hodari kiasi gani, aliyeweza kubadilisha hali za wananchi wake kwa uwezo wake peke yake. Kila mara maendeleo na mabadiliko ya kweli yameletwa na jamii iliyopevuka, na iliyopiga hatua katika nyanja kuu fulani, na maendeleo na mabadiliko hayo huja hatua baada ya hatua, hatua ya awali ikiwa ni msingi wa kuipokea hatua inayofuata.
Kutaraji kwamba tunaweza kupata mabadiliko ya haraka kutokana na mtu mmoja ni aina fulani ya ushirikina ambayo inanitisha kwa sababu nilikwisha kuibaini ingawa nadhani kwamba watu wetu walio wengi, na jamii yetu kwa ujumla, hatuitambui.
Wale tulio na umri fulani tulikwisha kushuhudia wale wanasiasa wa miaka ya 1990, Mrema na Mtikila. Baadhi yetu tuliowashabikia leo tumebaki tukiona haya tukikumbushwa juu ya ushabiki huo. Hatutaki kukumbushwa kwa sababu leo tunawaona kama walikuwa hawana lolote la maana la kutufanya tuwashabikie kwa kiwango hicho.
Lakini tukumbuke vile vile kwamba ushabiki huu hauna tofauti kubwa na ule tulioushuhudia miaka 10 iliyopita wakati mgombea wa CCM ni Jakaya Kikwete, na kaulimbinu ikiwa “Ari Mpya, Nguvu Mpya, Kasi Mpya!”. Ni kweli kwamba Lowassa alikuwa kinara wa kampeni hiyo na aliifanya kampeni kwa weledi mkubwa. Lakini baada ya Lowassa mwenyewe kujiuzulu kutoka nafasi yake ya juu, hatukuisikia kauli mbinu hiyo, na Kikwete amekuwa na uongozi wenye alama nyingi za kuuliza.
Mzee wa Samunge ni mfano mwingine wa ushirikina wa jamii yetu. Hivi ni nani anaweza kueleza ni sababu gani ilitutia kiwewe kuhusu nguvu ya ajabu ya utibabu wa mzee yule, tuliyemshabikia hadi tukawa kama hatuna akili za kawaida kabisa? Ni nani anaweza kutueleza ilikuwa vipi viongozi wa serikali waliingia wao wenyewe, na kisha wakatuingiza sote, katika upumbavu wa aina ile, upumbavu uliosababisha vifo vya watu wengi walioamini walichokuwa wakiambiwa?
Tatu, tuna tabia ya kukataa kurejea mambo tuliyoyapitia na kuyatafakari ili tupate mafunzo kutokana nayo. Laiti tungekuwa na tabia hiyo leo hii tungekuwa na hazina kubwa ya uzoefu iliyotokana na maisha tuliyoyapitia kwa miaka 50 iliyopita.
Lakini tumekuwa ni jamii ya kuanza upya kila wakati, bila kumbukumbu wala tafakuri. Hayo tumewaachia wasomi, wanazuoni na watafiti wanaoandaa mabuku ya kisomi katika vyuo vikuu. Lakini kwa hili tunapotea kwa sababu bila kuwa na jamii inayosaili yaliyopita hatuwezi kuona yanayokuja.
Ingefaa kurudi nyuma mara kwa mara na kujiuliza ni mambo gani tuliyopitia, ni kwa jinsi gani tulifanya tulivyofanya, ni kwa sababu zipi tulifanya hayo na tukayafanya hivyo hivyo, nini tumejifunza kutokana na hayo na nini ingefaa tufanye ili kuendeleza mema yaliyotokana na tulivyofanya, na vipi tufanye huko tuendako ili kuepukana na maovu tuliyoyafanya wakati ule.
Bila hivyo hatupati maendeleo kwa sababu utakuwa tukirudia kutenda makosa yale yale tuliyoyafanya huko nyuma. Aidha, mafunzo tunayoyapata kutokana na matendo yetu ya kihistoria hayana budi kuwa katika maandiko, kwa sababu hiyo ndiyo njia moja pekee ya kuhakikisha ujuzi unaotokana na uzoefu wetu hautoweki na unaenea kote utakakosomwa na utaendelea kuwapo na kurutubishwa kizazi hadi kizazi.
Wiki ijayo: Edward Ngoyai Lowassa: Hali isiyo ya kawaida huhitaji hatua sisizo za kawaida
VIA RAIA MWEMA
Next Post Previous Post
Bukobawadau